Makundi ya ndege aina ya Flamingo katika Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara.Picha kwa hisani ya Hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara
Na Phinias Bashaya -Bukoba
Hili ndilo tukio la kusisimua zaidi analotarajia mtalii wa maisha ya ndege pori,Kuamshwa alfajili na sauti mseto za mashindano ya nyimbo zinazotokea juu ya miti.
Sauti hizo humpa mtalii hakikisho la kupata picha za kutosha za ndege tofauti wakati wote wa safari. Sauti zinatoa ujumbe wa kuwepo uhai wa mazingira na viumbe vyake.
Sio kila nchi inaweza kuwa na matukio ya aina hii, isipokuwa Tanzania nchi yenye mifumo asili ya kiikolojia inayoratibu uhusiano mwema wa viumbe na mazingira yao.
Safari za kupokea wageni wanaofika kufanya utalii wa ndege haziwezi kukoma leo, kwa sababu ndege wengi wa porini hawafugiki,ni lazima uwakute kwenye mazingira yao ya asili.
Hata hivyo kuna tishio kubwa linalowakabili ndege hao kwa sasa,kutokana na uharibifu wa mazingira.Hiki ni kilio cha binadamu,ndege na wanyama.Mimea inapukutisha majani kwa wingi ili kubana matumizi ya maji sababu ya ukame.
Tishio hili linaanzia vijijini ambapo zamani,ndege kama kware na kanga walifika hadi kwenye kiambaza cha nyumba,mazingira yalikuwa rafiki,upande wa pili kuna uhasama wa binadamu na wanyama pori.
Hali hii tayari imewashtua wataalamu wa maisha na tabia za ndege,ambapo Dkt. Jasson John kutoka Idara ya Zoolojiia na Wanyamapori Chuo Kikuu Dar es Salaam,anasema kuna mifano hai ya ndege walioanza kupotea kutokana na uharibifu wa mazingira.
Mtaalam huyo ambaye ni mbobezi katika tafiti za maisha na tabia za ndege,anamtaja korongo nyangumi kuwa yuko hatarini kutoweka,kama jitihada za kulinda maisha yake hazitakuwa maradufu.
Mkazi wa Kisiwa cha Musira kilichopo Ziwa Victoria Manispaa ya Bukoba Mikoani Kagera akiharibu viota vya ndege.Picha na Phinias Bashaya
"Maeneo yao mengi ya asili yalivamiwa na mifugo, hupenda kujenga kiota mfano wa mtumbwi ardhini, mayai yao yanaharibiwa kuhusu chakula chao hupenda kuwinda samaki kando ya mito na mabwawa",anasema Dkt John
Mtaalam huyo anasema, kuanzishwa kwa hifadhi za Taifa Burigi Chato na Kigosi ni habari njema kwa kuwa ni makazi ya asili ya ndege hao.Mdomo wao mkubwa mfano wa kiatu huwapa sifa ya ziada.
Aidha ameandika vitabu tofauti kuhusu maisha na tabia za ndege, miongoni mwake ni kitabu kiitwacho"The Birds of Western Tanzania"au ndege wa Magharibi mwa Tanzania, kinatumika kama rejea maeneo mengi duniani.
Korongo nyangumi(domo kiatu)anaishi ukanda wa Kagera na Kigoma pekee hapa nchini, chakula chake kikuu ni samaki wa kwenye mito na mabwawa vilivyoathiriwa na uharibifu wa mazingira.
Uzuri wa Hifadhi ya Taifa ya Kitulo haunogi biila ndege aina ya tandawala(Denhams Bustard)ambaye sifa yake kubwa ni kusafiri mwendo mrefu angani kutoka bara moja hadi jingine.
Ndege huyo huvuta wageni kufanya utalii wa kupiga picha katika hifadhi hiyo, ambapo sababu zozote za uharibifu wa mazingira zinaweza kuwakimbiza ndege hao na itakuwa vile vile kwa watalii.
Tayari hifadhi inakabiliwa na changamoto za miti na vichaka vamizi, vinavyoathiri mito na vijito na inatishia uhai wa mimea ya asili na viumbe hai waliomo.
Hifadhi ya Taifa Serengeti ni makazi ya maelfu ya ndege.Sehemu ya picha zake zimetengeneza maudhui kwenye Filamu ya "The Royal Tour" ambayo muongoza watalii kinara ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan
Filamu hiyo inawaeleza wageni kwamba Serengeti ni chaguo bora zaidi la kufanya utalii wa kupiga picha za ndege na wanyama wa porini.Kuna ndege mnana na jamii zote za tai na korongo.
Maajabu katika filamu ya "The Royal Tour"yanatajwa kote duniani. Katika mtandao wa www.dumasclarion.com wa Marekani,Mwandishi wa Shirika la Associated Press(AP)David Bauder,katika makala yake anamtaja Rais Samia Suluhu Hassan ,kama muongoza watalii kinara anayeifungua nchi kupitia filamu hiyo.
Watalii wakiangalia ndege kutoka jukwaani katika Hifadhi ya Ziwa Manyara.Picha kwa hisani ya Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara
Anasema ni kiongozi aliyebeba wajibu wa kuieleza dunia kuhusu usalama wa wageni watakapofika nchini hasa baada ya janga la virusi vya COVID 19,ambavyo vilidhoofisha sekta ya utalii na mifumo mingine ya dunia.
Aidha makala hiyo imenukuliwa katika mtandao wa www.nzherald.co.nz wa New Zealand ,huku wageni wengi wakimiminika baada ya kuona vivutio ndani ya filamu hiyo.Kuwaona ndege ambao chakula chao, hupatikana kwenye migongo ya wanyama.
Baadhi ya watalii waliofika nchini kwa mara ya kwanza baada ya filamu hiyo kuzinduliwa wanaeleza hisia zao,kupitia mtandao maarufu wa www.tripadvisor.comNi jukwaa la watalii Kimataifa.
Pia kupitia mtandao huu,maelfu ya watalii hulitumia kupiga kura kupitisha vivutio bora zaidi duniani,
Tuzo zinazoratibiwa na Taasisi ya World Travel Awards kila mwaka
Tarehe 18,Oktoba 2024 Serengeti ilitangazwa kuwa Hifadhi bora Afrika, ukiwa ni ushindi wa sita mfululizo huku Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro ikitajwa kuwa kivutio bora zaidi Afrika.
Kupitia mtandao huo,mtalii aliyejitambulisha kwa jina la Rachely kutoka Houston,Texas anasifia uzuri wa Serengeti,huku akitaja orodha ndefu ya ndege na wanyama.Anamsifia muongozaji kwamba alikuwa na maarifa ya kutosha ya kazi yake.
"Hii ni safari ya kukumbukwa maishani,tulianzia Tarangire na kwenda Serengeti hapa tulifurahi kuona wanyama na ndege wengi wa kuvutia muongozaji wetu alikuwa mwema sana,alikuwa na maarifa ya kutosha kwa kila jambo tulilouliza"anaandika Rachely
Ndege wakiwa kwenye makazi yao katika Kisiwa cha Musira ndani ya Ziwa Victoria,Manispaa ya Bukoba.Picha na Phinias Bashaya
Pia kupitia mtandao huo wa Trip Advisor Isabellla.A anafurahia maisha ya mitaani Jijini Arusha na umakini wa muongoza alihakikisha wako salama pamoja na watoto wao wawili wadogo.
Baadhi ya watalii wanaofika nchini, wakati wa utoto walikuja na wazazi wao,baada ya kukua na kujitegemea hupenda kurejea historia ya maisha yao kwa kurejea maeneo waliyofika na wazazi wao.
Huu ni utamaduni wa kuiga kwa kuwa unajenga matokeo ya kudumu katika ukuzaji wa utalii wa ndani.Mtoto aliyeona ukubwa wa tembo akiwa na wazazi wake,katika maisha yake hawezi kuwa sehemu ya mtandao unaosaka meno yake au vipusa vya faru.
Tishio la kutoweka kwa ndege, haliwezi kuwaacha salama wanyamapori.Viumbe hivi vinaishi kwa kutegemeana.Tai mzoga au tumbusi hutegemea mabaki ya mawindo.Kwa njia hiyo husafisha hifadhi na kudhibiti uwezekano wa usambaaji wa virusi vya magonjwa.
Kengele ya tahadhari kuhusu athari za uharibifu wa mazingira,pia imelia kwa mnyama sheshe au puku ambaye kasi ya kutoweka katika maeneo yao ya asili ni kubwa.
Ndege aina ya Korongo Nyangumi ambaye yuko hatarini kutoweka duniani Picha kutoka mtandao wa Getty images
Sensa iliyofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori(Tawiri)na matokeo kuchapishwa kwenye tovuti yao mwaka huu 2024,yanatoa tahadhari katika mifumo ikolojia mitatu ya Nyerere,Selous na Mikumi.
Sensa hiyo ambayo hufanyika kila baada ya miaka mitamo,inasema idadi yao imeporomoka kutoka 1,579 mwaka 2018 hadi 496 mwaka 2022,maeneo yao ya asili ikitajwa ni mapori ya akiba ya Kilombero na ziwa Rukwa.
Pia matokeo ya utafiti wa sensa ya mwaka 2020 katika hifadhi ya Burigi Chato yanataja kuonekana kwa pofu,wanyama ambao hawakuonekana katika sensa ya mwaka 2014,huku pundamilia wakiongezeka kwa asilimia 22.
Mtafiti kutoka taasisi hiyo Dkt. Edward Kohi,anasema hata malalamiko ya wananchi kuvamiwa na tembo ni matokeo ya uvamizi wa maeneo yao ya asili, ambayo wananchi wameweka makazi na kuendesha shughuli za kilimo.
"Ni matokeo ya mabadiliko ya utamaduni wa chakula chao sio kwamba idadi yao imeongezeka sana,wananchi wanalma mazao kwenye njia zao za asili,tembo wanaona kuna chakula kipya wanaanza kukifuata wanatakiwa kujua historia ya eneo kabla ya kuanzisha kilimo na makazi", anashauri Dkt Kohi
Katika Hifadhi ya Ziwa Manyara watalii hufurahi kupiga picha za maelfu ya ndege aina ya flamingo,ambao muunganiko wao katika ziwa hilo lenye magadi huonekana kama shuka kubwa jeupe.
Muongoza watalii na Mkurugenzi wa Bukoba Tours William Rutha,anasema watalii hupenda kuona vivutio vingi katika eneo moja,huku wakitaka kupiga picha za kumbukumbu za ndege,wanyama na vivutio vingine.
Hapa ndipo kuna kusanyiko kubwa zaidi la ndege wahamao kutoka mabara ya Asia na Ulaya, kuna majukwaa kukuwezesha kupiga picha kwa karibu na kutazama wanyama kama viboko kutoka mita chache.
Kusanyiko la ndege hao ndani yao kuna vikao vya manung'uniko dhidi ya uharibifu wa mazingira yao ya asili ,wakionya utiririshaji wa maji yenye kemikali za sumu kutoka kwenye mbolea za viwandani wakati wa kilimo.
Social Plugin