WACHIMBAJI MADINI WASIMAMIWE USALAMA MAHALA PA KAZI


Na Christina Cosmas, Morogoro

CHAMA cha wachimba madini mkoa wa Morogoro (MOREMA) kimepata viongozi wapya wa kuongoza kwa muda wa miaka mitano na kujaza nafasi 15 huku wakiahidi kusimamia usalama mahala pa kazi kwa kuondoa changamoto za wachimbaji ikiwemo kufukiwa na vifusi migodini.

Akizungumza mara baada ya uchaguzi wa viongozi wa chama hicho uliofanyika mjini hapa Makamu Mwenyekiti wa MOREMA Samuel Kobelo Muhulo anasema MOREMA ina umuhimu wa kusimamia wachimbaji wadogo katika kufanya shughuli za uchimbaji madini huku ikiwahimiza kufuata kanuni za uchimbaji.

 “changamoto ni nyingi, ikiwemo kukosa mtaji, maeneo mengi wanayochimba wanachimba kwa bahati nasibu hawajui chini kuna madini gani lakini kama serikali itatusaidia kupata vifaa vya kutambua chini kuna madini gani, mfano kama dhahabu itatusaidia, wenzetu kanda ya ziwa wao wamepimiwa maeneo yao kwa hiyo wanajua watapoteza Milioni 30 au 40 lakini mwishoni watavuna” anasema

Anasema mkoa wa Morogoro una maeneo mengi ya uchimbaji madini yakiwa ya aina ya dhahabu inayopatikana maeneo ya Mazizi ambapo maeneo ya Matombo kuna Rubi, dhahabu na spino na Gairo kuna dhahabu.

Awali Msimamizi mkuu wa uchaguzi kutoka shirikisho la wachimba madini Taifa (FEMATA) Joseph Mombachepa amesema uchaguzi huo ulikuwa wa haki ambapo kutokana na wagombea kuwa mmoja mmoja kila nafasi wametumia demokrasia na kuwapitisha wagombea hao bila kupingwa.

Anawataja waliopita katika kinyang’anyiro hicho kuwa ni pamoja na nafasi ya Mwenyekiti wa MOREMA mkoa ilichukuliwa na Omari Mzeru Nibuka ambaye alitetea nafasi yake aliyokuwa akiiongoza awali, nafasi ya makamu mwenyekiti imechukuliwa na Samuel Kobelo Muhulo na nafasi ya katibu alipita Aquline Cloud Magalambula.

Anawataja wengine kuwa ni Kenneth Mangweha aliyepata nafasi ya Katibu Msaidizi, nafasi ya Mhazini alipata Luhende Richard Luhende, mhazini msaidizi alipata Mwanaidi Ngurungu.

Alisema katika uchaguzi huo pia kulikuwa na nafasi mbalimbali maalum za uongozi ambazo zilipitisha mgombea mmoja mmoja ambazo ni nafasi ya mwakilishi wa wafanyabiashara, mwakilishi wa makundi maalum na nafasi ya siasa na uhusiano wa jamii.

Alizitaja nafasi zingine kuwa ni mkaguzi wa migodi ambayo ilichukuliwa, mwakilishi wachimbaji  vijana, mwakilishi wachimbaji wasiokuwa  rasmi, mwakilishi kamati ya Nidhamu na usuluhishi, nafasi ya Mwakilishi wachimbaji wanawake na kamati ya afya usalama na mazingira.

Uchaguzi huo umehusisha wanachama hai 42 waliopiga kura za kupata viongozi hao kati ya wanachama 600 wa MOREMA waliopo mkoani hapa.  

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post