Kundi hili linadai kuwa CCM imenunua magari aina ya Toyota Land Cruiser kwa bei ya dola za Kimarekani 200,000 (sawa na shilingi milioni 540 za Kitanzania). Hata hivyo, taarifa hizo zilihusishwa na picha zinazodaiwa kuonyesha magari hayo yakipakiwa katika eneo la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Lumumba, Dar es Salaam.
UKWELI ULIVYO
Baada ya uchunguzi wa haraka kupitia mtandao wa Google, ukweli ulibainika kuwa picha zilizotumiwa na wanaharakati hao si za magari yaliyonunuliwa na CCM, wala hayakuhusiana na Tanzania. Picha hizo zinatokana na makala ya BBC Top Gear yenye kichwa cha habari “This Secret Dealer Is Selling New Old Toyota Land Cruisers That Are Supposed To Save The World.” Magari hayo yameonekana yakiwa yamepakiwa kwenye stoo moja nchini Uholanzi, yakisubiria wateja.
Tukio hili linaonyesha wazi jinsi wanaharakati hao walivyojaribu kutumia mbinu za udanganyifu kueneza habari potofu kwa lengo la kuipaka matope serikali ya Rais Samia. Picha hizo zilikuwa ni za magari ya Toyota 650 ambayo hayahusiani kabisa na Tanzania, achilia mbali UVCCM.
MBINU ZA KUPOTOSHA NA AJENDA BINAFSI
Wanaharakati hawa wamekuwa wakijaribu kwa muda mrefu kumchafua Rais Samia na uongozi wake kwa kueneza taarifa za kughushi. Inaonekana wameishiwa hoja za msingi, na sasa wanatumia mbinu za kutunga hadithi za uongo, huku wakilenga kuendeleza ajenda zao zisizokuwa na msingi wa kweli.
Kile kinachowasukuma wanaharakati hawa ni uhitaji wa fedha kutoka kwa wafadhili wa nje, ambao wanasubiri kuona ajenda inayoendeshwa dhidi ya serikali ya Tanzania. Katika jitihada za kujihakikishia fedha hizi, wanaharakati hawa wamekuwa wakiwalipa vijana wa mitandao ya kijamii ili kusambaza uzushi unaolenga kupotosha umma kuhusu uongozi wa Rais Samia.
KIPAJI CHA UONGO KIMEFIKIA KIWANGO CHA JUU
Mbali na kuwa na ajenda za kisiasa, wanaharakati hawa wanaonekana kuwa na kipaji cha hali ya juu cha kuunda hadithi za uongo. Walakini, badala ya kutumia kipaji hicho kwa manufaa ya jamii, wanakitumia kutunga simulizi za kupotosha ili kuwadanganya wananchi na ulimwengu mzima.
Pengine sasa ni wakati mwafaka kwa wanaharakati hawa kufikiria njia nyingine ya kutumia kipaji chao cha kutunga hadithi. Badala ya kuzusha na kueneza uongo kwa lengo la kupata fedha, wanaweza kutumia uwezo wao huo wa ubunifu kutunga script za tamthilia au filamu, ambazo zinaweza kupata nafasi kwenye runinga au majukwaa ya burudani. Bila shaka, wanaharakati hawa wana uwezo wa kuwa "director" wa uongo, na "Mariawood" inaweza kuwa kiwanda sahihi cha kuzalisha hadithi zao za kufikirika.
HITIMISHO
Kisa hiki cha udanganyifu kinathibitisha jinsi baadhi ya wanaharakati wamepoteza uhalali wa hoja zao na kuamua kuingia kwenye njia ya uongo na uzushi. Taarifa zisizo na msingi kama hizi zinaharibu hadhi ya siasa za Afrika na kuchochea migogoro isiyo na sababu. Ni muhimu kwa jamii kuwa na uwezo wa kuchuja na kuhoji taarifa zinazotolewa na vyanzo visivyo na uhakika, kwani ukweli hauwezi kusimama na uzushi.
Katika nyakati hizi ambapo ukweli na uongo vimechanganyika, tukio hili linatufundisha kwamba uchunguzi wa kina na uhakiki wa taarifa ni muhimu zaidi kuliko wakati wowote. Wananchi wanapaswa kuwa macho dhidi ya propaganda zinazolenga kupotosha ukweli, ili kulinda amani na utulivu wa taifa.