Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CHUMVI DHAHABU NYEUPE ISIYO THAMINIWA DODOMA


Mtendaji wa Kijiji cha Manchali B Ladislaus Loboto 

Na Dotto Kwilasa,DODOMA

Moja ya maono ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kupanua wigo kwenye sekta ya madini kwa kuhakikisha inaweka mpango mzuri wa usimamizi wa rasilimali hii kwa manufaa ya Taifa na kwa  vizazi vijavyo.

Wakati Dodoma ikitajwa kuongoza kuwa na idadi nyingi ya Madini yakiwemo Lithium, Nikel, Chuma, Urani, Shaba na Helium,bado yapo baadhi ya madini ambayo hayapewi kipaumbele ikiwemo chumvi ambayo ipo maeneo mengi mkoani hapa bila kuwepo kwa juhudi za wadau katika kuongezea thamani ili kuwasaidia wazalishaji kujikwamua kiuchumi.

Kila mtu anafahamu Chumvi ni kiungo muhimu katika chakula,hata ukirejea kwenye maandiko matakatifu yameelezea umuhimu wa chumvi ,hii inadhihishwa katika Matayo 5:13-16,"Ninyi ni chumvi ya ulimwengu,lakini chumvi ikipoteza ladha yake, haiwezekani kuwa chumvi tena maana haifai kwa kitu chochote, ila kutupwa nje ikanyagwe na watu.

Takwimu zinaonesha uwepo wa chumvi nyingi katika mkoa huu kwenye baadhi ya maeneo ikiwemo Ilindi wilayani Bahi,Buigiri na Manchali-Wilaya ya Chamwino,Mahomanyika na Nzuguni Wilaya ya Dodoma. 

Hatua hiyo ni kutokana na Mkoa wa Dodoma kuwa kwenye Ukanda maalum wa jiolojia unaupitiwa na mabadiliko tofauti ya kijiolojia na kuufanya kuwa na orodha ya madini mengi ya aina mbalimbali kuliko Mikoa mingine yote ukifuatiwa na Mkoa wa Morogoro na Lindi.

Hii ni kwa mujibu wa tafiti mbalimbali za madini zilizofanywa na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania(GST) zimeonesha kupitia kitabu kipya cha madini yapatikanayo Tanzania.

Hata hivyo kwa miaka mingi hakuna jitihada zozote za kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani ya madini hayo kwa kuwekeza viwanda vya kuchakata kama ilivyo kwa mikoa mingine ikiwemo Kigoma-Uvinza,Pwani-Mkuranga na kwingineko ili kumaliza vilio vingi na vya muda mrefu vya Wajasiriamali hawa.

Kutokana na hayo Wajasiriamali wanaochakata madini ya Chumvi Mkoani hapa wameiomba Serikali kulielekeza Shirika la Madini la Taifa kuwekeza viwanda cha kuchakata chumvi kwenye maeneo husika ambayo yatahudumia wazalishaji wa bidhaa hiyo na kuondokana na uhaba wa soko unaopelekea umasikini.

Wamesema kuwa ikiwa Uwekezaji huo utafanikiwa utasaidia kutatua changamoto ya soko la chumvi ghafi ambalo limekuwa likiwaadhiri kwa muda mrefu na kwamba hatua hiyo itatoa fursa kwa wazalishaji wengi kuvutiwa kuzalisha kisasa .

Malunde blog imezungumza na wajasiriamali wanaozalisha chumvi wa Kijiji cha Manchali B wa Kikundi cha JITEGEMEE CHUMVI mkoani hapa kata ya Manchali wilayani Chamwino ambapo wameeleza kuwa soko la bidhaa hiyo limedorola kutokana na kukosekana kiwanda cha uchakataji na chumvi hiyo kuuzika kwa msimu .

Mwenyekiti wa kikundi hicho Sarah Daniel ameeleza kuwa kikundi hicho chenye wanachama 12 kilianza mwaka 2000 kikiwa na wanachama 28 ambapo 16 kati yao walienguliwa kutokana na kutokidhi masharti ya kikundi na kuendelea kuwa wazalishaji wanaojitegemea.

Amefafanua kuwa wamekuwa wakizalisha Chumvi magunia 40 kwa kila msimu na kwamba soko lao kwa sasa lipo minadani ambapo kilo moja ya chumvi huuzwa shilingi 500 na debe lenye kilo 20 huuzwa kwa kiasi cha shilingi 6000 hadi 7000 kulingana na uhitaji uliopo.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo,msimu wa uzalishaji madini hayo huanza mwanzoni mwa mwezi Mei hadi Novemba kupisha shughuli za kilimo kuendelea kutokana na maeneo wanayozalishia chumvi kufurika maji.

“Licha ya kuwa tunatumia teknolojia ya kienyeji kuzalisha chumvi lakini bado tunapata chumvi nyingi,tunategemea minada kuendesha biashara yetu wakati mwingine hatupati soko,uzalishaji unakuwa mkubwa lakini soko hakuna,tunaishia kuifungia chumvi,”amesisitiza.

Akieleza faida wanazopata kupitia uzalishaji wa bidhaa hiyo Mwenyekiti huyo amesema umewasaidia kujikwamua kiuchumi kwa kuwasomesha watoto ,mahitaji ya familia ikiwa ni pamoja na kuwawesha kuishi maisha ya Kidigitali kwa kujenga nyumba nzuri za kisasa zenye huduma za umeme.

Amesema,kupitia kuunda kikundi hicho wamekuwa na hadhi ya kukopesheka kupitia mikopo ya Halmashauri hali iliyowasaidia kuanzisha ujenzi wa Ofisi yao itakayo warahisishia utekelezaji wa majukumu yao.

“Chumvi hii hii imetusaidia kuishi maisha ya kidigitali,ninapozungumza hapa naonekana ni mtu anayeenda na wakati,familia yangu inaishi kisasa kwa sababu ya chumvi,nina nyumba nzuri,televisheni ya kisasa kunisaidia kujua ulimwengu ulivyo,”amesema

Naye mmoja wa wanakikundi wa JITEGEMEE CHUMVI Damaris Mchiwa ameeleza tatizo kubwa ambalo limekuwa likiwakumba wazalishaji hao wadogo wa chumvi Manchali B ni ubora wa vifungashio huku akitumia nafasi hiyo kuwaomba Shirika la kuhudumia viwanda vidogo Mkoa wa Dodoma (SIDO)kuona haya ya kuwatatulia kero hiyo.

Amesema,mara baada ya uzalishaji wa chumvi kukamilika wamekuwa wakitumia vifungashio ambavyo havina ubora na hivyo soko lao kuonekana haliendi na wakati na hivyo kutaka vifungashio vya kisasa kuongeza thamani ya bidhaa hiyo.

“Ufungashaji mbovu unapelekea chumvi yetu kuonekana ina ubora hafifu tunategemea kwamba kama tutapata soko la uhakika wa kukidhi bidhaa yetu kwenye soko tutapata wateja wengi,”amesema

Naye Phoibe Chitema ameeleza hatua za uchakataji wa chumvi hadi kukamilika kwake kuwa ni lazima kukusanya udongo wenye chumvichumvi mbugani ambapo hatua hiyo hutumia zaidi ya siku nne kisha kuichemsha na kuichuja na kuihifadhi kwenye shimo ambalo linafunikwa kwa siku tano na kupatikana chumvi halisi.

“Baada ya kukamilisha hatua zote tunaianika chumvi juani na kuiweka madini joto,utalaamu huu tumeupata kutoka kwa Afisa afya wa wilaya ili kulinda afya za watumiaji,”amesema Chitema

Hata hivyo amesema wanatamani wanawake wote wanaozalisha chumvi waungane na kuwa jeshi kubwa litakaloleta tija kiuchumi .

“Kupitia chumvi ndoa zetu zimeimarika, Wanaume wetu wanatuheshimu na kutuona wanawake wa shoka kwa sababu tunakuwa na uwezo wa kuhudumia familia,pamoja na juhudi hizi tulizofikia tunapata pia sapoti kutoka kwao ambapo wamekuwa wakiturahisishia kupata kuni za kuchemsia maji yenye chumvi kazi ambayo ni ngumu kwetu,”amesema

Kuhusu utunzaji wa mazingira ameeleza,”Tunatumia kuni kwenye uzalishaji,lakini tunachukua tahadhari ya uhifadhi mazingira,tunatumia kuni aina ya Mchamwino ambayo asili yake huota kwenye maeneo yenye Chumvichumvi,miti hiyo ni rahisi kuchipua hivyo mara baada ya kuukata huchipua tena kwa kasi,”ameeleza

Kwa upande wake Mtendaji wa Kijiji cha Manchali B Ladislaus Loboto ameeleza kuwa kama Serikali,Ofisi hiyo imekuwa karibu na kikundi hicho kuhakikisha kinajidhatiti na kuwa na uwezo wa kujiinua kiuchumi kuondokana na umasikini kwa kuwahamasisha kufungua akaunti ya kikundi na kuwa na uwezo wa kukopesheka.

Kupitia hatua hivyo amewataka wachakataji wa chumvi ambao hawapo kwenye vikundi kuungana na kuwa na vikundi vyenye nguvu ili kunufaika zaidi.

“Kijijini hapa kuna wachakataji wa chumvi wa aina mbili wa muda mfupi na wa muda mrefu kuendana na msimu,wote hawa serikali ya kijiji imeshawaelekeza kuachana na ubinafsi na kuungana ili kuwa na soko la pamoja litakalosaidia uharaka wa maendeleo,”amefafanua

Amesema mbali na kikundi hicho kuna wachakataji wa chumvi wanaojitahidi kutumia fursa za uwepo wa madini hayo Kijijini hapo lakini jitihada zao zimekuwa zikirudishwa nyuma kutokana na changamoto ya masoko.

Loboto amesema,soko la madini ya chumvi limekuwa halipatikani baada ya wanunuzi wa mali ghafi hiyo kupendelea kutumia chumvi ya viwandani ambayo imetengenezwa kwa ubora.

“Hadi hapa tulipofikia bado kuna wafanyabiashara wanaagiza chumvi nje ya nchi,hata baadhi ya kampuni zilizokuwa zikinunua chumvi kutoka kwa wazalishaji wa muda mrefu zimeacha na inasemekana kwa sasa zinaagiza chumvi kutoka nje,hii haifai lazima tuhakikishe tunaboresha mazingira ya walishaji wetu ili kuendana na soko la uhakika,”amesema.

Mbali na hayo ameeleza kuwa Ofisi yake imekuwa ikifanya juhudi ya kuwasogezea huduma ya upatikanaji madini ya joto kwa ajili ya kurutubisha chumvi na kuwa salama kwa watumiaji.

“Madini joto ni muhimu kwenye mwili wa binadamu na iwapo kutakuwa na ukosefu wa madini hayo mtu anaweza akapata madhara kwa kupata magonjwa, Wanawake wajawazito wakikosa madini haya inaweza ikasababisha watoto kuzaliwa na mtindio wa ubongo na tezi la shingo,kwa kuliona hilo tunawaelimisha wazalishaji kuchanganya madini joto kitaalamu,”ameeleza

Kutokana na hayo Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Nchangwa Marwa,amesema Tume ya madini mkoani hapa inaangalia namna ya kuwawezesha wazalishaji hao wa chumvi kuzalisha kwa tija na kuwa na soko la uhakika nje ya mkoa wa Dodoma.

Amesema hivi karibuni Tume hiyo inatarajia kufanya ziara ya kuwatembelea wachakataji hao wa Chumvi kuwapa elimu juu ya uzalishaji wa kisasa utakaokidhi sokola dunia.

Ameeleza kuwa ili kufikia hatua hiyo wafanyabiasha hao na wa maeneo mengine wanapaswa kuwa na hati na leseni rasmi inayotolewa katika ofisi za madini itakayowapa kibali cha kuuza madini hayo ya chumvi.

“Ili kuwa na leseni wanapaswa kuwa na vielelezo vitakavyosaidia kutambulika kama vile TIN number, picha za passport size, na namba ya nida,nah ii ni kwa mtu binafsi, kikundi cha watu,Kampuni, Shirika au Taasisi kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za uchimbaji wa madini,”amefafanua.

Marwa ameeleza kuwa kila mchimbaji wa madini ya Chumvi na mwenye kibali au leseni atatakiwa kufanya tathmini ya athari ya mazingira kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Mazingira kabla ya kuanza uchakataji.

Kwa mujibu wa Kaimu Meneja wa Jiolojia(GST)Maswi Solomon ameeleza kuwa mbali na Chumvi madini mengine yanayopatikana mkoani hapa na ya kimkatakati ni Lithium, Nikel, Chuma, Urani, Shaba na Helium.

Mtaalamu huyo wa madini ameyataja madini mengine ambayo yametambuliwa kuwa Muhimu kwenye matumizi ya viwanda vya ndani kuwa ni Chokaa, Jasi, Feldspar, Mfinyanzi, Quartz na Kyanite.

“Madini mengine ambayo ni ya kipekee kwa sasa yanapatikanayo Tanzania tu ambayo ni madini ya Yoderite ambayo yako katika Mlima wa Mautya Wilaya ya Kongwa Mlima ambao GST imeshauri uhifadhiwe kwa ajili ya utalii wa jiolojia ikiwemo watafiti na wanafunzi kujifunzia na kushuhudia madini hayo,”ameeleza.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule ameeleza jitihada za kutangaza fursa za madini yanayo patikana Dodoma na kuahidi kuvutia zaidi uwekezaji kupitia madini yaliyopo.

“Mwenyezi Mungu ametujaalia rasilimali hii ya madini mkakati yenye mahitaji makubwa sana Duniani," amesema

Amesema Mkoa wa Dodoma umebarikiwa kuwa na madini mkakati kwa wingi na aina tofauti tofauti, na kueleza kuwa ni lazima rasilimali hiyo ikatafsirike katika maendeleo ya wananchi wa Dodoma na Tanzania kwa ujumla na kuahidi kuongeza usimamizi zaidi kwenye uvunaji wa madini hayo ili yalete faida kwa nchi kwa kuchochea uchumi na kuendeleza sekta ya madini.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com