ABDULAZIZ SAID SAKALA MWENYEKITI MPYA WA VIJANA CCM SHINYANGA MJINI




Mwenyekiti mpya UVCCM Wilaya ya Shinyanga Abdulaziz Said Sakala akizungumza baada ya kutangazwa kuwa msindi wa kwanza katika uchaguzi huo.

Na Mapuli Kitina Misalaba

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini leo Oktoba 27, 2024 wamefanya uchaguzi wa kumchagua mwenyekiti mpya wa jumuiya hiyo baada ya nafasi hiyo kuwa wazi kwa miezi minne.


Uchaguzi huo umekuja kufuatia kuondolewa kwa aliyekuwa mwenyekiti kutokana na kosa la utovu wa nidhamu.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, msimamizi wa uchaguzi ambaye ni katibu wa UWT Mkoa wa Shinyanga Bi. Habiba Musimu amesema kuwa jumla ya kura zilizopigwa ni 238, ambapo kura halali ni 232 na kura zilizoharibika ni 6.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, Halima Issa amepata kura moja (1), Daniesa Malula kura mbili (2), Azmina Amir kura mbili (2) sawa na Malula, Hamis Shija kura sita (6), Jasamila Maduhu kura 62, huku Abdulaziz Said Sakala akiibuka mshindi kwa kura 156.

Katibu wa UVCCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Naibu Katalambullah, amempongeza mwenyekiti mpya na kuahidi kushirikiana naye kwa ajili ya kuimarisha umoja wa vijana na chama kwa ujumla.

"Kuanzia sasa niko tayari kupokea maelekezo yako na kukusaidia katika majukumu yako tunakutegemea kuunganisha vijana na kusaidia ushindi katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwa maslahi ya vijana na chama cha mapinduzi," amesema Katalambullah.

Kwa upande wake, mwenyekiti mpya Abdulaziz Sakala ameahidi kuleta mabadiliko chanya ndani ya jumuiya ya vijana na kuwaunganisha vijana wote bila kujali makundi huku akiwasisitiza vijana kuchangamkia fursa za maendeleo katika Manispaa ya Shinyanga.

"Nawaomba vijana wenzangu tushikamane kwa umoja na mshikamano tutumie fursa zinazotokea ili kujiajiri wenyewe, hususani mikopo ya asilimia 10 iliyotolewa na serikali kwa ajili ya vijana," amesema Sakala

Uchaguzi huo ni hatua muhimu katika kuimarisha uongozi wa vijana wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini na kuendeleza juhudi za kuwakilisha maslahi ya vijana kwenye ngazi mbalimbali za serikali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post