Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WIKI YA AZAKI KUHAMASISHA JAMII KUSHIRIKI DIRA 2050, UCHAGUZI




Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation For Civil Society FCS- Justice Rutenge, akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Jijini Arusha, kuelekea ufunguzi wa Wiki ya Asasi za Kiraia - AZAKI, inayotarajiwa kuanza rasmi Septemba 9 - 13, 2024 Jijini humo.
Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi Wiki ya AZAKI 2024, Nesia Mahenge, akitoa ufafanuzi wa baadhi ya mambo yatakayojadiliwa katika maadhimisho hayo yatakayofanyika kwa wiki moja Jijini Arusha.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la HAKIELIMU, John Kallaghe, akizungumza katika mkutano huo kuhusu ushiriki wao na mambo watakayofanya katika Wiki hiyo.

PICHA NA; HUGHES DUGILO Na; Mwandishi wetu, ARUSHA.

Ushiriki wa makundi mbalimbali ya kijamii hususan vijana katika kutoa maoni yao kwenye michakato ya Kidemokrasia nchini, umetajwa kuwa moja ya mambo yatakayojadiliwa kwa kina na kufikiwa maazimio ya kuhakikisha makundi hayo yanashiriki kikamilifu katika michakato hiyo.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Foundation For Civil Society FCS- Justice Rutenge, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo Jijini Arusha, ikiwa ni siku moja kuelekea kwenye ufunguzi rasmi wa Wiki ya Asasi za Kiraia - AZAKI, inayotarajiwa kuanza rasmi Septemba 9 - 13, 2024 Jijini humo.

Rutenge amesema kuwa Tanzania ipo kwenye michakato muhimu ya Kidemokrasia inayotoa fursa kwa wananchi kupaza sauti zao hasa kwa watu wanaoishi pembezoni kutoa maoni yao katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, na kushiriki kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu, na uchanguzi mkuu wa 2025.

“Dira ni fursa muhimu sana, na safari hii lazima iaksi maoni, mawazo, matarajio na vipaumbele vya makundi mbalimbali ya wananchi wa Tanzania. Sisi kama AZAKI kwa pamoja tumeshatoa maoni yetu kwenye huu mchakato, na tunaamini kwamba yale yote tuliyoyapeleka yatazingatiwa“ amesema Rutenge.

Ameongeza kuwa katika wiki hiyo kutakuwa na wigo mpana wa ushiriki wa sekta mbalimbali ikiwemo serikali na binafsi, na kwamba kwa pamoja watajadili namna bora ya kushirikiana katika kuwaletea maendeleo wananchi na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza katika mkutano huo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la HAKI ELIMU John Kallaghe, amesema kuwa katika wiki hiyo kutakuwepo na siku maalum waliyoiandaa inayohusu ushiriki wa vijana katika michakato ya kidemokrasia, lengo ni kutambua umuhimu wao kwenye michakato hiyo, na kuwapa fursa ya kujadiliana na kuona umuhimu wao katika kushiriki katika matukio ya kitaifa ikiwemo Dira 2050 na uchaguzi.

Naye Naibu Mkurugenzi Mtendaji, Shirika la Tanzania Bora Initiative - TBI, Ismail Biro, amesema kuwa kupitia njia za Kidijitali katika Wiki hiyo wanaamini sauti za vijana zitaangaziwa kwenye Dira ya Taifa 2050 na kupata fursa ya kuitekeleza kwa sababu ikifika 2050 wengi wao watakuwa watu wazima.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi Wiki ya AZAKI 2024, Nesia Mahenge, amesema wanatarajia kuwa na washiriki zaidi ya 600 kutoka katika AZAKI zaidi ya 400, na kwamba maandalizi yote yamekamalika,.

“Mgeni rasmi kwenye maadhimisho haya anatarajiwa kuwa Waziri wa Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo ambaye atafungua mkutano huu. Na ufunguzi safari hii tutaufanya wa tofauti kidogo kwani hautakuwa wa kusoma risara bali utakuwa ni wa mazungumzo akiwa na rais wa FCS wakijadiliana mada mbalimbali zilizopo kwenye ratiba“ amesema Mahenge.

Maadhimisha hayo ya wiki hiyo yanatarajiwa kutoa fursa kwa Asasi za Kiraia kukutana, kufahamiana na kubadilishana uzoefu, wakijadili masuala mbalimbali yanayohusu AZAKI na mambo mengine ya Kitaifa ikiwemo Dira 2050, Uchaguzi wa Serikali za Mtaa wa 2024,na Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani..

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com