Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HIFADHI MPYA YA ISAWIMA,KUVINUFAISHA KIUCHUMI VIJIJI VINAVYOIZUNGUKA SANJALI NA WAKAZI WAKE

Viongozi mbalimbali wakiwa katika eneo la Isawima
Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Kaliua,Japhael Lufungija,kulia,akikagua eneo la Isawima. Picha na Robert Kakwesi

Na Robert Kakwesi,Tabora

Hifadhi ya wanyamapori ya Isawima, WMA,imejipanga kuwekeza katika biashara ya hewa ya ukaa ili ipate mapato makubwa na kusaidia zaidi vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo katika miradi ya maendeleo.

Hifadhi hiyo iliyokuwa ikijulikana kama Jumuiya ya Isawima,imepewa G.N 442 na Serikali mwishoni mwa mwezi wa tano mwaka huu baada ya kupitia hatua mbalimbali sanjali na misukosuko katika kufikia hatua hiyo.

Katibu wa Isawima Hamis Katabanya ,anasema wanataka Hifadhi hiyo iingize mapato mengi na kuleta neema kwenye vijiji vinavyozunguka kwa wakazi wake kunufaika kiuchumi na kimaendeleo.

“Fedha ambazo tutazipata katika biashara ya hewa ya ukaa ,tunatarajia itakuwa nyingi na wananchi kunufaika pamoja na miradi yao ya maendeleo”Anasema

Katibu wa Isawima ,Hamis Katabanya

Anaeleza kuwa wana mazungumzo na viongozi ,mashirika na taasisi mbalimbali katika kufikia azma yao huku kiongozi mkuu akiwa ni Serikali kuu pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii na idara ya Wanyamapori.

Hifadhi ya Isawima iliyopo Wilayani Kaliua,ina eneo la kilomita za mraba 291 na vijiji 15,ilianzishwa mwaka 2007 na vijiji 11 vilivyotenga ardhi yenye eneo la kilomita za mraba 1,597.3 kwa lengo la kuhifadhi mazingira na kunufaika na rasimali zilizopo kwenye eneo hilo,wakiwemo wanyamapori.

Hata hivyo kutokana na usimamizi duni,eneo hilo lilivamiwa na wafugaji pamoja na wakulima na kusababisha Serikali kuridhia kupandisha hadhi eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,367.14 kuwa pori la akiba Igombe,lililoanzishwa kwa tangazo la Serikali Namba 455 la 26 Novemba mwaka 2022 mbapo eneo lenye kilomita za mraba 291.8,zilibaki nje na ndilo lililotangazwa kuwa Jumuiya ya Hifadhi ya wanyamapori Isawima na kusajiliwa rasmi 31 may 2024 kama jumuiya iliyoidhinishwa kisheria,ikiundwa na vijiji vya Limbula,Tuombe Mungu,Kombe,Imalampaka,Kamsekwa,Mpwaga na Mtakuja Mashariki.

Vingine ni Mtakuja Magharibi,Kazana upate,Wachawaseme,Ugansa,Usinge,Luganjo,Malanga na Limbula Siasa.

Katabanya anaeleza kuwa kabla ya kuwa Hifadhi,ikiwa jumuiya ilifanikiwa kusaidia vijiji kwa kuvipa vifaa vya ujenzi kwa ajili ya shule,zahanati pamoja na fedha na kwamba baada ya kuwa Hifadhi ya Isawima,wanataka kuona mambo makubwa yanafanyika kwenye vijiji na wakazi wake.

Awali jumuiya hiyo ilipitia changamoto mbali mbali,zikiwemo za uvamizi wa eneo kwa shughuli za binadamu,ujangili,migogoro ya mipaka,kutokuwepo mpango wa matumizi bora ya ardhi na mauaji ambayo yalisababishwa na waliovamia eneo hilo kuuana wenyewe kwa wenyewe kwa kugombea maeneo au katika mapambano dhidi ya vyombo vya usalama ambapo pande zote mbili ziliathirika.

Katabanya anasema hayo yote bada ya kuwa Hifadhi yatakuwa historian na sasa wanajiandaa kuwa hifadhi ya mfano nchini ambayo wananchi na vijiji vinavyoizunguka watanufaika kiuchumi na kimaendeleo.

Anaeleza kuwa mbali ya kuingiza fedha kupitia biashara ya hewa ya ukaa,watapata fedha kupitia shughuli za uwindaji  na Utalii

Anaeleza kuwa watagawa mapato kwa Serikali Kuu,Halmashauri ,Isawima yenyewe pamoja na taasisi tanzu zitakazokuwepo.

Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Kaliua,Japhael Lufungija ambaye halmashauri yake ilishiriki katika mchakato wa kuifikisha ilipo,anasema wanataka kuona manufaa kwa hatua iliyofikia na kuona vijiji na wnaanchi wananufaika.

Anaeleza kuwa tayari wameipitishia mipango yake ikiwemo matumizi bora ya ardhi kwenye eneo husika sanjali na vijiji vinavyozunguka na kwamba migogoro iliyokuwepo imeshughulikiwa ikiwemo ya mipaka.

Viongozi Wilaya ya Kaliua wakiangalia eneo la Isawima.

“Tunataka kuona vijiji vinanufaika na wakazi wake ili wengine waje kujifunza kutoka kwetu na wenyewe nao wanufaike”Anasema.

Lufungija anaeleza kuwa halmashauri yake imekuwa ikinufaika na baadhi ya rasimali ikiwemo misitu ambayo imekuwa ikiingizia halmashauri fedha nyingi na kuwa wataendelea kunufaika na rasilimali nyingi zilizopo zikiwemo zilizo kwenye Hifadhi ya Isawima yenye wanyamapori wa aina mbalimbali,wakiwemo tembo,chui,nyati,twiga pamoja na ndege mbalimbali .

Mkurugenzi msaidizi idara ya wanyamapori Pellage Kauzen,anasisitiza rasilimali kwenye eneo hilo kutunzwa na wananchi kunufaika na eneo hilo.

Anasema lengo la Serikali mbali ya kuhifadhi mazingira lakini pia kuhakikisha rasilimali za nchi zinatunzwa kwa maendeleo endelevu kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.

“Sisi tumeridhishwa na waliotutangulia hivyo tunapaswa kuhakikisha nasi tunawaridhisha watakaokuja baada yetu”Anasema

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kaliua,Dk Rashid Chuachua ambaye sasa yupo Mkoa wa Kigoma ,wilaya ya Kigoma,anasema ana matumaini makubwa Hifadhi hiyo kuwanufaisha wananchi na vijiji vyao hasa wakifanya biashara ya hewa ya ukaa.

“Biashara ya hewa ya ukaa itawapa fedha nyingi ambazo watazitumia katika shughuli za kiuchumi pamoja na maendeleo,hivyo kutokuwa na kelele za kuchangia miradi ya maendeleo”Anasema

Mkazi wa kijiji cha Wachawasema,Ibrahim Haruna,anaeleza furaya yake kwa Jumuiya kufikia hatua hiyo,akisema anaona mabadiliko yake kimaisha muda sio mrefu ujao.

“Tulinufaika na uwepo wa jumuiya lakini sio sana ,lakini kwa sasa tuna matumaini makubwa kwani tutapata fedha nyingi kutokana na mpango uliopo”Anasema

Naye Mwanaidi Isihaka,anaeleza kufurahia kupatikana hifadhi ya Isawima,akisema ni jmbo zuri kwao,kwani wanatarajia makubwa kuliko ilivyokuwa jumuiya ya Isawima,akieleza kutokana na udhibiti unaofanyika,wanyama watatulia na kuongezeka kwa wingi na kupata watalii wengi watakaoingiza fedha kwenye Hifadhi.

‘fedha tutapata kupitia baadhi ya maeneo ikiwemo utalii wa uwindaji na picha pamoja na hewa ya ukaa,jambo litakalobadilisha maisha yetu”Anasema

Eneo hilo linazungukwa na vijiji vyenye huduma mbalimbali za kijamii zinazowezesha jamii na wageni kupata huduma husika au kuchangia maendeleo ya jamii,zikiwemo shule za msingi 23,sekondari 6,zahanati 8,mashine za kusaga na kukoboa nafaka mbalimbali 112,masoko ya vijiji 15 na maghala ya kuuzia tumbaku na kutuznia nafaka mbalimbali.

Huduma zingine ni maduka ya dawa baridi 69,vituo vya afya 2,vituo vya polisi 2,maduka ya pembejeo za kilimo na mifugo 20,huduma za kifedha 87,nyumba za kulala wageni 41,vyama vya msingi vya tumbaku 21,vituo vya kuuzia mafuta ya petrol na dizeli 2 na huduma zinginezo.

Madhumuni ya kuanzishwa kwa Jumuiya ya Isawima baadhi ni pamoja na kutekeleza uhifadhi uliojikita kwenye jamii,kuamsha ari ya wananchi ili washiriki katika uhifadhi wa wanyamapori,kuhamishia jukumu la kuzuia matuizi haramu ya wanyamapori katika eneo hilo na kwa jamii pamoja na kutoa mafunzo na msaada kwa viongozi wake na askari wa wanyamapori wa vijiji,ili waweze kulinda wanyamapori chini ya utaratibu wa uhifadhi uliojikita katika jamii.

Madhumuni mengine ni kuhamishia jukumu la usimamizi wa wanyamapori wanaopatikana katika makazi ya watu nan je ya makazi ya watu,kwa jamii za vijijini na kuruhusu jamii za vijijini kunufaika kutokana na matumizi endelevu ya rasilimali za wanyamapori zinazopatikana katika maeneo ya vijiji kwa utaratibu maalum.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com