Chuo cha VETA ya Makete kimeshuhudia ongezeko kubwa la udahili wa wanafunzi katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, kutokana na kampeni maalum ya kuhamasisha wadau mbalimbali kufadhili wanafunzi wanaojiunga na mafunzo chuoni hapo.
Taarifa hiyo imetolewa jana, tarehe 4 Oktoba 2024 na Mkuu wa Chuo cha VETA Makete, Elisha Nkuba kwa Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, aliyezuru chuo hicho pamoja na Menejimenti ya VETA Makao Makuu kwa lengo la kukagua maendeleo yake.
Nkuba ameeleza kuwa kampeni hiyo haikuongeza tu idadi ya wanafunzi bali pia imepunguza kiwango cha wanafunzi wanaoacha masomo (dropouts).
"Wafadhili wamekuwa mabalozi katika maeneo yao, wakieneza habari kuhusu mafunzo tunayotoa na gharama zake. Hali hii imevutia watu wengi zaidi kujiunga na chuo chetu," amesema.
Mkakati wa Chuo cha VETA Makete umekuwa ni kushiriki makongamano mbalimbali na kutumia fursa ya kuzungumzia mafunzo ya ufundi stadi, pamoja na kuwaalika watu mashuhuri kwenye mahafali ili kuonesha fursa zilizopo.
Amengoza kuwa chuo kimekuwa kikishirikiana na Maafisa Maendeleo ya Jamii kupata orodha ya mashirika yanayotoa msaada kwa jamii, ili kuyafikia na kuyashawishi kufadhili wanafunzi.
Ametoa takwimu kuwa, idadi ya wanafunzi waliosajiliwa iliongezeka kutoka wanafunzi 93 mwaka 2022 (62 katika kozi za muda mrefu na 31 kozi za muda mfupi), hadi wanafunzi 286 mwaka 2023 (67 katika kozi za muda mrefu na 219 kozi za muda mfupi), na hadi kufikia sasa, Oktoba 2024 tayari idadi imefikia wanafunzi 217 mwaka (73 katika kozi za muda mrefu na 144 kozi za muda mfupi) na kuongeza kuwa matarajio idadi itaongezeka zaidi kabla ya mwisho wa mwaka.
Amewataja baadhi ya wadau walioshawishiwa na kuanza kufadhili Mafunzo kuwa ni pamoja na shirika lisilo la kiserikali la Compassion, ambalo lilifadhili wanafunzi sita (6) mwaka 2023 na wanafunzi kumi (10) mwaka 2024; Paroko wa Parokia ya Nyabula Jimbo la Iringa, Father Emily Kindole, alifadhili wanafunzi watano (5) mwaka 2023 na watatu (3) mwaka 2024 na Mbunge wa Makete, Mh. Festo Sanga, ambapo aliahidi na kutimiza ufadhili kwa wanafunzi kumi (10) mwaka 2023 na wanafunzi kumi (10) mwaka 2024.
Nkuba alieleza kuwa juhudi hizi za wadau zimekuwa muhimu katika kukuza udahili wa chuo hicho, huku wakiendelea kuwashirikisha wadau zaidi ili kuhakikisha wanafunzi wengi wanapata nafasi ya kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi.
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, amepongeza uongozi wa Chuo cha VETA Makete kwa juhudi za kuongeza udahili kupitia ushirikiano na wadau mbalimbali wanaofadhili wanafunzi.
Hata hivyo, CPA Kasore alitoa mapendekezo kadhaa ili kuendeleza mafanikio hayo ikiwemo kushirikiana zaidi na jamii katika kuwatambua watu wenye mahitaji maalum kama vile watu wenye ulemavu, yatima, na wengine walio katika mazingira magumu, ili kuwaingiza katika mafunzo ya ufundi stadi.
"Hawa nao wanahitaji kunufaika na mafunzo haya, kwani yatakuwa ni njia bora ya kuwasaidia kujikwamua kiuchumi," amesema CPA Kasore.
Pia ameshauri chuo hicho kushirikiana na mafundi mahiri kutoka maeneo mbalimbali ili kuwasaidia wanafunzi kupata mafunzo ya vitendo zaidi na uzoefu wa kazi.
“Ushirikiano na mafundi wenye ujuzi mkubwa utaimarisha ubora wa mafunzo na kuwawezesha wanafunzi kujifunza kwa undani zaidi kuhusu mazingira halisi ya kazi,” amesema.
Aidha, CPA Kasore amekihimiza Chuo cha VETA Makete kuendelea na mpango wa kurasimisha ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa Mafunzo, kwani ni hatua muhimu inayolenga kuwasaidia watu ambao tayari wanai ujuzi wa kiufundi lakini hawajapata mafunzo rasmi, ili wathaminiwe zaidi kwenye soko la ajira.
Kasore pia amesisitiza umuhimu wa kutoa mafunzo maalum kwa madereva wa bodaboda, akibainisha kuwa kundi hili linakabiliwa na changamoto nyingi za kiusalama barabarani kutokana na uhaba wa mafunzo rasmi.
Amehamasisha uongozi wa vyuo vya VETA kuanzisha au kuimarisha mafunzo kwa bodaboda ili kusaidia kupunguza ajali barabarani na kuongeza ufanisi wa sekta hiyo ya usafiri.
Ziara hiyo ya CPA Kasore ni sehemu ya mkakati wa VETA kuhakikisha vituo vyake vinatoa Mafunzo bora ya ufundi stadi kwa makundi mbalimbali, ili kuboresha ustawi wa jamii na kuongeza fursa za ajira nchini.