Mara baada ya Rais Samia kuingia madarakani Machi 19,2021 amekuwa akifanya kazi kubwa ya kufungua milango ya maendeleo kwenye kila sekta.
Ameweza kuwakaribisha wafanyabiashara wenye mitaji kutoka ndani na nje ya nchi kuwekeza nchini.
Dhamira yake hiyo ya kumwondelea mwananchi umaskini imemfanya Rais Dkt. Samia kuwa kiongozi pekee mwanamke aliyeeingiza nchi kwenye 10 bora za ukuaji wa uchumi Afrika, akiziacha nchi 44 nyuma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Shirika la Fedha duniani (IMF), mwishoni mwa wiki iliyopita, licha ya changamoto zinazoukumba uchumi wa dunia kwa sasa kutokana na vita na magonjwa mbalimbali ya milipuko, Rais Dkt. Samia ameendelea kuifanya Tanzania kuwa imara kwenye ukuaji wake kiuchumi kwa mwaka 2024.
Ukuaji wa pato la Taifa (GDP) kwa sasa umefikia katika kiwango cha dola bilioni 79.87.
Maendeleo ya uchumi wa Tanzania yanaonesha athari chanya katika sera bora, uongozi Madhubuti na kujitolea kwa maendeleo chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia.
Kupanda kwa Tanzania kiuchumi kunadhihirisha ukuaji wa uchumi endelevu na jumuishi, hususan katika sekta muhimu za kilimo, utalii na viwanda hali inayotoa nafasi ya kustawisha maisha ya mwananchi na nchi kwa ujumla.
Kwa kipindi kifupi Rais Dkt. Samia amefanikiwa kuhakikisha uchumi wa Tanzania unaendelea kukua barani Afrika na duniani kwa ujumla.
Kwa sasa matarajio ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania yanatajwa kuwa ni asilimia 5.4 kwa mwaka 2024 kutoka asilimia 5.1 mwaka 2023, kiwango hiki ni juu kidogo ya wastani wa asilimia 4.4 uliotazamiwa mwaka 2023 kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na asilimia 3.8 kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)
Aidha ukuaji huo unatazamwa kufikia asilimia 6.0 kwa mwaka 2025, kiwango kinachoifanya ionekane kuwa ni mojawapo ya nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi zaidi Afrika.
Sababu kuu zinazochangia ukuaji huu ni pamoja na ongezeko la uwekezaji katika sekta za kilimo, utalii, viwanda, miradi ya miundombinu kama reli ya kisasa, usafirishaji na kuimarisha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini.
Ustawi wa uchumi wa Tanzania pia umechangiwa na utulivu wa kisiasa, kudhibitiwa kwa mfumuko wa bei, utulivu kwenye bei za bidhaa muhimu kama chakula na nishati.
Aidha, serikali ya Awamu ya Sita imekuwa na sera bora za kifedha na imekuwa ikichukua hatua madhubuti za kuboresha miundombinu na huduma za kijamii, pamoja na mikakati ya kupunguza deni la taifa kwa kushirikiana na taasisi za kimataifa.
Tanzania imeingia kwenye 10 bora za ukuaji wa uchumi Afrika ikitoka kwenye kundi la nchi zilizokuwa nje ya 10 bora Afrika.
Kwa sasa Tanzania inaungana na nchi za Afrika Kusini, Misri, Algeria, Nigeria, Morocco, Ethiopia, Kenya, Angola na Ivory Coast.