TAMWA, TCRA WAZINDUA 'SAMIA KALAMU AWARDS 2024' ....'Uzalendo Ndio Ujanja'


Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA Dkt. Rose Reuben akizungumza wakati wa kutangaza  Mashindano ya Tuzo za Waandishi wa habari za maendeleo 'Samia Kalamu Awards'  zenye kauli mbiu ya 'Uzalendo ndio Ujanja'  Kushoto ni Meneja Huduma za Utangazaji TCRA Mhandisi Andrew Kisaka

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) wametangaza rasmi Mashindano ya Tuzo za Waandishi wa habari za maendeleo 'Samia Kalamu Awards' zenye kauli mbiu ya 'Uzalendo ndio Ujanja' zikiwa na lengo la kuchochea uandishi wa makala zilizofanyiwa utafiti na uchambuzi kuhusu maendeleo, uwajibikaji, uzalendo na kujenga chapa na taswira ya nchi ya Tanzania.

Akizungumza wakati wa kutangaza tuzo hizo, leo Jumapili Oktoba 13,2024 katika ukumbi wa Serena Hotel Jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA Dkt. Rose Reuben amesema tuzo  zitahusisha maudhui yaliyochapishwa kupitia magazeti, redio, televisheni, majukwaa ya mtandaoni akisisitiza kuwa ni tuzo maalumu kwa vyombo vya habari na maafisa habari wa serikali.

"Tuzo hizi  zilizoandaliwa na TAMWA na TCRA zitahusisha habari zilizochapishwa kati ya Januari 1 hadi Oktoba 26,2024. Tuzo hizi zitatolewa kwa wanahabari Watanzania kwa lengo la kuhamasisha, kuhimiza na kukuza wigo wa uchakataji, utangazaji na uchapishaji maudhui ya ndani kupitia vyombo vya habari",ameeleza Dkt. Rose.
Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA Dkt. Rose Reuben akizungumza wakati wa kutangaza Mashindano ya Tuzo za Waandishi wa habari za maendeleo 'Samia Kalamu Awards' 

"Kutokana na maendeleo ya teknolojia na utandawazi, uandishi wa habari nchini umekuwa ukijikita kwenye kuburudisha, kuhabarisha huku uandishi wa makala za kuelimisha zikiwa kwa kiwango kidogo lakini pia vyombo vya habari nchini vimekuwa vikitangaza maudhui ya nje yasiyokidhi mahitaji ya hadhira ya Kitanzania.

Na kwa muktadha huo, TAMWA kwa kushirikiana na TCRA tuliamua kutoa mafunzo maalumu kwa waandishi wa habari, watangazaji , wahariri,mameneja, maafisa habari, wamiliki wa vyombo vya habari, wahadhiri na watengeneza maudhui wa mitandaoni wapatao 2,054 kote nchini kwa kipindi cha miezi mitatu mwaka huu 2024",ameongeza Dkt. Rose.

Amefafanua kuwa, pamoja na mafunzo hayo wameona ni vyema kutoa tuzo kwa wanahabari pamoja na vyombo vya habari ambao wamekuwa wakifanya jitihada za kuandika, kuchapisha na kutangaza maudhui ya ndani hasa makala zilizofanyiwa utafiti na uchambuzi wenye tija kwa watanzania.

"Tuzo hizi zimepewa jina la Samia Kalamu Awards ili kutambua na kuenzi historia ya kuwa na Raiss wa kwanza mwanamke nchini Tanzania na zinatarajiwa kutolewa Novemba 2024 zikiwa katika makundi matatu ambayo ni Tuzo Maalum za kitaifa, Tuzo kwa vyombo vya habari na Tuzo za Kisekta",amesema Dkt. Rose.

Amevitaja vigezo vya ushiriki kuwa ni Makala zinazoshindanishwa ziwe zinahusu masuala ya maendeleo yanayogusa maisha ya wananchi na fursa zinazopatikana kutoka kwenye miradi mbalimbali.
Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA Dkt. Rose Reuben.

VIGEZO VYA USHIRIKI

"Makala hizo ziwe zimechapishwa, kutangazwa au kurushwa kwa lugha ya Kiswahili au Kiingereza kwenye vyombo vya habari vya ndani au nje ya Tanzania. Aidha mwandishi awe Mtanzania na makala iwe imefanyiwa utafiti na uchambuzi wa kina. Vyanz vya habari visipungue vinne na makala hazipaswi kuwa zimeshawahi kushindanishwa kwenye tuzo nyingine",amefafanua Dkt. Rose.

"Kwa kuzingatia ulinzi wa haki miliki, kazi zote zitakazowasilishwa kwa ajili ya mashindano ni lazima ziwe za kipekee na zifuate masharti ya hakimiliki ya mwandishi na kituo kilichotangaza",amesema.

UPIGAJI KURA

Amesema mchakato wa upigaji kura utahusisha wananchi kwa asilimia 60 na majaji kwa asilimia 40, kura zitapigwa kupitia SMS SHORT CODE namba 15200 kupitia simu na kutumia tovuti ya https://samiaawards.tz kwa mawasiliano zaidi tembelea tovuti https://samiaawards.tz

"Matarajio yenu ni kwamba Samia Kalamu Awards zitahamasisha uandishi wa habari unaozingatia weledi, maadili, kukuza maendeleo ya Tanzania na uzalendo hivyo kila mwanahabari anatakiwa kutumia fursa hii kuwasilisha kazi kupitia  tovuti ya https://samiaawards.tz",amesema.
Meneja Huduma za Utangazaji TCRA Mhandisi Andrew Kisaka

Kwa upande wake, Meneja Huduma za Utangazaji TCRA,  Mhandisi Andrew Kisaka akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt. Jabiri Bakari amesema lengo la tuzo hizo pia ni kuhakikisha waandishi wa habari wanaandika makala zenye maudhui bora na zenye kuleta mabadiliko.

“Hizi ni tuzo za kipekee kwa sababu vyombo vya habari vyote vitashindishwa, maafisa habari nao watashindanishwa hivyo ni chachu kubwa kwa vyombo vya habari na waandishi wa habari kufanya kazi kwa weledi zaidi. Zitaleta matokeo chanya katika tasnia ya habari, Tunataka waandishi wa habari wanaoandika habari zenye kuleta mabadiliko 'Quality local contents' lengo ni kuongeza kiwango bora cha maudhui ya ndani", ameongeza Mhandisi Kisaka.











Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post