Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DKT. MPANGO KUFUNGUA KONGAMANO LA JOTOARDHI AFRIKA LITAKALO FANYIKA DAR

Meneja Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mhandisi Mathew Mwangomba


Na Dotto Kwilasa, DODOMA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango anatarajiwa kuwa mgeni rasmi Kongamano la 10 la Jotoardhi Afrika (ARGeo-C10) litakalofanyika nchini Tanzania kuanzia tarehe 21-27 Oktoba, 2024 huku washiriki zaidi ya 700 wakitarajiwa kushiriki.

Meneja Mkuu wa Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC), Mhandisi Mathew Mwangomba ameyasema hayo leo Oktoba 02, 2024 jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu ufunguzi wa kongamano hilo lenye lengo la kuchagiza adhma ya Serikali ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Amesema ,"Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Kampuni ya Uendelezaji Joto Ardhi Tanzania (TGDC) pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira (UNEP) imeandaa Kongamano la 10 la Jotoardhi Afrika (ARGeo-C10) ambalo litachagiza adhma ya Serikali ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, "amesema

Ameeleza kuwa kongamano hilo lina kaulimbiu inayosema, "Kuharakisha Maendeleo ya Rasilimali za Jotoardhi katika Afrika, Masoko ya Gesi ya Ukaa na Upunguzaji wa Gesi ya Ukaa", inayosadifu adhma ya Serikali kupitia Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia.
Mhandisi Mwangomba amesema kuwa washiriki wa kongamano hilo watafaidika kwa kupata elimu na maarifa, mtandao wa kitaaluma, fursa za biashara, ziara za mafunzo, ufahamu wa sera na masoko, kukuza uwezo na kupata maarifa ya kimataifa.

"Kongamano hilo linatarajiwa kuwa na washiriki takriban 1000 kutoka nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Msumbiji, Djibouti, Newzealand, Japan, Iceland, Marekani, Canada na Saudi Arabia, " Amefafanua.

Amefafanua kuwa nishati ya jotoardhi, ni endelevu, salama na rafiki wa mazingira na ina faida nyingi ikiwa ni pamoja na uwezo wake wa kutoa umeme bila kuzalisha gesi chafu, kutoharibu mazingira na uwezo wa kutoa umeme kwa kiwango kikubwa.

"Kwa sasa TGDC imeainisha takriban maeneo 52 katika mikoa 16 nchini ambayo ina uwezo wa kuzalisha nishati ya umeme zaidi ya megawati 5,000 na nishati ya joto zaidi ya megawati 15,000. Kampuni inaendelea na miradi mitano ya kipaumbelea ambayo inalenga kuzalisha MW 200 za umeme." amema Mhandisi Mwangomba.

Mwangomba ameeleza kuwa Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) ni kampuni tanzu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambayo inamilikiwa na serikali ya Tanzania kwa 100% iliyoanzishwa tarehe 19 Desemba 2013 kwa lengo la kuendeleza rasilimali ya jotoardhi (geothermal) nchini na kuanza rasmi shughuli zake tarehe 1 Julai, 2014.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com