BARAZA la ushauri la wazee manispaa ya Shinyanga, wamewasilisha mahitaji na mapendekezo yao kwa mbunge wa jimbo la Shinyanga mjini Patrobas Katambi, ambaye pia ni Naibu Waziri ofisi ya waziri mkuu kazi, ajira, vijana na watu wenye ulemavu,ili ayafanyie kazi pamoja na mengine kuyawasilisha ngazi za juu kupitia nafasi yake.
Mwenyekiti wa baraza la ushauri la wazee manispaa ya Shinyanga Stephano Tano, amewasilisha mapendekezo hayo leo Septemba 10,2024 kwa niaba ya wazee wote wa manispaa hiyo.
Ametaja mahitaji na mapendezo ya wazee kwa katibu wa mbunge Samweli Jackson kwa niaba ya Katambi, amesema wazee wanahitaji sheria ya wazee itungwe na siyo kuishi na sera ya mwaka 2003, ambayo haina nguvu katika utekelezaji wa kuhudumia wazee.
Mahitaji mengine ametaja ni wazee wawe na pensheni ya kuwasaidia kama ilivyo kwa wazee Zanzibar, ambao hulipwa kila mwezi sh.50,000, pamoja na kuimarisha mfumo wa bima za afya kwa wazee ili wapate huduma za matibabu bure.
“tunataka pia wazee kuwepo na kitengo cha mikopo kinacho jitegemea katika idara ya maendeleo ya jamii, ili na sisi tupate mikopo ile ya asilimia 10, sababu kuna wazee wenye nguvu wanaweza kukopa na kufanya shughuli za uzalishaji mali,”amesema Tano.
Ametaja mahitaji mengine ni kuwapo na sheria mahususi ambayo itawabana watoto na jamii kuwatunza wazee, kwa ajili ya kuepuka wazee kutelekezwa.
Aidha, ametaja mahitaji mengine kwamba kwenye suala la kikokotoo liboreshwe kwa wazee wastaafu, pamoja na wale wazee wa zamani waongezewe pesheni, na pia kuwepo na idara ya maendeleo ya jamii inayojitegemea na iwe na bajeti ya kuratibu shughuli za wazee.
Mapendekezo mengine ni kwamba wazee wawe wanashirikishwa kwenye vikao vya maamuzi kuanzia ngazi za chini, mabaraza ya madiwani pamoja kuwa na uwakilishi bungeni.
Naye Afisa ufuatiliaji masuala ya wazee kutoka baraza la ushauri la wazee mkoa wa shinyanga Lurent Mihayo,amempongeza Mbunge Katambi kwa kujali wazee, na kwamba wataendelea kuwa naye bega kwa bega.
Katibu wa mbunge Samweli Jackson, amesema Katambi anathamini sana wazee, na amekuwa akikutana nao mara kwa mara kwa ajili ya kupata ushauri na kuchota baraka zao, na pia ameshawapatia majiko ya gesi kwa ajili ya kupata nishati safi ya kupikia.
Amesema mapendekezo ambayo yamewasilishwa na wazee anatayafikisha kwa mbunge Katambi na atayafanyia kazi, sababu ni mbunge ambaye anawapenda sana wazee na kuwathamini.
TAZAMA PICHA HAPA CHINI👇👇
Mwenyekiti wa baraza la ushauri la wazee manispaa ya Shinyanga Stephano Tano akiwasilisha mapendekezo ya wazee.
Mwenyekiti wa baraza la ushauri la wazee manispaa ya Shinyanga Stephano Tano akiwasilisha mapendekezo ya wazee.
Mwenyekiti wa baraza la ushauri la wazee manispaa ya Shinyanga Stephano Tano akiwasilisha mapendekezo ya wazee.
Mwenyekiti wa baraza la ushauri la wazee manispaa ya Shinyanga Stephano Tano akikabidhi mahitaji na mapendekezo ya wazee kwa katibu wa mbunge.
Katibu wa mbunge Samweli Jackson akizungumza kwenye kikao cha wazee.
Picha ya pamoja ikipigwa.
Social Plugin