Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa nishati safi ya kupikia siyo tu ajenda ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan bali ni ajenda ya kuokoa maisha ya watu.
Ameyasema hayo leo Septemba 13, 2024 jijini Dodoma wakati akizindua jengo la Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na kushuhudia utiaji saini wa mikataba ya kuwezesha miradi ya nishati safi ya kupikia.
"Naomba ajenda hii iwe ya watu wote, Serikali inafanya kila linalowezekana kushusha bei ya nishati safi ya kupikia na kuifanya nishati hiyo iweze kupatikana nchi nzima, imeanza kwa kutoa mitungi 400,000 itakayouzwa kwa bei ya ruzuku", amesema Dkt. Biteko.
Akizungumza kuhusu mikataba saba iliyosainiwa, Dkt. Biteko amesema imani ya wananchi ni kuona mikataba hiyo inafanyiwa kazi kwani ni aibu kwa Watanzania kushuhudia utiaji saini huo halafu wasione matokeo.
Aidha, ametoa agizo kwa Wizara ya Nishati na taasisi zake kuwa mfano kwa kuanza kutumia nishati ya umeme wa jua kwenye ofisi hizo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Daniel Sillo amesema ushirikiano baina ya REA na Jeshi la Magereza umewezesha kuanzishwa kwa programu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia magerezani ambayo inatekelezwa katika vituo 211 vya jeshi hilo.
"Programu hii itawezesha upatikanaji wa chanzo kikuu na chanzo mbadala cha nishati safi ya kupikia ambapo gharama za mradi huu ni shilingi bilioni 35.2" ,amesema Sillo.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy amesema jengo hilo limejengwa ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Serikali kuhamia jijini Dodoma ambapo gharama za mradi huo ni shilingi bilioni 9.8.
Aidha, Wakala huo umesaini mikataba saba ya kutoa ruzuku kuwezesha upatikanaji na matumizi ya mifumo ya kisasa ya kupikia kwa Jeshi la kujenga Taifa, Magereza pamoja wananchi.
"Utiaji saini wa mikataba hii ni kielelezo cha dhamira ya dhati ya serikali katika kulinda mazingira yetu pamoja na afya za wananchi",amesema Mhandisi Saidy.
Social Plugin