Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MUZIKI WA ASILI: NGUZO YA UTAMADUNI NA UMOJA KATIKA ENZI ZA KIDIJITALI


Na Kadama Malunde - Shinyanga

Katika ulimwengu wa kidigitali wa leo, ambapo teknolojia inabadilisha namna tunavyofanya mambo, ni muhimu zaidi kuliko hapo awali kuimarisha na kutetea nyimbo za asili na wasanii wa muziki wa utamaduni. Muziki huu sio tu sehemu ya burudani, bali ni urithi wa kitaifa unaohitaji kulindwa na kuendelezwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Muziki wa asili nchini Tanzania una mizizi yake katika desturi za zamani za makabila mbalimbali na mabadiliko ya kiteknolojia katika miaka ya hivi karibuni yameleta fursa mpya kwa wasanii wa muziki wa asili.

Kwa kutumia mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali, wasanii wameweza kufikia hadhira kubwa zaidi na kusambaza kazi zao kwa urahisi. Hali hii imewasaidia wasanii kutangaza tamaduni zao na kuendeleza urithi wa kiutamaduni kwa njia ambayo haikuwa rahisi hapo awali.

Kwa Mujibu wa Ripoti ya Takwimu za Mawasiliano kwa kipindi cha robo ya kwanza ya Mwaka wa fedha 2024/2025 (Julai - Septemba) iliyotolewa na 
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inabainisha kuwa, hadi kufikia Mwezi Septemba 2024 kuna Laini za Intaneti Milioni 41.4 nchini ikiwa ni ongezeko la asilimia 5 kutoka Laini za Intaneti Milioni 39.3 mwezi Juni 2024.

Wasanii kama Ng’wana Kang’wa, Saida Karoli, Bhudagala Mwanamalonja, Kisima Majabala, Mchele Mchele na Elizabeth Maliganya ni mifano hai ya wasanii wanaoendeleza muziki wa asili Kanda ya Ziwa, wakitumia mitandao ya kijamii kupitia Intaneti ili kufikia mashabiki, kujiinua kiuchumi na kuhamasisha kuhusu umuhimu wa tamaduni zao. Wakati huo huo wanakumbushia jamii kuhusu majukumu yao katika kulinda urithi wa kiutamaduni.

Haya yanathibitishwa na Msanii wa nyimbo za asili zenye mahadhi ya asili ya Afrika Moses Petro Lutema maarufu ‘Ng’wana Kang’wa’ kupitia Kundi la BTM Africa, anayepatikana Wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga anasema nyimbo za utamaduni na nyimbo za asili nchini Tanzania katika ulimwengu huu wa Kidijitali zinasaidia sana katika uhifadhi wa historia na tamaduni, kujenga umoja na mshikamano, kuendeleza utamaduni na mila, elimu na uhamasishaji, kukuza uwezo wa wasanii na kuhamasisha utu na utambulisho wa Kitaifa.

Ng’wana Kang’wa anayejulikana kwa sauti yake ya kipekee na mtindo wa kipekee wa kuandika nyimbo zinazohusisha hadithi za jadi na maisha ya jamii anaeleza kuwa, zipo fursa nyingi mtandaoni kwa Wasanii wa nyimbo za asili ikiwemo kuwafikia hadhira kwa haraka kwani kabla ya mitandao ya kijamii ilikuwa vigumu kuwafikia mashabiki.

“Mitandao ya Kijamii ikiwemo Facebook, Whatsapp, Youtube imewarahisishia wasanii wa nyimbo za utamaduni kufikisha ujumbe kwa jamii. Mitandao imekuwa daraja la kuwaunganisha wasanii na jamii hivyo kulinda utamaduni wa eneo husika. Hivi sasa unaweza kuwapata wasanii kwa urahisi sana kwa sababu mawasiliano yapo wazi. Mitandao imerahisisha kupeleka elimu kutoka serikalini kwenda kwa watu wa chini mfano kuhusu ukatili wa kijinsia, kuhamasisha maadili na uzalendo”,anaeleza Ng’wana Kang’wa.
Ng’wana Kang’wa

“Moja ya majukumu yetu Wasanii wa nyimbo za asili ni kulinda na kuenzi utamaduni wetu, tutengeneze nyimbo zinazohimiza utamaduni wetu. Niwahamasishe wasanii wenzangu wajikite kutengeneza nyimbo zinazohamasisha utamadauni wa Mtanzania. Tutumie lugha zetu, tutangaze maeneo ya utamaduni, historia yetu, kuenzi mila na utamaduni wa mavazi yaliyokuwa yanatumiwa na mababu zetu”,anaongeza Ng’wana Kang’wa anayesifika kwa nyimbo za kuhamasisha utamaduni kama vile Nalhi NsukumaLhugendo, Lyakandwa, Buhangwa na Bhashabiki.

Ng'wana Kang'wa, msanii maarufu wa muziki wa jadi ambaye amekuwa akihamasisha utamaduni wa Kanda ya Ziwa kupitia nyimbo zake, anawasisitiza Wasanii wenzake waepuke kuiga mavazi ya mataifa ya nje, wahamasishe vyakula vya asili bila kusahau kutangaza vivutio vilivyopo nchini kupitia nyimbo zao.
“Mfano Kanda ya Ziwa tumebarikiwa kuwa na vivutio vingi ikiwemo Ziwa Victoria, Visiwa kama vile Kisiwa cha Saa Nane, Mawe ambayo watemi wa zamani akiwemo Mwanamalundi walikanyaga wakaacha nyayo, maajabu ya Chemchemi ya Baloha- Chela Halmashauri ya Msalala ambapo kuna maajabu hayatangazwi. Kimsingi tuna vivutio vingi vinavyopaswa kutangazwa kupitia Sanaa yetu kwa kurekodia pia nyimbo zetu”,ameongeza Ng’wana Kang’wa.

Ng’wa Kang’wa ambaye sasa anatumika kutumbuiza kwenye shughuli mbalimbali zikiwemo za sherehe, kiserikali anaiomba Serikali iweke nguvu zaidi katika kuwatambua wasanii wa nyimbo za asili kuanzia ngazi ya Kijiji, ijue wapo na itambue umuhimu wao katika kuhamasisha maendeleo na kudumisha utamaduni.


Naye Elizabeth Maliganya kutoka kundi la Eliza Band anayepatikana Wilaya ya Bariadi Mkoa wa Simiyu ambaye ameendelea kujizolea umaarufu kupitia nyimbo za harusi (Ng’wanike Bhejaga Kaya, Haki Elimu, Mbina ya Ng’wana Wane), nyimbo za sherehe na siasa anasema Mitandao ya Kijamii imekuwa msaada mkubwa katika kusambaza nyimbo, kupanua wigo wa kazi, kupata kazi kupitia mitandao na kulipwa kupitia kazi anazoweka Mtandaoni.
Elizabeth Maliganya

“Nyimbo zetu za asili zina mafundisho ya kudumisha utamaduni wetu, nyimbo zetu zinahusu jamii, zinaelimisha na kukosoa maovu katika jamii. Nawashauri wasanii wenzangu wabadilike, mitandao ya kijamii siyo kwa ajili ya matusi, na ukiweka mtandaoni vinabaki huko, watoto watajifunza hayo wanayoweka mtandaoni, hivyo tusitumie vibaya mitandao hii, tutumie vizuri”,ameongeza.

Msanii mwingine wa muziki wa asili anayechangia pakubwa katika kuhifadhi na kuendeleza utamaduni wa Afrika ni Saida Karoli kutoka Bukoba Mkoani Kagera ambaye anaimba kwa Lugha ya Kihaya, Kiswahili, Kikurya, Kiganda na Kisukuma amesema Mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram, Tiktok na YouTube imerahisisha wasanii kutangaza kazi zao kwa urahisi, kwa gharama nafuu na hivyo kufikia hadhira kubwa.
Saida Karoli

Anawashauri Wasanii wa Tanzania wasijiweke kwenye mambo ya Kizungu wajikite katika mambo yanayolinda utamaduni wa Mtanzania kwani mambo ya nje ya nchi yanaturudisha nyuma hivyo kuchangia mmomonyoko wa maadili.

“Mimi naimba kuwakilisha taifa la Tanzania, Mitandao ya Kijamii inatusaidia kutangaza kazi, kupata pesa. Naomba tuhakikishe utamaduni wetu tunaulinda. Tuhamasishe ulinzi wa utamaduni kwa kuhamasisha mavazi, vyakula vya asili, lugha tunayotumia, maeneo tunayorekodie mfano ziwani, kwenye migomba, milima na maeneo yetu mengine ya asili”,anafafanua Saida Karoli.


WATAYARISHAJI WA NYIMBO WASIENDEKEZE PESA

Mtayarishaji na Muongozaji wa Picha Jongefu (Video) wa nyimbo za asili Migera Mkami Chacha maarufu Director Migera kutoka Kampuni ya Mbasha Studio anasema Waandaaji wa nyimbo za asili wanaendelea kupambana ili Wasanii wabaki kwenye utamaduni, wabaki kwenye jadi kwa kuhakikisha nyimbo wanazoandaa zinaendana na maadili ya Mtanzania.

Anathibitisha kuwa Wasanii wa Kanda ya Ziwa wanatumia mitandao ya kijamii kwa ufanisi, si tu kutangaza kazi zao, bali pia kujenga mazingira mazuri ya kiuchumi na kuendeleza utamaduni wao sambamba na kujenga majina yao na chapa katika tasnia ya muziki.

“Kupitia kazi za wasanii wa nyimbo za asili, watu wanarudi kwenye tamaduni wao, wanaupenda na kuuthamini. Kutokana na hali hiyo wasanii wetu wanatakiwa waoneshe jadi zao, waachane na usasa, usasa upo lakini lazima tusimamie jadi zetu, tusidharau mila zetu. Huu usasa unafanya tupoteze ujadi wetu, turudi kwenye tamaduni wetu”,anasisitiza.

Amewashauri Waandaaji wa muziki wakatae nyimbo zinazoharibu maadili ya kitanzania hivyo watengeneze kazi zinazosaidia jamii.

“Waandaaji wa muziki wenzangu tusiweke tamaa ya fedha mbele, tusiangalie pesa tu, tuangalie heshima kwa sababu nyimbo inapoenda kwenye jamii inaweza kwenda kuharibu jamii, mfano mtu akiimba nyimbo ya matusi usimruhusu kwa sababu jamii inaweza kuiga. Tuhimize nyimbo nzuri, wasivae nguo fupi, waelimishe jamii, wasiipotoshe jamii”,anahamasisha.

Anasema ni lazima jamii itambue kuwa mitandao ya kijamii sasa ni maisha ya watu, kuna watu wanapata pesa kupitia mitandao ya kijamii, wanatangaza kazi zao na kuongeza wigo wa kazi zao.

“Muziki sasa ni biashara, awali kuna watu walikuwa wananyonya wasanii mtandaoni sasa wengi wameanza kunufaika na mitandao ya kijamii kama vile, Bhudagala, Kisima, Juma marco, Ng’wana Kang’wa. Kutokana na dunia ya kidigitali, jamii inapata vitu vizuri kutoka wasanii hawa wa nyimbo za jadi kupitia tu simu za mkononi”,amesema Director Migera.


MASHINDANO YA KUHAMASISHA UJUMBE AINA MOJA

Mwana Sanaa, Mwigizaji, Mchekeshaji Maarufu Magambo Machimu Lenga kutoka mkoa wa Geita anaishauri Serikali ianzishe mashindano ya wasanii wanaoimba nyimbo za kuhamasisha utamaduni wa Mtanzania mfano kuwepo na matamasha ya wasanii wanaoimba nyimbo za maadili ili kuwe na nyimbo zinazojenga jamii.
Magambo Machimu Lenga 

“Tusiimbe tu imradi tu tunaimba kwa sababu hivi sasa wasanii wengi wanaimba tu nyimbo za hovyo hasa kusifu Mapenzi tu. Ni wakati sasa Serikali iweke mikakati maalumu ya kulinda utamaduni wa kitaifa kwa kuwa na Kampeni maalumu au ujumbe maalumu kama inavyofanyika kwenye Siku Maalumu za Mashabiki wa Simba SC au Yanga SC ambapo wasanii huimba nyimbo zenye ujumbe wa aina moja zinazohusu tukio husika.

Mfano kuwe mashindano ya kuimba yakiongozwa na ujumbe maalumu mfano ujumbe wa kuhamasisha ‘Vijana wafanye kazi’ , ambapo wasanii wowote wataimba wimbo wenye ujumbe mmoja kwa mitindo tofauti. Hii itasaidia kuwa na ajenda inayofanana.
Kuwe na mada moja, mashindano yanayohusu ajenda moja, tuzo zitolewe ili kuwa na nyimbo zinazolinda utamaduni wetu”,anasema Magambo Machimu Lenga anayejulikana kwa vichekesho vyake vinavyogusa maisha ya kila siku na tamaduni za jamii.


WABORESHE KAZI KISASA BILA KUATHIRI UASILI

Afisa Utamaduni Mkoa wa Shinyanga, Janeth Elias anasisitiza kuwa, Wasanii wa ngoma asili wana mchango sana katika jamii, wanasaidia kuelimisha jamii mfano kukemea ushoga, vitendo vya ukatili wa kijinsia, kuhamasisha matumizi ya Nishati mbadala ya kupikia, kutunza mazingira na wamekuwa mstari wa mbele kulinda maadili kupitia kazi za Sanaa.
Janeth Elias

“Niwasihi wasanii waendelee kudumisha mila zetu, ni nzuri inapendeza, wageni kutoka nje ya nchi wanapenda, waboreshe kazi zao ziende kwa usasa bila kuathiri vionjo vya asili na wasibadili wala kuharibu uasili wa makabila.

“Ili kuuishi uzalendo na kuenzi utamaduni wetu wasanii wazingatie mavazi ya asili wasivae nguo za kubana zinazoleta usasa na kuleta taswira mbaya kwa mila na desturi zetu, wavae mavazi ya asili yale ya makabila mfano mashuka, usinga, simbi na mengineyo”,amesema Elias.

Aidha amekiri Mitandao ya Kijamii kuwa imesaidia sana kulinda utamaduni ambapo amewakumbusha Wasanii wa muziki wa asili kutumia Mitandao ya kijamii kutangaza kazi zao, kuboresha na kutunza kazi zao na wasitumie mitandao vibaya.

“Ili kuenzi kuulinda utaifa wetu, wasanii watumie uasili, waimbe kwenye vyombo vya kisasa bila kuathiri uasili wao, afanye ngoma ya asili kwa usasa bila kuathiri uasili”,ameongeza.


MKAKATI WA KUTAMBUA WASANII

Afisa Utamaduni wa Mkoa wa Shinyanga anaeleza kuwa Serikali inaendelea kuwatambua na kuwatumia wasanii wa nyimbo za asili kwenye shughuli mbalimbali za kiserikali na matukio mengineyo.

“Mkakati tulionao ni kuwatumia wasanii waliopo kwenye maeneo yetu, kwani ni rahisi sana kufikisha ujumbe vizuri kwa jamii kwa kutumia vionjo vyao kwenye jamii husika. Ni vyema kutumia wasanii waliopo eneo husika ili kuwainua kiuchumi na kufikisha ujumbe kwa haraka na kwa urahisi zaidi kwa lugha inayoeleweka”,anaeleza Elias.


KUWE NA MWONGOZO, WATAALAMU WANAOPITIA KAZI STUDIO

Mtafiti wa Kujitegemea wa mila na desturi za Kabila la Wasukuma mkazi wa Kijiji cha Shatimba wilaya ya Shinyanga, bw. Sonda Kabeshi anashauri sehemu ambako Wasanii Wanakwenda kurekodia nyimbo (Studio) kuwe na mwongozo au wataalamu wa kuuliza wimbo una maana gani ambapo wataalamu hao watakuwa na wajibu wa kuwasimamia wasanii ili nyimbo ziwe na maadili na kulinda utamaduni katika taifa.
Sonda Kabeshi

“Hii mitandao ya kijamii inasaidia lakini wasanii wachague aina ya nyimbo za kuimba badala ya kuimba tu na kucheza, wachague utamaduni wa upande upi, achague ngoma anayocheza. Nyimbo ziwe na mafunzo mfano kuna huyu Msanii anaitwa Kisima ana nyimbo za mafumbo zinazofundisha maadili, hazimtaji mtu lakini zinamgusa mtu yeyote. Msanii Kisima anatumia nyimbo zake kuwasilisha ujumbe wa kihistoria, maadili, na tamaduni za Kiafrika, hasa za jamii za Kanda ya Ziwa”,anabainisha Mzee Sonda Kabeshi.


“Katika ulimwengu huu wa kidijitali Wasanii hawa wanapaswa wawe wabunifu, waimbe nyimbo za matukio ziendane na mafundisho mfano utunzaji mazingira, kupinga mimba za utotoni, ndoa za utotoni, zenye maadili zinazohimiza uwajibikaji”,amesisitiza.


WASANII WAMEJISAHAU?

“Utamaduni wanaocheza leo ni kama nusu kwa sababu hawatumii vile vitu vya asili, japo wanasema ngoma za asili, lakini vitu vya asili hatuvioni, mfano lugha wanayotumia ni ya Kisukuma japo baadhi yao mavazi yao siyo ya asili, tuendelee kuhamasisha wote warudi kwenye uasili zaidi”,anasema mzee Kabeshi.

Anasema zamani Ngoma za asili zilikuwa na majina yake lakini sasa wasanii wanacheza tu na kuimba kidogo na hawana mfumo rasmi kama zamani ambapo ngoma zilikuwa na majina yake kabisa.

“Mfano huku Usukumani kulikuwa na ngoma maarufu Bucheye, Bucheyegi, Buyeye, Bugidu (Wigashe) Bhununguli, Bugoyangi na Beni (hizi zilishawahi kwenda kutambulishwa nje ya nchi Sweden na Denmark tarehe 14.08. 1974 ambapo Watanzania 34 kutoka mkoa wa Mwanza na Shinyanga walikwenda kuwakilisha ngoma ya Beni inayochezwa kwa kuvaa kanzu, mavazi meupe na vitambaa waliporudi ndiyo walichangia kuanzisha Makumbusho ya Wasukuma ya Bujora yaliyopo Kisesa Mkoa wa Mwanza wakishirikiana na Padre David Clement yaliyozinduliwa tarehe 06.08. 1978 ambapo Mgeni rasmi alikuwa Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere aliyeshuhudia mchuano mkali kati ya Ma Manju maarufu wa ngoma ya Bugidu Kali Kali Mbagule (Ngalu)  na Sitta Mhogota (Ngika) ”,ameeleza Mzee Kabeshi.
Mzee Sonda Kabeshi anashauri wasanii  na watanzania kwa ujumla waunge mkono jitihada za  kuenzi mila na desturi zinazosisitizwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyesimikwa kuwa Chifu Mkuu wa Machifu wote Tanzania na kuitwa Chifu Hangaya (Nyota Angavu/Inayong'aa) 
 Septemba 8,2021 wakati wa Hitimisho la Tamasha la Utamaduni (Mila na Desturi) lililofanyika kwenye Viwanja vya Msalaba Mwekundu (Redcross)  Kisesa wilayani Magu Jijini Mwanza.

Amewashauri Wasanii wa nyimbo za asili/muziki wa asili Kanda ya Ziwa watembelee Makumbusho ya Bujora wakajifunze wajue wanacheza ngoma gani na kama wamebuni ngoma mpya wafanyeje ili kupata ngoma zinazoendana na utamaduni.

Muziki wa asili unachangia sana katika kuhifadhi historia na tamaduni za makabila mbalimbali. Nyimbo hizi sio tu za burudani, bali pia zina ujumbe wa kijamii, zikiwemo maadili, elimu na kukemea vitendo vya ukatili. Pia, muziki huu unasaidia kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa jamii, ukifungua njia za mawasiliano kati ya vizazi.


MUSTAKABALI WA KUKUZA UTALII KUPITIA MUZIKI WA ASILI

Ili kuing'arisha nchi ya Tanzania kwenye jukwaa la kimataifa kuthibitisha sifa yake kama kivutio kikubwa cha utalii duniani 
 ikiwa na mbuga zake za kitaifa, fukwe zake safi na alama maarufu kama Mlima Kilimanjaro zinazovutia wageni kutoka pande zote za dunia ni wakati muafaka sasa Wasanii wa muziki wa asili na wasanii kwa ujumla nchini kutumia mitandao ya kijamii kuonesha uzuri wa Tanzania ikiwa ni kuunga mkono juhudi madhubuti za uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Filamu ya The Royal Tour, ambaye amejikita katika kukuza sekta ya utalii ya Tanzania kimataifa na kuwekeza kwenye maendeleo endelevu. 

Kupitia Tovuti ya Malunde.com kazi za wasanii wa nyimbo za asili/muziki wa asili (Gusa 👉Utamaduni , Nyimbo za asili)  zimekuwa zikipewa nafasi kubwa ili kueneza na kukuza nyimbo hizi, kuhakikisha kwamba hazipotei na zinabaki kuwa sehemu muhimu ya maisha yetu.

Wasanii wa Muziki wa Asili wanaendelea kutumia mitandao ya kijamii kuongeza ufanisi wa matangazo, kuunda jukwaa la mawasiliano, kufanya mauzo ya kijanja, kushiriki matukio na tamasha, kujenga jina na chapa, kujifunza na kubadilishana mawazo, kuweka kazi zao kwenye maktaba ya mtandao na uhamasishaji wa masuala ya utamaduni.

Kazi za wasanii wa muziki wa asili zinahitaji kuungwa mkono na kuthaminiwa katika ulimwengu wa kidigitali, ambapo teknolojia inatoa fursa nyingi. Ni wajibu wetu, kama jamii, kulinda na kukuza muziki huu ili kudumisha utambulisho wetu wa kitaifa na kuimarisha umoja miongoni mwa Watanzania.

Kwa kufanya hivyo, tutachangia katika kujenga jamii yenye nguvu na yenye maadili, huku tukihifadhi historia na utamaduni wetu kwa vizazi vijavyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com