Watu wawili wameuawa kwa kunyongwa na kamba kisha kutobolewa macho nyumbani kwao katika eneo la barabara ya nne jijini Tanga huku baba mwenye nyumba Alii Mohamed Bagidad (60) naye akiwa hajulikani alipo.
Watu hao wamefahamika kama Saira Ali Mohammed (50) ambaye ni mama mwenye nyumba pamoja na binti wa kazi aliyetambulika kwa jina moja la Asha (20).
Mwandishi wa habari hizi amefika nyumbani kwa marehemu na kuzngumza na majirani wa familia hiyo ambao walisema walikuta miili ya marehemu hao ikiwa na kamba shingoni huku wakiwa wamewekwa nguo mdomoni.
"Baada ya jirani mmoja kuja kugonga kwenye hii nyumba na kukuta ukimya alilazimika kuchungulia ndani ndipo akamuona mama mwenye nyumba yupo chini amelala na ikaonekana miguu ya msichana wa kazi,
"Lakini yule mama alivyokuwa akionekana pale chini alionekana kama amekufa ikabidi atafutwe Mwenyekiti wa serikali za mitaa akasema haiwezekani kuvunja mlango itabidi tuwatafute polisi" alisema Halima Shebe jirani yake.
Shuhuda huyo amebainisha kwamba baada ya polisi kufika walivunja mlango wa mbele na kuingia ndani akaonekana mama yuko kwenye korido wakaendelea mbele chumbani wakamkuta dada wa kazi naye amelala chini.
"Polisi walifanya taratibu zao za kutoa ile miili ya marehemu na kuiweka ndani ya gari lakini mpaka sasa hatujui wale tukio wamefanyiwa na nani na baba mwenye nyumba mpaka saa hizi anatafutwa hajulikani yuko wapi simu zake tangu jana hazipatikani kwa hiyo hapa hatujui nani kafanya tukio hilo,
"Gari la baba mwenye nyumba lipo hapo nje tangu jana na yenye mwenyewe jana mpaka majira ya saa kumi jioni nimemuona, yaani bado tuna wasiwasi kufuatia jambo hili, tunasubiri polisi wafanye kazi yao" ameongeza.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa umoja wa wenyeviti Wilaya ya Tanga Bunu Omari Bahero amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kukabiliana na matukio ya kuuawa na kutekwa ili kuifanya jamii kuishi bila hofu kwenye nchi yao.
"Huyu bwana ninamfahamu sababu ni jirani hapa kwa dada yangu kweli ilinishtusha sana kusikia hilo tukio kiukweli ni tukio ambalo limetusikitisha sana kwasababu huyo mfanyakazi simfahamu lakini marehemu ambaye ni mke wa Bagdadi namfahamu vizuri sababu tunakutana hapa nje mara nyingi vyombo vya ulinzi tuviombe viendelee kufanya upelelezi ili kuwabaini waliofanya hili tukio, "amesisitiza Bahero.
"Sasa hivi inakuwa ni tishio kubwa sana katika nchi yetu na miji yetu hii ya kuuliwa na kutekwa kwahiyo tuwaachie kazi polisi waendelee na kazi yao kisha tutapata taarifa kamili, " ameema Bahero.
Jeshi la polisi limethibitisha kutokea kwa mauaji hayo huku likiendelea kumtafuta Alii Mohamed Bagidad pamoja na mauaji hayo ambaye hadi hivi sasa naye hajulikani alipo.
Katika taarifa yake Kamanda wa Polisi Mkoa Tanga Almachius Mchunguzi imesema tukio hilo limetokea septemba 30 majira ya saa moja usiku.
Aidha Kamanda Mchunguzi ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na jeshi la polisi kwa kutoa taarifa mahali popote atakapoonekana baba mwenye nyumba hiyo ili akamatwe na sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Social Plugin