*Mkurugenzi Mkuu asema kila mwanachama atafungua madai ‘online’
*Aahidi kuifikia sekta isiyo rasmi ili Watanzania wengi waweze kunufaika na huduma za NSSF
Na MWANDISHI WETU
MBEYA. Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) amesema Mfuko unaendelea kuboresha na kutoa huduma bora kwa wateja kwa kutumia mifumo mbalimbali ya TEHAMA, ambapo kwa sasa wanachama wanaweza kufungua madai kidijitali ‘online’ bila ya kulazimika kufika katika Ofisi za NSSF.
Amesema hatua hiyo ni njia mojawapo ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita katika kuwaondolea kero wananchi, ambapo kwa upande wa NSSF wanachama wanapata taarifa zao mbalimbali huko huko waliko jambo ambalo linawaondolea usumbufu wa kufuata huduma umbali mrefu.
Bw. Mshomba amesema hayo tarehe 7 Oktoba 2024 jijini Mbeya wakati akifungua Wiki ya Huduma kwa Wateja iliyobeba kauli mbiu isemayo ‘Huduma Bora Popote Ulipo’.
Aidha, amesema NSSF inaendelea kufikisha elimu ya hifadhi ya jamii kwa sekta isiyo rasmi ambayo imebeba kundi kubwa la Watanzania kama wakulima, wafugaji, wavuvi, wachimbaji wadogo wa madini na wajasiriamali wengine ili waweze kujiunga na kujiwekea akiba kwa maisha bora ya sasa na ya baadaye.
Bw. Mshomba amewahakikishia wateja kuwa NSSF iko imara na endelevu katika kutoa huduma za hifadhi ya jamii hususan kupitia majukumu ya msingi ambayo ni kuandikisha wanachama, kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao. Hivi sasa thamani ya Mfuko imefikia trilioni 8.5.
“Natumia fursa hii kuwashukuru wateja, watumishi wenzangu, Bodi ya Wadhamini, Benki Kuu ya Tanzania, Ofisi ya Waziri Mkuu hawa wote wamekuwa wadau muhimu katika kufanikisha utoaji wa huduma zetu,” amesema Bw. Mshomba.
Amesema mafanikio makubwa ambayo NSSF imeyapata yamechangiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye katika uongozi wake amefungua nchi na kumekuwa na ongezeko kubwa la waajiri kutokana na mazingira mazuri aliyoweka.
Naye, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Bw. Omary Mziya, amesema wanaendelea kuboresha huduma za wateja siku hadi siku kwa kuwa umuhimu wa wateja ni mkubwa na ndio sababu za kuwepo kwa NSSF.
Amesema wanachama wachangiaji wa NSSF wameongezeka kutoka 1,189,000 mwezi Juni 2023 na kufikia 1,342,654 mwezi Juni 2024. Idadi ya wanufaika wa Pensheni nao wameongezeka ambapo mpaka kufikia mwezi Juni 2024 wamefikia wastaafu 31,914.
Bw. Mziya amesema wanufaika wa mafao mengine wakiwemo wa Matibabu wamefikia 207,229 mpaka kufikia Juni 2024 na kuwa idadi ya waajiri imeongezeka na kufikia 41,616.
Amesema wanufaika wa Mafao ya Uzazi mpaka kufikia Juni 2024 walikuwa 10,809, wanufaika wa Mafao ya Kupoteza Ajira mpaka kufikia Juni 2024 walikuwa ni 109,286. “Hivyo utaona idadi ya wateja wetu imekuwa ikiongezeka siku hadi siku na sisi kipaumbele chetu ni kuendelea kutoa huduma bora na kuongeza idadi ya wanachama wengi zaidi,” amesema Bw. Mziya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Ekwabi Mujungu ameahidi kuwa wafanyakazi wataendelea kusikiliza wateja, kutoa huduma za kipekee, kuwasiliana kwa uwazi, kujitolea kwa wateja kwa maana ya kuvaa viatu vyao, kujifunza na kuboresha huduma kila siku, lengo ni kupunguza malalamiko.
Naye Robert Kadege, Meneja wa Huduma kwa Wateja, amesema Wiki ya Huduma kwa Wateja ilianza kuadhimishwa rasmi mwaka 1987 kwa lengo la kutambua umuhimu wa huduma bora kwa wateja pamoja na wafanyakazi wanaotoa huduma bora kwa wanachama.
Amesema NSSF inatumia wiki hii kwa ajili ya kukumbushana umuhimu wa huduma bora kwa wateja na kuwashukuru kwa namna ambavyo wanaunga mkono juhudi mbalimbali za NSSF ambapo kwa sasa imejikita katika kuboresha huduma zake kupitia mifumo ya kidijitali.
Awali, Meneja wa NSSF Mkoa wa Mbeya, Bw. Deus Jandwa amewahakikishia wateja kuwa wanaendelea kutoa huduma bora za hifadhi ya jamii, kutatua kero mbalimbali pamoja na kufikisha elimu ya hifadhi kwa sekta binafsi na sekta isiyo rasmi.
Social Plugin