BODI YA KITAIFA YA USHAURI YA MSAADA WA KISHERIA YATEMBELEA WASAIDIZI WA KISHERIA IRINGA

Bi. Eveline Haule, Msaidizi wa Kisheria  kutoka shirikala Iringa Paralega Center akisoma taarifa ya utekelezaji Mbele ya Bodi ya Kitaifa ya Ushauri ya Msaada wa Kisheria ilipofika katika ofisi zat zilizopo Iringa Mjini maeneo ya Mwembetogwaleo 24/10/2024.

*****************

Na Lusajo Mwakabuku – WyKS Iringa

Bodi ya Kitaifa ya Ushauri ya Msaada wa Kisheria ikiwa katika kikao kazi cha Kumi kinachofanyika kwa siku mbili Mkoani Iringa imefanya ziara ya kuwatembelea watoa huduma za msaada wa kisheria waliopo Iringa Mjini na Wilaya ya Kilolo kwa lengo la kukagua utekelezaji wa majukumu yao na kubaini changamoto zao.

Bodi hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti Bwana Saulo Malauri, imefanya ziara hiyo leo tarehe 24 Oktoba, 2024 ikianzia katika Wilaya ya kilolo katika Shirika la Kilolo Paralegal Unit na kuelekea Iringa Mjini ambapo moja kati ya changamoto zilizoelezwa na watoa huduma ni muingiliano unaoonekana ni wa kimaslahi na taasisi nyingine zinazoshughulikia masuala ya Haki.

Akimtaarifu Mwenyekiti wa bodi na wajumbe wake, Bwana Manase Mhando ambaye ni Mratibu wa Shirika hilo Kilolo Paralegal Unit amesema kutokana na uhalisia kuwa mashirika ya msaada wa kisheria yanatoa msaada wa kisheria bila malipo yeyote, mara kwa mara wamejikuta katika mikwaruzano na baadhi ya taasisi na wananchi wengine ambao wanaendesha kazi za huduma za kisheria kwa malipo kwa madai kuwa wanawapunguzia wateja.

Mwenyekiti wa bodi bwana Malauri akaelezea kuwa mchanganyiko huo unaoleta msuguano unatokana na uelewa mdogo juu ya mipaka ya majukumu ambayo wasaidizi wa sheria wanatakiwa kuitambua na kushauri elimu zaidi itolewe kwa umma juu ya ukomo kitu ambacho mtoa msaada wa kisheria anakomea.

“Kinachojitokeza hapa na kusababisha huu mwingiliano ni uelewa mdogo juu ya mipaka ya utekelezaji kwamba paralegal anaanzia wapi mpaka wapi na hao wengine wanafanya nini! Naamini kuwa hili likielimishwa basi hii migogoro itakwisha kwani paralegal hawaendi Mahakamani” Alisema Mwenyekiti Mashauri.

Aidha Mwenyekiti akatumia nafasi hiyo kutoa rai kwa zile taasisi ambazo zinapenda kutumia migogoro ya wananchi kama chanzo cha mapato kitu ambacho si kizuri kwa jamii lakini pia sio tamanio la serikali na pia sio sababu zilizopelekea kuanzishwa kwa sheria hizi.

Kwa upande wake Katibu wa Bodi hiyo ambaye ni Msajili wa Watoa Huduma za Msaada wa Kisheria na pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Bi. Ester Msambazi alisema Kikao hicho cha siku mbili kilichojumuisha pia ziara ya kuwatembelea watoa huduma ambapo bodi imeshuhudia hali halisi ya utekelezaji kimekuwa na manufaa hasa katika kuelewa changamoto zinazohusiana na Msaada wa Kisheria.

“Katika ziara hii tumeweza kukutana na mambo mbalimbali ambayo yameisaidia Bodi kutambua changamoto hizo kwa kuzishuhudia zikiwemo uhitaji wa wasaidizi zaidi wa kisheria kutokana na jiografia ya maeneo husika lakini pia tumewasikia wasaidizi wakisheria wakiomba ‘refreshers course’ ili waweze kuendana na mabadiliko mbalimbali yanayotokea katika sheria na hilo ni suala ambalo tutalifanyia kazi” alisema Msajili Ester.

Aidha Msajili alisema anajipanga na timu yake kuhakikisha kuwa wanakuwa wanawatembelea wasaidizi wa kisheria nchi nzima katika maeneo yao mara kwa mara kwa lengo la kuongeza ufanisi na hivyo kupunguza mlundikano wa mashauri au migogoro ambayo yanaweza kumalizikia katika ngazi hiyo ya chini na hivyo kumpunguzia gharama mwananchi ambalo ndio lengo la uanzishwaji wa sheria hii.
Mratibu wa Shirika la Kilolo Paralegal Unit  Bwana Manase Mhando akitoa Maelezo ya utekelezaji kwa Bodi ya Kitaifa ya Ushauri ya Msaada wa Kisheria ilipofika katika ofisi za shirika zilizopo Ilula wilayanii Kilolo tarehe 24/10/2024.
Wajumbe wa Bodi na wasaidizi wa kisheria wa Kilolo Paralega Unit wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza mazungumzo patika shirika hilo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Ushauri ya Msaada wa Kisheria Bwana Saulo Malauri akifafanua jambo ikiwa ni sehemu ya ziara ya bodi hiyo kutembelea mashirika wa wasaidizi wa kisheria Mkoani Iringa

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post