DAWASA YAGONGA HODI KWA WANANCHI KINONDONI WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA

Wiki ya huduma kwa mteja ikiwa inaendelea, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetembelea wateja wake katika maeneo ya Msasani, Masaki, Mwananyamala wilayani Kinondoni kwa lengo la kubadilishana nao mawazo juu ya uboreshaji huduma za maji.


Akizungumza na wateja mbalimbali, Meneja wa DAWASA Kinondoni, Ndugu Tumain Muhondwa ameahidi kuendeleza mashirikiano mazuri yaliyopo baina ya Mamlaka na wateja ili kuhakikisha huduma bora inawafikia wote kwa wakati.

"Leo tumetembelea wateja mbalimbali ambao ni Slipway Hotel, Seacliff Hotel, Ada estate na Ubalozi wa Marekani na pia wateja wa kawaida katika kata ya Mwananyamala na Kinondoni. Tumeahidi kuboresha huduma ya maji katika maeneo yao," ameeleza ndugu Muhondwa.

Muhondwa ameongeza kuwa Mamlaka imejipanga kuongeza maunganisho ya huduma ya maji na kufikia asilimia 95 ya upatikanaji wa huduma ifikapo mwaka 2025.

"Tumeadhimisha wiki ya huduma kwa wateja kwa kutembelea wateja wakubwa na wadogo, tunafahamu kuna maeneo ambayo huduma haijafika, nipende kuwahakikishia wananchi kuwa Mamlaka inafanya kazi kubwa kusogeza huduma maeneo yote kwa kuongeza vyanzo vya maji na kufanya miradi ili kila mwananchi apate huduma ya maji," ameeleza ndugu Muhondwa.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Mwananyamala na Meya wa manispaa Wilaya ya Kinondoni, ndugu Songoro Mnyonge ameishukuru DAWASA kwa huduma bora zinazotolewa na kuahidi ushirikiano wa kutosha kwa Mamlaka ili huduma izidi kuimarika.

"Nikiri kwamba DAWASA wanatoa huduma hapa kwetu, huduma ya maji tunaipata kama inavyostahiki na imechangia utulivu mkubwa kwa wananchi, tutaendelea kutoa ushirikiano kwao ili huduma iwe bora na endelevu," ameeleza ndugu Mnyonge.

Josephine Wange mkazi wa Kinondoni ameishukuru DAWASA kwa kuwafikia katika wiki ya huduma kwa mteja na kueleza kuridhishwa na huduma.

Wiki ya huduma kwa wateja inaakisi usimamizi bora na wa viwango wa huduma zitolewazo na Mamlaka kwa wateja na kaulimbiu ya mwaka huu inasema "Ni zaidi ya Matarajio."

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post