Elimu ya Mpiga Kura Yazidi Kuimarishwa Katika Maeneo ya Vijijini Tanzania


Na Mwandishi Wetu

Ngorongoro, Oktoba 27, 2024 – Katika juhudi za kuhakikisha ushiriki wa wananchi kwenye mchakato wa uchaguzi unaongezeka, mradi wa #MpigaKura255 unaoratibiwa na mashirika ya Haki Mwananchi na Mtanzania Foundation umeendelea kutoa elimu ya mpiga kura kwa wakazi wa maeneo ya vijijini, ukiwalenga hasa wale wa jamii za pembezoni. 

Lengo kuu la mradi huu ni kuwapa wananchi uelewa wa haki na wajibu wao ili waweze kufanya maamuzi sahihi na yenye mantiki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba 2024.

Ezekiel Ndotunti, mmoja wa watoa elimu kutoka mradi wa #MpigaKura255, ameendelea na zoezi la kutoa elimu katika kitongoji cha Maasusu, kata ya Pinyinyi, kijiji cha Pinyinyi ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro. Ndotunti amesisitiza kuwa elimu hii inawapa wananchi nafasi ya kuwa na sauti katika kuchagua viongozi wanaoweza kuwawakilisha kwa usahihi, akiwataka waone kuwa kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi ni haki na wajibu wa kila mmoja kwa maslahi ya taifa.

Katika hatua nyingine, Efrem Genge, mtoa elimu ya mpiga kura kutoka kata ya Oldonyo Sambu ambaye amepitia mafunzo maalum kutoka Haki Mwananchi na Mtanzania Foundation, alikuwa na haya ya kusema: “Leo, tarehe 26 Oktoba 2024, nimeendelea na zoezi la kutoa elimu ya mpiga kura katika kijiji cha Jema, na nimeweza kuwafikishia ujumbe huu kwa wapiga kura 58, ambapo wanawake walikuwa 27 na wanaume 31.” Genge alieleza kuwa elimu anayotoa inalenga kuwaandaa wananchi kwa ajili ya kufanya maamuzi yanayojenga jamii imara na yenye mwelekeo wa maendeleo.

Naye Sarah Laizer Mtoa Elimu ya Mpiga kura aliyewezeshwa na asasi za Haki Mwananchi na Mtanzania Foundation kutoka Kata ya Engoserosambu katika tarafa ya Sale alikuwa na haya ya kueleza “nilijengewa uwezo wa kutoa Elimu ya Mpiga kura ijumaa tarehe 25 Oktoba 2024, na haraka sana siku iliyofuata tarehe 26 Oktoba 2024 Jumamosi nilirudi kwenye kata yangu na kuanza kutoa Elimu ya Mpiga kura kwenye Kijiji cha Orkiu Juu, na kwa muda mfupi tu nimefikia wananchi 384, kati ya hao wanawake walikuwa 213 na wanaume 171. Dhamira yangu ni kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa siku tano zijazo”

Mradi wa #MpigaKura255 unalenga kuhakikisha kuwa kila mwananchi anajua na kuelewa thamani ya kura yake, huku ukisisitiza kwamba nguvu ya mabadiliko na ujenzi wa taifa la kidemokrasia iko mikononi mwa wananchi wenyewe. Kwa kutoa elimu kwa jamii za vijijini kama katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, mradi huu unapania kuleta usawa na haki kwa wananchi wote kwa kujenga jamii iliyo na mwamko wa kidemokrasia na kuwajibika kwa kutumia kura kwa uangalifu na hekima.

Kupitia elimu hii, wananchi wa Ngorongoro wanapewa fursa ya kuwa mstari wa mbele katika kuleta mabadiliko ya kidemokrasia kwa kutumia haki yao ya msingi ya kupiga kura. Zozi hili linaendana na kaulimbiu ya #MpigaKura255 na #Pigapigika, ikisisitiza kuwa ushiriki wa kila mmoja ni muhimu katika kujenga taifa bora lenye misingi ya uwazi na uwajibikaji. Haki Mwananchi na Mtanzania Foundation, kupitia mradi huu, zimedhamiria kukuza demokrasia nchini Tanzania na kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata nafasi sawa ya kushiriki katika michakato ya uamuzi wa kitaifa kwa ajili ya mustakabali bora wa nchi.






Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post