DKT. MPIGAHODI: KUSIKILIZA MUZIKI INASAIDIA KUPUNGUZA MAUMIVU


Na George Mganga, SHINYANGA RRH

DAKTARI Bingwa wa Magonjwa ya Upasuaji katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga, Hamis Mpigahodi, amesema moja ya tiba ya maumivu kwa mgonjwa ni kusikiliza muziki.

Hayo ameyasema leo Oktoba 09, 2024 wakati akitoa elimu ya afya kuhusiana na namna ya kumhudumia mgonjwa mwenye maumivu kwa watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga.

Ameeleza kuwa mtu anapokuwa ana maumivu, kitendo cha kusikiliza muziki kinasaidia zaidi kumfariji na kumfanya ajisikie vizuri, tofauti na kumtenga ama kuzungumza naye vitu ambavyo vitachagiza asiwe sawa.

“Maumivu yapo ya aina mbalimbali, na mara nyingi tunashauri kumtibu mtu kulingana na aina ya maumivu aliyonayo ili kumsaidia aweze kupona.

“Yapo maumivu ambayo yanatibika kwa kwa dawa na mengine siyo kwa dawa, mfano ambayo hayahitaji dawa ni kutoa taarifa, kusikiliza muziki, taarifa ya mrejesho wa jambo nakadhalika”, ameeleza.

Vilevile, Mpigahodi amesema kuna maumivu mengine yanahitaji mtu ahudumiwe kwa kutumia dawa maalumu ambazo zinasaidia kutibu, lakini kwa kutegemeana na aina ya maumivu ambayo mtu yamempata.

Aidha, Dkt. Mpigahodi ameainisha kuwa mtu mwenye maumivu anaweza akapatwa na athari mbalimbali ikiwemo mapigo ya moyo kupanda, presha kupanda na kinga ya mwili kushuka.

Lakini pia, ameeleza maumivu huweza sababishwa na jinsia, tamaduni, umri na akieleza kuwa maumivu ya mtu yanapaswa kuheshimiwa.

“Kutofautiana kwa maumivu ya mtu isiwe sababu ya kufanya mlinganisho kwenye matibabu, kuna mtu anaweza akawa anaumia zaidi kuliko mwingine, hivyo inabidi aheshimiwe kwani tamaduni, umri, jinsia na sifa zingine zinatofautiana baina yake na mtu mwingine”, amesema.

Mpigahodi ametoa wito kwa watumishi kuwa maumivu yanahuisha kada zote za afya, hivyo ni vema ieleweke kuwa yanatofautiana na akiwaomba kuhakikisha wanawatibu wagonjwa kwa kulingana na aina ya maumivu waliyonayo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post