DAWASA YAONGEZA WIGO UBORESHAJI HUDUMA ZA USAFI WA MAZINGIRA

 

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeanza rasmi utoaji wa huduma ya kutibu majitaka kwa watoa huduma wa kuondosha majitaka waliosajiliwa rasmi na DAWASA katika mabwawa ya Airwing yaliyopo kata ya Kipunguni A, Dar es Salaam baada ya kukamilisha maboresho katika mabwawa hayo.

Meneja wa Huduma za Usafi wa Mazingira, Mhandisi Jolyce Mwanjee amesema DAWASA imefungua mabwawa ya Airwing kwa ajili ya kusogeza huduma kwa watoa huduma wa kuondosha majitaka ambao wamekuwa wakilazimika kwenda kumwaga majitaka katika mabwawa ya Vingunguti na Buguruni.

"Kwa sasa mabwawa haya Yana uwezo wa kutibu Lita 648,000 kwa siku hivyo kusaidia kuboresha huduma ya Usafi wa Mazingira katika eneo la kihuduma la DAWASA, hii ni baada ya kukamilisha maboresho mbalimbali katika mifumo ya kutibu majitaka" amesema

Mhandisi Mwanjee ametoa rai kwa watoa huduma ya kuondosha majitaka kuanza kutumia mabwawa hayo ili kuepusha msongamano katika mabwawa ya Vingunguti na Kurasini.

"Kwa watoa huduma wanaoondosha majitaka katika maeneo ya Ukonga, Kivule, Kitunda, Kinyerezi na kadhalika, sasa wanaweza kufika hapa ili kujipatia huduma na kupunguza umbali ambao walikuwa wakisafiri kabla hatujafungua hapa.DAWASA imejipanga kutoa huduma iliyo bora." ameeleza

Ufunguzi wa mabwawa hayo ni muendelezo wa jitihada zinazofanywa na Mamlaka katika kuboresha huduma ya Usafi wa Mazingira katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post