Katika ulimwengu wa kidijitali wa sasa, ambapo taarifa zinaweza kusambaa kwa kasi kubwa, uelewa wa usalama mtandaoni umekuwa wa lazima. Mhandisi Francis Mihayo, Meneja wa TCRA Kanda ya Kaskazini, anachukua hatua muhimu katika kuhamasisha umma kuhusu matumizi sahihi na salama ya mtandao kupitia kampeni ya "Ni Rahisi Sana."
Akiwa katika Kituo cha Redio cha Habari Maalum cha Jijini Arusha, Mhandisi Mihayo anatoa mwanga wa matumaini, akieleza jinsi kampeni hii inavyolenga kuwapa Watanzania ujuzi wa kujilinda dhidi ya hatari za mtandao. Anasisitiza kuwa kila mmoja wetu ana jukumu la kuchukua tahadhari ili kulinda taarifa zetu binafsi.
"Kampeni ya "Ni Rahisi Sana," iliyozinduliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ina lengo la kutoa elimu muhimu kuhusu hatari zinazoweza kujitokeza mtandaoni na njia za kujilinda. Sasa ni wakati wa kuchukua hatua, kujifunza, na kuhakikisha kuwa tunatumia teknolojia kwa usalama. Tuchukue jukumu la kujiweka salama mtandaoni kwa pamoja, tunaweza kujenga jamii salama ya kidijitali",amesema Mhandisi Mihayo.
"Ni rahisi sana huruhusiwi kurudisha pesa yoyote inayoingia kimakosa , matapeli wanaweza kukutisha sana lakini waambie ni rahisi sana anayetakiwa kurudisha hiyo pesa ni Kampuni husika ya simu, mimi sina mamlaka ya namna hiyo", amesema Mhandisi Mihayo.
Katika kampeni hii, kuna kauli mbiu zinazosisitiza mambo mbalimbali muhimu, mfano.
Kumtambu Tapeli: Ni rahisi sana kumtambua tapeli. Watu hawa (Matapeli) mara nyingi watakupigia simu kutoka kwa namba za kawaida badala ya namba 100. Hii itawawezesha watumiaji kuwa makini na mawasiliano wanayopokea.
Kutoa Taarifa: Ikiwa unakumbana na mtu anayetaka kukutapeli, ni rahisi sana kutoa taarifa. Tuma namba ya tapeli hiyo kwenye namba 15040, ili kusaidia katika kudhibiti uhalifu mtandaoni.
Wasiliana na TCRA: Kama una malalamiko kuhusu mtoa huduma wako, au unahitaji ushauri wa kuanzisha biashara ya mawasiliano, ni rahisi sana kuwasiliana nasi. Piga namba ya bure 0800008272.
Kujua Maudhui Mabaya: Ni rahisi sana kujua maudhui mtandaoni yanayolenga kupotosha. Tunahitaji kuwa makini katika kuchambua habari tunazoziona mtandaoni.
Klabu za Kidijitali: Tunawatia moyo shule za awali, msingi, sekondari, na vyuo kuanzisha klabu za Kidijitali. Hii itasaidia vijana kujifunza na kuwa na uelewa mzuri wa teknolojia.
Kujisajili Kikoa cha DOT TZ: Ni rahisi sana kujisajili na kuanza kutumia Kikoa cha DOT TZ, na hivyo kukuza biashara mtandaoni.
Rasilimali kwa Wabunifu: Wabunifu wa TEHAMA wanaweza pia kupata rasilimali kama namba na masafa kwa ajili ya kufanya majiribio bunifu zao. Hii ni fursa kubwa kwa maendeleo ya teknolojia nchini.
Kuongeza Usalama wa Vifaa: Ni rahisi sana kuhuisha mifumo ya kifaa cha mawasiliano ili kujilinda dhidi ya udukuzi. Hakikisha unatumia toleo la kisasa ili kulinda taarifa zako.
Kujilinda na Watoto: Ni rahisi sana kuchukua tahadhari kwa watoto wetu wanapotumia mitandao. Wawape mafunzo sahihi kuhusu matumizi salama ya teknolojia.
Kuhakiki Taarifa Mtandaoni: Ni rahisi sana kutumia teknolojia kuhakiki taarifa na kujua vyanzo vya habari. Hii ni muhimu katika dunia ya habari za uongo.
Kujielimisha: Ni rahisi sana kujielimisha na kusoma zaidi kuhusu usalama mtandaoni, ili tuweze kulinda taarifa zetu.
Kampeni ya "Ni Rahisi Sana" inatoa mwanga na elimu kwa jamii kuhusu usalama mtandaoni. Ni jukumu letu sote kuhakikisha tunatumia teknolojia kwa usalama na kwamba tunawasaidia wengine kufanya vivyo hivyo.
Tuchukue hatua, tujifunze, na tushirikiane ili kujenga jamii salama ya mtandao. Ulinzi wa taarifa zetu ni jukumu letu sote!