Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RC MACHA AHAMASISHA WANANCHI SHINYANGA KUSHIRIKI KIKAMILIFU ZOEZI LA UANDIKISHAJI WAPIGA KURA OKTOBA 11 - 20, 2024


Na Paul Kasembo, SHY RS.

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amewaomba Wanashinyanga kwa ujumla wao kujitokeza na kushiriki kikamilifu kwenye zoezi la Uandikishaji wa Wapiga kuanzia tarehe 11 - 20 Oktoba, 2024 ili kuweza kuchagua viongozi mbalimbali katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba mwaka huu.

RC Macha ameyasema haya leo tarehe 5 Septemba, 2024 alipokuwa akihutubia wajumbe wa Kikao cha Wadau kilichokuwa kinajadili Mpango wa Matumizi ya Ardhi katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga ambapo pamoja na ombi hili kwa wananchi lakini pia amewakumbusha kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali zitakazotangazwa.

"Niwaombe sana Wanashinyanga, tujitokeze kwa umoja wetu na kila mwenye sifa ya kujiandikisha kupiga kura aende katika maeneo yetu tunayoishi kuanzia tarehe 11 hadi 20 Oktoba, 2024 ili itakapofika wakati wa kuchagua viongozi aweze kutumia vema haki yake hiyo ya msingi," amesema RC Macha.

Aidha, RC Macha amesema kuwa baada ya kujiandikisha pia mwananchi anayo haki ya kugombea nafasi hizo za uongozi kupitia vyama vya siasa na baadae kutafuatiwa na zoezi la Upigaji wa Kura kuwachagua viongozi wa Serikali za Mitaa ifikapo tarehe 27 Novemba, 2024.

Kando na haya, RC Macha amewaomba wajumbe wote waliohudhuria kikao hiki kwenda kusaidia kutoa elimu kwa wananchi, wasaidizi wao na wale wote wanaowazunguka katika maeneo yao ili waweze kushiriki vema katika zoezi hili linalokuja huku akisisitiza kuwa Serikali nayo itaendelea na utoaji wa matangazo ya kuwakumbusha kushiriki kikamilifu wakati ukifika.

Ikumbukwe kwamba, mwaka huu ni wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao utafanyika tarehe 27 Novemba, 2024 nchini kote ambapo viongozi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji watachaguliwa kuongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo ambapo Mkoa wa Shinyanga una jumla ya Mitaa 90, Vijiji 506 na Vitongoji 2749.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com