Msabila Malale Kulwa (kushoto) na Zuhura Waziri (kulia)
Na Mwandishi wetu - Shinyanga
Katika tukio la kuhuzunisha linaloonyesha mvutano wa kisiasa, Diwani wa Kata ya Ibadakuli Manispaa ya Shinyanga, Msabila Malale Kulwa, anadaiwa kumshambulia Diwani wa Viti Maalum wa tarafa ya Ibadakuli, Mhe. Zuhura Waziri, kwa kumvua hijab na kumpiga ngumi.
Tukio hilo lilitokea tarehe 23 Oktoba 2024, wakati Mhe. Zuhura alipokuwa akisimamia uchaguzi wa kura za maoni katika Kijiji cha Ibadakuli. Zoezi hilo lilihusisha uchaguzi wa wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) watakaowakilisha chama hicho katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 mwaka huu.
Taarifa kutoka eneo la tukio zinasema kuwa Zuhura alishambuliwa ghafla wakati akitekeleza majukumu yake ya kimsingi, hali iliyoleta taharuki miongoni mwa wajumbe wa uchaguzi na kuathiri uaminifu wa mchakato wa kidemokrasia katika eneo hilo.
Inaarifiwa kuwa Diwani Msabila, ambaye aliteuliwa kusimamia uchaguzi katika kituo cha Mwagala, alikwenda Kijiji cha Ibadakuli na kudaiwa kuanzisha vurugu kwa kumpiga Zuhura, ambaye alijeruhiwa usoni.
"Mvutano ulianza baada ya Diwani Msabila kuingilia uchaguzi, akionekana kumuunga mkono mmoja wa wagombea aliyekuwa anatetea kiti chake ambaye hata hivyo alishindwa kwenye uchaguzi huo, Diwani wa Viti maalum Zuhura ameumizwa usoni ,ni kama amechanwa kwa kitu chenye ncha kali usoni, huenda mpiga ngumi alikuwa amevaa pete... hata hivyo wananchi waliokuwa eneo hilo walimdhibiti Msabila asiendelee kufanya vurugu eneo la uchaguzi",kimeeleza Chanzo chetu cha habari.
Diwani wa Viti maalumu Mhe. Zuhura Waziri, ameeleza tukio lilivyokuwa :
"Mimi nilikuwa msimamizi wa Uchaguzi wa kura za maoni, Wakati naanza kusoma majina ya wagombea kwenye kujieleza, yeye sijui alikuwa na mtu wake? sasa yule mwenyekiti aliyekuwa anatetea nafasi alizungumza muda zaidi ya dakika tatu nilizowapa wagombea yeye alijinadi zaidi ya dakika muda uliopangwa, nikamwambia mgombea Omba kura muda umeisha. Wakati naendelea kuzungumza Diwani wa kata ya Ibadakuli akasimama akasema unajua Mheshimiwa huyu nani, Nikamwambia HAPANA kwanza wewe hujapangiwa kusimamia uchaguzi hapa umepangiwa kusimamia Mwagala kwanini umenifuata kwenye kituo changu?
...Sasa mimi nikajua mwenzangu yameisha baada ya kumwelewesha lakini ghafla akasimama, sikujua kama atanipiga kwa sababu sina ugomvi naye, akanivuta, akanivua ushungi, akanipiga nikamuuliza Mheshimiwa shida nini", ameeleza Zuhura.
Hata hivyo Diwani wa kata ya Ibadakuli Msabila Malale Kulwa akielezea tukio lilivyokuwa, amedai kuwa wakati wagombea walivyomaliza kujinadi na wajumbe kuanza kupewa karatasi za kupiga kura, ndipo akahoji mbona kwenye mfuko wa kuweka kura zilizopigwa hamjajiridhisha kama kuna usalama,na kueleza kwamba baada mfuko kukung’uta ikaanguka kura moja ambayo imeshapigwa.
Ameeleza kuwa, baada ya hapo akamuona tena msimamizi wa pili wa uchaguzi huo, akipigia kura watu ambao hawajui kusoma wala kuandika napo akahoji, na kueleza kwamba ndipo Diwani wa Vitimaalumu Zuhura Waziri, ambaye ndiye alikuwa msimamizi mkuu wa uchaguzi huo akamwambia asiwafundishe kazi na kisha kumsusia bahasha ya karatasi za upigaji kura.
Amefafanua kwamba diwani huyo alianza kumtolea maneno ya kashfa, kwamba wao ndiyo wamechaguliwa kusimamia uchaguzi huo, yeye diwani amekwenda kufanya nini hapo bali anapaswa kuondoka,na kubainisha alimjibu kwamba hapo ni kituo chake cha kupiga kura.
Amesema baada ya muda diwani huyo akiwa na Katibu Mwenezi wa Kata ya Ibadakuli na wajumbe wengine, walikaa pembeni wakiongea, lakini ghafla Zuhura alimsogelea na kuanza kumwambia kwamba hamjui eti, huku na yeye akijibu kwamba hamjui ndipo ugomvi ukaanza.
“Zuhura yeye alinirukia ili kunikamata sehemu zangu nyeti, na mimi nikamkamata kumtoa wala sikumpiga, ndipo watu wakajaa na kutuamua ndivyo ilivyokuwa Mwandishi,”amesema Msabila.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Anold Makombe
NI JAMBO LA KAWAIDA WATU KUVUTANA
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini Anold Makombe, amesema taarifa alizonazo ni jambo la mvutano tu baina ya Madiwani hao.
"Tunalifanyia kazi hili jambo lililojitokeza...Ni jambo la kawaida tu watu kupishana maneno, kutofautiana tu kwa maneno wala siyo kwamba ilitokea tafrani watu wakapigana, hawakupigana, halikuwa jambo la kupigana. Kwenye chaguzi kama hizi watu kutofautiana kwenye maneno ni vitu vya kawaida. Lingekuwa la kupigana sisi kama chama tungekuwa tumechukua hatua kwanini wamepigana hadharani",amesema Makombe.
Kuhusu Madai ya Zuhura kuumizwa usoni, Mwenyekiti wa CCM amesema "Viongozi wa Chama tutakwenda kumuona ili tujue kwa undani kilichojitokeza lakini kwa sura tu walitofautiana tu maneno, nilichoelezwa kama kiongozi ni kwamba hapakuwa na ngumi, walipishana maneno tu... Msabila alitakiwa tu apige kura aondoke na Zuhura ndiyo alikuwa msimamizi wa uchaguzi eneo hilo".
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com