Watoto 25,890 wameondolewa katika utumikishwaji na kaya 1,124 zikianzisha shughuli za ujasiriamali na biashara ndogo ndogo za kuongeza kipato kupitia vikundi 56 vilivyoanzishwa na kusimamiwa na mradi wa Prosper Reset katika Wilaya tano nchini kwenye mikoa ya Mbeya (Chunya),Songwe (Songwe)na Tabora(Sikonge,Urambo na Kaliua).
Mradi huo unaolenga kuwaondoa watoto kwenye kazi hatarishi na zisizo na staha,ulianzishwa mwaka 2011 na kutekelezwa katika wilaya tatu za Mkoa wa Tabora na mwaka 2018 kuongezwa wilaya za Chunya na Songwe.
Meneja wa mradi wa Prosper Reset,Fredrick Malaso anaeleza Katika mkoa wa Tabora,kilimo ni mojawapo ya shughuli kuu ya uzalishaji mali na hivyo inatambulika watoto wengi kushiriki katika shughuli mbalimbali za kilimo ambapo baadhi ya shughuli hizo zinakuwa hatarishi kwa mtoto.
Anaeleza kuwa kuanzia mwaka 2021 mradi wa Prosper Reset unaoendelea kutekelezwa sasa, unalenga kuchangia kukuza uchumi jumuishi na endelevu unaoongeza ajira na kazi zenye staha huku mafanikio mengi yakipatikana kutokana na utekelezaji wa mradi huo.
“Mradi umekuwa na mafanikio makubwa na kupokelewa vizuri na wakazi wa maeneo mradi uliopo kwenye wilaya hizo tano kwa sasa”Anasema
Utafiti uliofanyika mwaka 2020/21(Tanzania Integrated labour force survey,ILFS,) ulionesha kuwa vitendo vya utumikishwaji watoto vimeendelea kuathiri watoto wapatao milioni 5.02 wenye umri wa miaka 5-17 sawa na asilimia 24.9.Pia utafiti huo ulibainisha kuwa asilimia 83.7 ya matukio ya utumikishaji yanafanyika katika sekta ya kilimo,misitu na uvuvi.
Ikumbukwe kuwa Tanzania ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa na Shirika la kazi Duniani,ILO, ambapo imeridhia mikataba kadhaa ukiwemo mkataba wa umoja wa Mataifa kuhusu haki za mtoto ya mwaka
1989,mkataba kuhusu ajira mbaya kwa watoto,mkataba namba 138 unaohusu umri wa chini wa mtoto kuajiriwa na mkataba namba 182 unaohusu kazi hatarishi zisizoruhusiwa kufanywa na mtoto(worst forms of child labour convention C182.mikataba yote hiyo inalenga kuwalinda,kuwatetea na kuendeleza haki za watoto.
Mtaalamu wa mradi wa prosper Reset Leah Masolwa anaeleza kuwawezesha waliotumikishwa kwenye maeneo yanayolima tumbaku kwa kuwapa ujuzi na vifaa ,ujuzi ambao unawasaidia katika maisha yao.
Anaeleza kuwapatia vyerehani na vifaa vinavyoendana na ujuzi waliopewa na hivyo kufanya kazi na kujipatia kipato ambacho kinawafanya kuondokana na kufanya shughuli hatarishi.
“Ujuzi ambao tumewapa umewafanya wafanye kazi za staha zinazowaingizia kipato na kuachana na shughuli hatarishi”Anaeleza
Vijana waliopewa ujuzi na shirika la Prosper reset na kupatiwa vitendea kazi, wanakiri kunufaika na mradi huo ambao mbali ya kuwafanya waingize kipato pia umewaondoa kufanya kazi hatarishi.
“Nimejifunza ufundi cherehani na sasa ni fundi mzuri ambaye nawashonea watu na kuingiza kipato kinachonisaidia”anaeleza
Pia anabainisha kuwa yeye kwa sasa ni mwalimu wa kutoa elimu kuhusu athari za utumikishwaji watoto kwa jamii na amepokelewa vizuri.
Simon Cornel anaeleza kupata ujuzi wa kutengeneza pikipiki na kwamba alikuwa na changamoto ya ukosefu wa vifaa ambavyo anashukuru amepatiwa na mradi huo wa Prosper Reset.
“Nina ujuzi wa kutengeneza pikipiki ambao unanisaidia kuingiza kipato ingawa awali nilikuwa sina vifaa lakini nashukuru mradi kuniwezesha kuvipata”anasema
Mwingine aliyenufaika na mradi huo ni Simon Benedict ambaye ni fundi ujenzi aliyepewa vifaa kutokana na ujuzi wake alioupata kupitia mradi huo.
Afisa tarafa wa Urambo,Majura Lusato,anataka watoto kutotumikishwa kwani ni kosa huku akisisitiza jamii kuachana na tabia ya kuwatumikisha watoto ikiwemo kwenye mashamba ya tumbaku.
Anasema baadhi ya wazazi na walezi wamekuwa wakiwatumikisha watoto katika mashamba ya tumbaku ,kuanzia uandaaji na uwekaji wa madawa na hivyo kuhatarisha usalama na afya zao.
“Nawaombeni sana acheni kuwatumikisha watoto katika kazi hatarishi kwani ni kosa ambalo linaweza kuwaingiza matatani”anasema
Kwa upande wake afisa kazi mkoa wa Tabora,Muhenga Richard,anaeleza Kazi ambazo mtoto hatakiwi kuzifanya kwa mujibu wa sheria kuwa ni nyingi zikiwepo za kwenye migodi,uwekaji madawa mashambani na kazi zingine za hatari kwa ustawi na usalama wa mtoto.
Wawakilishi wa makampuni ya ununuzi wa tumbaku, wanaunga mkono watoto kutotumikishwa ikiwemo kwenye mashamba ya tumbaku na kwamba wanatoa elimu kwa wakulima kuhusu athari za kutumikisha watoto.
Mwakilishi wa kampuni ya Mkwawa Leaf Tobacco, Lawrance Safari,anaeleza kampuni ya Mkwawa kuwa inapinga utumikishwaji watoto na inatoa elimu ya madhara ya utumikishwaji mtoto katika kilimo cha tumbaku.
“Hatuungi mkono kabisa kitendo cha mtoto kutumikishwa huku tukitoa elimu kuhusu madhara yake kwa mtoto “Anaeleza
Karagho Huruma ambaye ni mwakilishi wa kampuni ya JTI, anabainisha kuwa wanatoa elimu endelevu kuhusu madhara ya kutumikishwa mtoto ambayo inapokelewa vizuri na jamii ya wakulima wa tumbaku.
“Pamoja na changamoto ya baadhi kuwa wagumu kuelewa lakini wengi wanatuelewa na hilo tunaendelea kulifanya pasipo kuchoka”Anasema
Kwa upande wake mwakilishi wa kampuni ya Alliance One, Kelvin Pesambili, anabainisha kuwa elimu ya madhara ya utumikishwaji mtoto ndio muhimu ili kuhakikisha hatumikishwi na kushindwa kupata stahiki zake kama mtoto.
“Lazima tuhakikishe mtoto anakuwa salama katika makuzi yake pasipo kufanyishwa kazi za hatari ili akue kwa kimo , akili na afya njema”Anasema
Katika kuhakikisha watoto wanakuwa salama na kutotumikishwa ,ndio maana kuna Siku ya kupinga na kutokomeza utumikishwaji wa mtoto Duniani ,ikiwa ni matokeo ya Azimio la shirika la Kazi Duniani,ILO, lililopitishwa mwaka 2002 na kufanya kila ifikapo Juni 12 kila mwaka kuadhimishwa Duniani kote.
Mradi wa Prosper Reset unapaswa kuungwa mkono ili uzidi kupinga na kutokomeza utumikishwaji wa mtoto katika kazi hatarishi, ambao ni kinyume cha sheria za nchi na mikataba ya Kimataifa ambayo Nchi imeridhia kuhusu Haki za Mtoto.