Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CWT BAGAMOYO YAWAFUTA MACHOZI WAHANGA WA MOTO SEKONDARI YA WASICHANA MANDERA

Mkuu wa shule ya sekondari ya Wasichana ya Mandera katika halmashauri ya Chalinze Mwalimu Regina Ngereza akipokea zawadi ya vifaa mbalimbali kutoka kwa baadhi ya viongozi wa CWT Wilaya ya Bagamoyo

**

NA. ELISANTE KINDULU, CHALINZE

CHAMA cha walimu Tanzania- Wilaya ya Bagamoyo (CWT) kimetoa vifaa mbalimbali kwa wanafunzi waliounguliwa vifaa vyao baada ya moto mkubwa kuteketeza bweni la wanafunzi wa kidato cha nne wa sekondari ya Mandera katika halmashauri ya Chalinze mkoa wa Pwani.

Vifaa hivyo vimetolewa na katibu wa chama hicho Wilaya ya Bagamoyo Mwalimu Joyce Maisa kwa niaba ya kamati ya uendeshaji na utendaji ya wilaya ya Bagamoyo akiambatana na baadhi ya wajumbe wa kamati ya uendeshaji, utendaji na kitengo cha wanawake leo (17.10.2024).

Vifaa vilivyotolewa ni pamoja viatu na mavazi mbalimbali ili ziweze kutoa nafuu katika kipindi hiki kigumu kwa wanafunzi hao.

"Sisi chama cha walimu wilaya ya Bagamoyo tulipokea kwa mshtuko mkubwa taarifa ya janga hili la moto. Tukasema ni lazima tufike kutoa chochote kwa watoto wetu maana sisi ni sehemu ya wadau wa taasisi hizi za elimu ni lazima tulie pamoja", alisema katibu huyo.


Akipokea vifaa hivyo mkuu wa shule ya Sekondari ya wasichana ya Mandera Mwalimu Regina Ngereza alikishukuru chama hicho kwa kuwakimbilia na kutoa msaada huo kwani umefika kwa wakati muafaka ambapo wao wamefarijika sana kwa kilichopatikana.

Taarifa za awali zinasema chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme ambapo moto huo uliunguza bweni na kuteketeza vifaa vyote vya wanafaunzi wapatao 111, japo wanafunzi hao walisalimika baada ya kujiokoa.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com