Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DKT. NYEMBEA AIPONGEZA HOSPITALI YA RUFAA MKOA SHINYANGA KWA UTOAJI MZURI WA HUDUMA, AOMBA WATUMISHI WAPEWE MAFUNZO



Na George Mganga, Shinyanga RRH

MKURUGENZI wa Tiba Wizara ya Afya, Dkt. Hamad Nyembea ameipongeza Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Shinyanga (SRRH) kwa utoaji mzuri wa huduma kwa wananchi wanaofika kuhudumiwa.

Hayo ameyasema leo Oktoba 03, 2024 alipowasili Hospitali, kwa ajili ya kukagua mazingira na namna watumishi wanavyowajibika kutoa huduma kwa wagonjwa.

Dkt. Nyembea ameeleza kufurahishwa na huduma zinavyotolewa huku akitoa maelekezo kwa watumishi kuendelea kuwajibika ipasavyo na kurekebisha changamoto kadhaa ikiwemo suala la miundombinu.

“Naona kazi yenu ni nzuri na mnaifanya vizuri, niwapongeze kwa maana mmejitahidi.

“Muendelee kufanya kazi kwa bidii ili kuwasaidia wagonjwa wanaofika hapa kupata huduma, rekebisheni baadhi ya miundombinu ambayo haijakaa sawa ili huduma ziwe nzuri zaidi”, amesema Dkt. Nyembea.

Aidha, Dkt. Nyembea ameutaka uongozi wa Hospitali hiyo kuwezesha mafunzo kwa watumishi wake mara kwa mara ili kuwajengea uwezo pindi wanapotimiza majukumu yao ya kazi.

Ameeleza kuwa mafunzo yanaongeza uelewa zaidi, hivyo ni vema yakafanyika ili kuwasaidia watumishi kufanya kazi vizuri kwa kuzingatia maadili na miongozo hususani katika sekta ya afya.

Kwa upande wake Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali, Dkt. Yohana Bunzali, amesema watatekeleza maelekezo yaliyotolewa na Dkt. Nyembea ili kukuza zaidi ustawi wa huduma chanya na nzuri kwa wananchi wa mkoa wa Shinyanga na maeneo jirani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com