BONANZA LA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA WILAYANI MKALAMA LAFANA

 

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Moses Machali amewataka wananachi wilayani Mkalama kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Mpiga Kura ili wawe na sifa za kuchagua viongozi katika Uchaguzi wa Serikali Za Mitaa utakaofanyika tarehe 27/11/2024.


Wito huo ameutoa tarehe 6/10/2024 wakati wa Bonanza la Hamasa ya Uchaguzi wa Serikali Za Mitaa lililofanyika katika viwanja vya shule ya Msingi Nduguti inayopatikana katika kata ya Nduguti wilayani Mkalama.

“Ili uweze kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 unapaswa kuwa umejiandikisha katika Daftari la orodha ya Wapiga Kura. Hivyo wenye Umri kuanzia miaka 18, nawasihii mjitokeze kujiandikisha ili muwe na sifa ya kuchagua viongozi mnaowataka” Mhe. Machali amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Moses Machali amesema kuwa zoezi la uandikishaji Orodha ya Wapiga Kura litaanza tarehe 11-20, Oktoba 2024 na zoezi hilo litachukua muda wa siku 10 hivyo wananchi watumie fursa hiyo kujitokeza kwa wingi “Kama unataka kumchagua kiongozi umpendae hakikisha unajiandikisha”, amesema Mhe. Machali.

Kwa upande wake, Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Wilaya, Mohamed Atiki ametoa rai kwa vijana na wanawake  wenye sifa kujitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

“Vijana wenye umri kuanzia miaka 21 na kuendelea, pamoja na kina mama nawasihi mjitokeze kwa wingi mgombee nafasi za uongozi ili kwa pamoja muwe sehemu ya mabadiliko katika jamii zetu lakini pia wananchi wenye sifa wakati wenu ni huu wa kuchagua viongozi mnaowataka” amesema Atiki.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post