CCM KIMEAHIDI KUENDELEA KUSHIRIKIANA NA ASASI ZA KIRAIA NCHINI


Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Ndugu John Mongela, amesema kuwa Serikali ya CCM itaendelea kushirikiana na ASASI za Kiraia (AZAKI) nchini na kuhakikisha zinafanya kazi zake kwa Ubora na kuzingatia misingi ya sheria na taratibu za nchi.

Ndugu Mongella amesema hayo wakati akipokea Ilani za Asasi za Kiraia ya Mwaka 2024 – 2029 leo Oktoba 12, 2024, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM Balozi Dkt. Emanuel Nchimbi katika Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam, iliyowasilishwa na Mratibu wataifa wa Mtandao watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, Wakili Onesmo Olengurumwa .

Ameongezea kuwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 - 2025 Ibara 8 imegusa vipaumbele 6 ambavyo kwa kiasi kikubwa vimetekeleza kwa asilimia kubwa vipaumbele vya Ilani ya AZAKI ya vipindi viwili vilivyopita.

Aidha ametaja kuwepo kwa vipaumbele vilivyotajwa katika Ilani hii ya AZAKI ya 2024 – 2029 ambavyo serikali ya CCM inayongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan imeishaanza kuvifanyia kazi na vingine vikiwa katika mpango kazi wake.

Baadhi ya Vipaumbele hivyo ni Suala la Katiba Mpya, Haki za Binadamu, Utawala wa Sheria na Ulinzi wa Mazingira na kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi.

Ndugu Mongella ameongezea kuwa CCM katika kuandaa Ilani yake ya Uchaguzi ya Mwaka 2025 – 2030, kitazingatia maoni ya wananchi wote zikiwemo Asasi za Kiraia, maoni ambayo yanalenga kuboresha ustawi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Pamoja na hayo amevipongeza vyama vya siasa nchini kwa kufanya kazi pamoja katika kudumisha Amani na Utulivu wa Taifa huku akikosoa baadhi ya kauli zinazotelewa na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa zenye lengo la kulifarakanisha Taifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post