MKUU wa Mkoa wa Tanga Balozi, Dkt. Batilda Buriani ataongoza wananchi mkoani humo kwenda kujiandikisha kwenye daftari la mpiga kura, zoezi litakaloanza Oktoba 11, majira ya saa mbili asubuhi hadi saa 12 jioni.
Akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake Dkt. Buriani amesema atafanya zoezi hilo akiwa sambamba na viongozi wote wa Mkoa huku akihimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kuungana nae kwenye kujiandikisha.
Amesema zoezi hilo litaanza Octoba 11 hadi 20 na ni hatua ya kuelekea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa zitakazosaidia kuwapata viongozi wa vitongoji, vijiji na mitaa ambao watu watachagua kwa ridhaa yao.
"Kitaifa zoezi hili linazinduliwa rasmi na Mh. Rais Dkt. Samia Sulluh Hassan pale Chamwino, Dodoma, na sisi huku kwenye Mikoa yetu, Tanga tutakwenda kushiriki zoezi hili katika maeneo yetu ambayo violngozi wanaishi,
"Kwa hiyo Mimi mkuu wa Mkoa nitapanga foleni kwenye eneo langu na kuungana na wakazi waliopo kwa ajili ya kujiandikisha, vile vile na viongozi wengine wa Mkoa pamoja na wakuu wote wa Wilaya tutashirikiana na wananchi kufanikisha zoezi hili " amefafanua.
Lakini pia amesema watahikisha zoezi hilo linafanyika kiuweledi na kiusalama na kwamba siku 10 zilizotolewa kwa ajili ya uandikishaji zinatosheleza ikijumuishwa na siku 7 za uhakiki wa taarifa ya kila mtu kwenye daftari hilo.