Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt. Philip Mpango ameweka jiwe la msingi mradi wa ujenzi na upanuzi wa Kiwanja cha ndege Tabora na kuipongeza Wizara ya Ujenzi wa kazi wanayoifanya katika mradi huo.
Akizungumza leo tarehe 9 Octoba 2024 mara baada ya kukagua na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanja cha ndege Tabora Dkt Mpango amezitaka Wizara ya Ujenzi pamoja na Wizara ya Ichukuzi kushirikiana kikamilifu ili mradi huo ukamilike kwa wakati na thamani ya fedha ionekane.
"Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Uchukuzi Mnapaswa kutambua kuwa Fedha hizi ni za wananchi hivyo zitumike vizuri kwa maendeleo ya wananchi kama ilivyokusudiwa", Amekaririwa Dkt. Mpango.
Aidha, kuhusu usalama barabarani Dkt. Mpango ametoa rai kwa madereva na watumiaji wa vyombo vya moto nchini kuhakikisha wanazingatia alama za barabarani ili kuepuka ajali na kuwaonya wanaohujumu alama za barabarani kwani hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema kuwa ukarabati na upanuzi wa kiwanja hicho umefikia asilimia 72 huku jengo la abiria likiwa na uwezo wa kuhudumia abiria 120 kwa wakati mmoja litakapokamilika.
"Mheshimiwa Makamu wa Rais, mradi huu pia unahusisha barabara ya kuruka na kutua ndege, mnara wa kuongozea ndege, barabara za maingilio na maegesho ya ndege na barabara ya kuingia katika kiwanja cha ndege, maegesho ya magari, uzio wa usalama na Kituo cha hali ya hewa", amefafanua Mhandisi Kasekenya.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kasekenya amesema Serikali itaendelea kuunganisha barabara za lami katika mikoa ya magharibi ili ifikike kwa urahisi na kuchochea shughuli za uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara na hivyo kukuza uchumi wa wananchi.
Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi, Mohamed Besta amesema kuwa ujenzi wa kiwanja hicho unatekelezwa na mkandarasi Beijing Construction Engineering Group Co, kutoka nchini China kwa gharama ya shilingi bilioni 24.6
Kiwanja cha ndege cha Tabora kilianzishwa mwaka 1940 na kimekuwa kikiboreshwa mara kwa mara na kukamilika kwake kutawezesha ndege nyingi kubwa kukitumia kiwanja hicho na kuchochea shughuli za kijamii na kiuchumi katika mkoa wa Tabora na ukanda wa magharibi kwa ujumla.
Social Plugin