ENDELEENI KUCHUKUA TAHADHARI DHIDI YA VIRUSI VYA UKIMWI” MHE. NDERIANANGA



Na Mwandishi wetu - Dodoma

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Ummy Nderiananga ameihimiza jamii kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI nchini kwa kuendelea kuzingatia elimu inayotolewa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) ili kuunga mkono jitihada za Serikali dhidi ya mapambano hayo na kuyafikia malengo yaliyopo.

Mhe. Nderiananga ametoa wito huo wakati akitoa ufafanuzi kuhusu taarifa ya utekelezaji wa Mkakati wa Tano wa Taifa wa kudhibiti UKIMWI wa mwaka 2021/22 hadi 2025/26 iliyowasilishwa leo tarehe 21 Oktoba 2024 katika ukumbi wa Bunge, jijini Dodoma na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa tume hiyo Dkt. Jerome Kamwele katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI.

Alisema, jamii haina budi kuendelea kujilinda na kuwalinda wengine kwa kuzingatia ushauri na elimu inayotolewa ili kuhakikisha hali ya maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI nchini ipungue na kuyafikia malengo ya kuzifikia sifuri tatu ifikapo 2030.

“Suala la UKIMWI siyo la TACAIDS na Ofisi ya Waziri Mkuu peke yake, Wizara ya Afya inapambania kuboresha huduma ya mama na Mtoto, Ofisi ya Rais TAMISEMI ndio imejenga miundombinu na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewekeza Ujenzi hadi ngazi ya Kata kuna vituo Vya afya yote hii ni kusogeza huduma karibu na wananchi na uwekezaji huu tutaona matunda yake katika mapambano dhidi ya VVU,”Alieleza Mhe. Nderiananga.

Pia aliishukuru TACAIDS kwa kufanya kazi nzuri ya kuifikia jamii kwa njia ya elimu huku akiwahimiza kuendelea kuongeza nguvu kwa vijana kwani ndilo kundi linaloongoza kwa maambukizi bila kusahau ni kundi muhimu katika uzalishaji na kujiletea maendeleo.
Awali akiwasilisha taarifa kuhusu utekelezaji wa Mkakati wa Tano wa Taifa wa kudhibiti UKIMWI wa mwaka 2021/22 hadi 2025/26 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa tume hiyo Dkt. Jerome Kamwele alieleza kwamba, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi Oktoba 2024, tume hiyo imefanikiwa kuratibu kwa ufanisi utekelezaji wa mkakati katika sekta zote ndani ya Serikali na sekta binafsi, Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Taasisi za dini na wadau mbalimbali.

“Tume pia tumefanikiwa kupunguza maambukizi mapya ya VVU kutoka maambukizi 61,281 mwaka 2020 hadi maambukizi 60,000 mwaka 2023, kupungua kwa vifo vitokanavyo na UKIMWI kutoka vifo 32,639 mwaka 2020 hadi vifo 25,000 mwaka 2023 na kupungua kwa kiwango cha ubaguzi na unyanyapaa unaogokana na VVU kutokana na elimu ambayo imeendelea kutolewa kwa jamii na wadau,” alieleza Dkt. Kamwele.

Alifafanua kwamba mafanikio mengine ni pamoja na kufikia lengo la utekelezaji wa shabaha za Kimataifa 95-95-95 zinazohusu kupima na kutibu ifikapo 2026 ambapo asilimia 98 ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI (WAVIU) wameanza tiba huku utafiti ukionyesha mwelekeo mzuri wa kufikia shabaha ya asilimia 95 ya tatu inayohusu kufubaza Virusi vya UKIMWI na kusisitiza ushirikiano wa pamoja kufikia asilimia 95 ya kwanza inayohusu watu wote wanaoishi na VVU kupima na kujua hali zao.

“Serikali inaendelea kuweka mkazo katika utekelezaji wa afua zinazolenga kupunguza kasi ya maambukizi mapya ya VVU hasa makundi maalum, kuendelea kutoa elimu na kuhamasisha watu kupima kujua hali zao, kuongeza nguvu kuyafikia makundi maaalum hasa vijana, wanawake, wanaume, Watoto, watu wenye ulemavu na wanaoishi katika mazingira hatarishi,” alifafanua.

Aidha Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Mhe. Bernadeta Mushashu aliipongeza TACAIDS kwa jitihada zake ikishirikiana na wadau kuhakikisha wananchi wanafanya shughuli zao za kiuchumi wakiwa katika hali njema ya kiafya.







Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post