HALMASHAURI YA JIJI LA TANGA YAONGEZA MUDA WA MAOMBI KWA WANAWAKE, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU


Na Hadija Bagasha - Tanga

Halmashauri ya jiji la Tanga imeongeza muda wa maombi ya mikopo kwa Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu ili kupata idadi ya wakopaji inayolingana na kiasi cha bilioni tatu ambazo zimetengwa na serikali kwa ajili ya kuyawezesha makundi hayo kiuchumi.


Akizungumza na waandishi wa Habari jijini Tanga kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Mhandisi Juma Hamsini, Mkuu wa Idara ya maendeleo ya jamii, Simon Mdende amesema kwamba muda ulioongezwa ni siku 14 pekee kutoka tarehe 27 mwezi octoba hadi Novemba 10 mwaka huu.

Amesema hatua hiyo imekuja kufuatia muingiliano wa masuala ya uchaguzi wa serikali za mitaa sambamba na kutoa fursa kwa wananchi wengine ambao hawakuweza kushiriki zoezi hilo hapo awali.

Mdende amebainisha kuwa mpaka sasa Vikundi zaidi ya 340 katika Halmashauri ya jiji la Tanga vimepeleka maombi kwajili ya kusajili kwenye dirisha la mikopo hiyo ya asilimia 10 ambapo wanawake ni vukundi 211, Vijana 119 na wenye ulemavu vikiwa 10.

"Tumeongeza dirisha kwa muda wa siku 14 pamoja na kuongeza dirisha hili lakini bado tumepata mafanikio sababu mpaka sasa jumla ya vikundi 340 vimeleta maombi kwajili ya hatua ya kwanza ya usajili na hatua ya pili ni kuomba mkopo, ukiangalia uwiano bado kuna nafasi kubwa hususani kwa vijana na watu wenye ulemavu kwajili ya bilioni 3 tulizotenga,"amesisitiza Mdende.


"Kilichobaki ni wananchi kuendelea kujitokeza katika dirisha kwani tunamshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza umri kwa vijana katika mikopo hii hapo awali walikuwa wanachukua miaka 18 - 35 lakini hivi sasa ni miaka 18 - 45 na hii ni kwajili ya kusaidia vijana waweze kupata mikopo itakayowawezesha kujikwamua kiuchumi, "amesema Mdende.

Aidha Mdende ametolea ufafanuzi kuhusu mikopo hiyo kwamba hapo awali ilikuwa ikiwalazimu wanakikundi kufanya biashara moja ambapo hivi sasa ni tofauti kanuni imetoa mwanya kwa wanakikundi kila mmoja kuwa na biashara yake kwa kuandika mchanganuo wa biashara yake, gharama na namna zitakavyotumika.

Ameongeza kuwa baada ya mchanganuo kufanyika kwa kila mwanakikundi wataunganisha michanganuo yote na kupata andiko moja lenye thamani ya fedha wanazohitaji wanakikundi ambapo baada ya kamati zinazotembelea kujiridhisha kuwa wanasifa ya kupata mkopo fedha hizo zitaingia katika akaunti ya kikundi husika.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post