Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BINTI ADAIWA KUJIUA KWA KUJINYONGAA KABLA YA HARUSI... AKUTWA AMEKUFA CHINI YA MKWAJU AKIWA KAMBA SHINGONI

Na Mapuli Kitina Misalaba

Binti mwenye umri wa miaka 19, Eva (Nyanzobe) Ngasa Seni, mkazi wa Kitongoji cha Mwangingingi, kijiji cha Mwajipugila, kata ya Busangwa, Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, amefariki dunia kwa kile kinachoelezwa kuwa amejinyonga kwa kutumia kamba ya neti kwenye mti wa ukwaju leo Oktoba 16, 2024.

Baba wa marehemu, Ngasa Seni, alielezea jinsi alivyopokea habari za tukio hilo ambapo amesema kuwa tukio hilo limemtokea kwa ghafla na hakuwa na dalili zozote za tatizo hilo na kwamba yeye alikuwa ameaga familia asubuhi ya leo kwenda kwenye shughuli zake za kila siku.

"Hili tukio limenishtua sana nilikuwa nimetoka kidogo nyumbani, nikaelekea Old Shinyanga muda wa saa saba mchana nikiwa huko, nilipigiwa simu na majirani wakisema kuna tukio limetokea nyumbani kwangu. Niliporudi nikakuta mtoto wangu Eva amejinyonga kwa kutumia kamba ya neti kwenye mti wa ukwaju. Hali hii imenishangaza, kwani asubuhi tumesalimiana vizuri, nikawaaga nikiwa naenda kwenye shughuli zangu za kila siku. Sijajua sababu ya kujinyonga kwake, na kifo hiki kimeniingia kwa mshangao mkubwa.”amesema baba wa marehemu

Ngassa pia ameeleza kuwa Eva alikuwa na mipango ya ndoa mwezi huu.

"Mtoto wangu alikuwa anatarajia kufunga ndoa mwezi huu, na tulikuwa na maandalizi ya harusi Eva alizaliwa tarehe 25 Mei, 2005, na alikuwa na umri wa miaka 19 alimaliza kidato cha nne mwaka jana, 2023. Mpaka sasa, sijajua sababu ya kujinyonga kwake."amesema baba wa marehemu

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mwangingingi, Jonas Nkilijiwa Ihano, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza jinsi alivyopokea taarifa hizo.

"Nilipokea taarifa majira ya saa tisa alasiri kwamba kuna binti amejinyonga nilipofika eneo la tukio nilikuta watu wamekusanyika, na yule binti alikuwa tayari amefariki dunia inasemekana alitumia kamba ya neti kujinyonga, lakini ile kamba ilikatika na mwili wake ukaanguka chini hata hivyo, tulipomkuta tayari alikuwa amefariki."amesema Mwenyekiti wa kijiji

Eva alikuwa akifanya kazi za nyumbani leo mchana amepika chakula, kisha akaenda kuchota maji lakini hakuchukua ndoo ambapo Msichana mwingine aliyekuwa akienda kuchota maji alimuona Eva akiwa amelala chini ya mti wa ukwaju, akiwa na kamba shingoni alipojitahidi kumsogelea, alibaini kuwa Eva alikuwa amejinyonga na tayari amefariki dunia.

Marehemu Eva alizaliwa tarehe 25 Mei, 2005, na alikuwa na umri wa miaka 19, alimaliza kidato cha nne mwaka jana, 2023, na alikuwa akitarajia kuingia kwenye hatua mpya ya maisha yake.

Chanzo- Misalaba Media

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com