Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TFS YAIBUKA NA UTALII WA NYUKI KATIKA MAONESHO YA SITE 2024

Dar es Salaam, Oktoba 11, 2024 – Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)  imekuwa kivutio kikubwa katika Maonesho ya Nane ya Kimataifa ya Swahili International Tourism Expo (SITE), yaliyofunguliwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mlimani City, Jijini Dar es Salaam.

TFS, moja ya washiriki wakuu, imepata nafasi ya kuonyesha fursa za kipekee za utalii ikolojia nchini, huku ikiibua vivutio vipya ambavyo vimewafanya watu kushiriki kwa hamasa kubwa.

Katika banda lake, TFS inawasilisha fursa za uwekezaji kwenye maeneo inayaoyasimamia kama vile maeneo ya kihistoria ya Magofu ya Tongoni Ruins, Kaole Ruins, na Mji Mkongwe wa Bagamoyo, pamoja na vivutio vya utalii wa kiikolojia vilivyoko kwenye hifadhi zake. Hata hivyo, kilichovuta hisia zaidi mwaka huu ni utalii mpya wa nyuki (Api-tourism), unaowapa wageni nafasi ya kipekee kudungwa na nyuki kwa lengo la tiba na kujipatia bidhaa mbalimbali zinazotokana na nyuki.

Hiki ni kivutio kipya ambacho kimewafanya wengi kufurahia uzoefu wa moja kwa moja. Nyuki walioko kwenye sehemu ya banda la TFS wamekuwa wakitumika kuwadunga wageni wanaotembelea banda hilo, na huduma hii imepokelewa kwa shangwe, ikizingatiwa kuwa inatolewa bure. 

Aidha, bidhaa za mazao ya nyuki kama vile asali imekuwa maarufu kutokana na faida zake kiafya, ikitajwa kusaidia kinga ya mwili na kutibu maradhi mbalimbali.

“Tumeleta jambo jipya mwaka huu, utalii wa nyuki! Wageni wanapata fursa ya kudungwa bure na nyuki, na leo hata mimi nimedungwa, lakini sihisi maumivu yoyote. Ni fursa adimu, na mwitikio wa wananchi ni wa kushangaza!” alisema kwa furaha Afisa Utalii Mkuu wa TFS, Josephy Sendwa, huku akiwaonyesha wanahabari mzinga uliojaa nyuki.

Brenda Mwakipesile, mmoja wa wahifadhi kutoka TFS anayehusika na kudungisha nyuki wageni, alisema, “Utalii huu wa nyuki unazidi kuvutia watu kwa sababu ya faida zake kiafya. Nyuki wana uwezo wa kuimarisha kinga ya mwili na kusaidia kutibu maradhi mbalimbali. Wananchi wengi wanaendelea kujitokeza kupata huduma hii, na tumekuwa tukiendelea kuitoa hata baada ya maonesho katika Msitu wa Hifadhi wa Mazingira Asilia Vikindu uliopo Mkurnga mkoani Pwani.”

Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Dk. Ramadhan Dau, ambaye pia alijitokeza kudungwa na nyuki katika mikono yote miwili, aliwahamasisha wananchi zaidi kufika kujionea na kushiriki katika utalii huu wa kipekee. 

Alisisitiza kuwa hii ni nafasi adimu ambayo si tu inasaidia afya bali pia inatoa fursa ya pekee ya kujifunza kuhusu maajabu ya nyuki.

Kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, TFS imejikita kuleta aina mpya za utalii ambazo hazipatikani sehemu nyingine, huku ikihakikisha kuwa watalii wanapata uzoefu wa kipekee unaohusisha si tu vivutio vya asili bali pia tiba asilia kupitia utalii wa nyuki.

Maonesho ya SITE yanaendelea hadi mwisho wa wiki, na TFS inaendelea kuwakaribisha wadau wote kufika kwenye banda lake ili kujifunza, kushiriki, na kupata huduma za kipekee zinazotolewa, ikiwemo utalii huu wa nyuki unaovutia watu wa rika zote.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com