MADAKTARI BINGWA 77 WA RAIS SAMIA WATUA TANGA..RC BATILDA AKABIDHI MAGARI IDARA YA AFYA

Na Hadija Bagasha Tanga, 

Madaktari bingwa 77 wa Rais Samia  wamewasili Mkoani Tanga na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa Tanga Balozi Dkt. Batilda Burian,  kisha kuelekea kwenye Halmashauri 11 Mkoani humo ili  kutoa huduma mbalimbali za afya. 

Madaktari hawa watatoa huduma mbalimbaliz zikiwemo huduma za madaktari bingwa wa watoto, usingizi,  upasuaji,  magonjwa ya ndani,  kinywa na meno, pamoja na wauguzi bingwa ambao wamegawanyika katika makundi tofauti tofauti.

 Ujio wa madaktari hao ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya kuboresha upatikanaji wa huduma za afya nchini.

Mara baada ya kuwapokea madaktari hao Dkt. Batilda amekabidhi magari nane kwa idara ya afya ya Mkoa wa Tanga ili kuboresha utoaji wa huduma za afya katika wilaya za mkoa huo.

Hatua hiyo inatajwa kuonyesha dhamira ya serikali katika kuboresha miundombinu na upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi.

Madaktari hao watakuwepo Mkoani humo kwa muda wa wiki moja,  ambapo wanaelekea kwenye Halmashauri za Wilaya za Lushoto,  Bumbuli,  Korogwe,  Handeni,  Kilindi,  Muheza,  Mkinga na Pangani,  pamoja na Halmashauri za mji Korogwe na Handeni na jiji la Tanga. 

Mkuu wa Mkoa Tanga Balozi Dkt Batilda Burian amesema,  ujio wa madaktari hao unaotoa ishara za namna Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anavyotekeleza ahadi zake katika kuwahudumia watanzania katika nyanja tofauti. 

Naye Ofisa Programu Idara ya Afya ya uzazi,  mama na mtoto kutoka Wizara ya Afya Joachim Masunga amesema wapo madaktari bingwa wa watoto, usingizi,  upasuaji,  magonjwa ya ndani,  kinywa na meno, pamoja na wauguzi bingwa ambao wamegawanyika katika makundi tofauti tofauti. 

"Katika makundi hayo wapo wauguzi bingwa wa akina mama na watoto,  kwahiyo nina imani kupitia hatua hii ya pili ya madaktari bingwa wa Rais Samia" amebainisha Masunga. 

Akizungumza katika hafla ya kuwapokea madaktari hao,  mkuu wa Wilaya ya Korogwe Willium Mwakilema amesema wananchi huko vijijini wana uhitaji mkubwa wa huduma hivyo wawafikie na kuwapa huduma bora zinazostahiki. 

"Hii kazi ni ya wito, wananchi wetu wana uhitaji moubwa,  kwahiyo mimi niwaombe mkawahudumie vizuri wale wote mtakaowafikia ili kuweza kutatua shida mbalimbali za kiafya zinazowakabili" amesema. 

Mkoa wa Tanga una jumla ya watumishi wa afya 3837 sawa na asilimia 50 ya mahitaji ya Mkoa huo .

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post