Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

EWURA YAWAITA WENYE MALALAMIKO WIKI YA HUDUMA KWA MTEJA

 

 

Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA),Tobietha Makafu,akieleza namna EWURA ilivyojipanga kuwahudumia wadau wake katika kipindi hiki cha Wiki ya Huduma kwa Wateja iliyoanza Oktoba 7, mwaka huu.

Na.Alex Sonna-DODOMA

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imewaita wote wenye malalamiko kuhusu huduma zinazodhibitiwa na Mamlaka hiyo kuyawasilishwa kwao ili kupatiwa ufumbuzi.

Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa EWURA, Tobietha Makafu, ameyasema hayo leo Oktoba 9,2024 jijini Dodoma, akieleza namna EWURA ilivyojipanga kuwahudumia wadau wake katika kipindi hiki cha Wiki ya Huduma kwa Wateja iliyoanza Oktoba 7, mwaka huu.

“Mathalani mtu amejenga nyumba yake, amelipia huduma ya kufungiwa umeme au maji lakini unapita muda mrefu bila kupata huduma hiyo, tunakusihi leta malalamiko hayo kwetu na sisi EWURA tutahakikisha unapata huduma hiyo kwa mujibu wa utaratibu uliopo kisheria”. Alieleza

“Lakini pia mteja anapopatiwa bili ya maji ambayo haridhiki nayo, au msoma mita anapokadiria tu bili ya maji bila kusoma mita na mteja kuwasilisha suala hilo kwa mamlaka ya maji lakini hakuweza kupata suluhu, aje EWURA, sisi tutahakikisha kuwa tunamsaidia kupata mustakabali wa suala hilo”. Amesema.

Kwa upande wa malalamiko yanayohusu mafuta, Bi. Tobietha ameeleza kuwa, inapotokea mtu ameweka mafuta na labda yakapelekea kuharibu chombo chake, na kuwasilisha suala hilo kwa msimamizi wa kituo cha mafuta na hakuweza kupata suluhu, awasiliane na EWURA ndani ya siku saba, kwani bidhaa ya mafuta inatoka haraka hivyo ni muhimu kuwasiliana nasi kwa haraka kabla mafuta yanayohusika hayajaisha ili wataalamu wa EWURA waweze kufanya uchunguzi na kumuwezeha mteja kupata haki yake.

“Katika Ofisi ya Makao Makuu ya EWURA, wateja wamepata fursa ya kuhudumiwa moja kwa moja na Mkurugenzi Mkuu, Dkt James Andilile na Wakurugenzi wa Idara mbalimbali na kwa upande wa Ofisi za Kanda, watendaji wametoka maofisini kuwafuata wadau wetu, mathalani kwa Kanda ya Magharibi, wanatoa huduma katika viwanja vya shule ya msingi Uyui mkoani Tabora hivyo tumejipanga kuhakikisha kila mwenye changamoto anapata huduma”. Amesisitiza.

Wiki ya huduma kwa wateja ina maana kubwa kwa EWURA katika kuwahudumia wateja na wadau wake na EWURA imejipanga kuhahakisha kila Mtanzania anaendelea kupata huduma bora za umeme, mafuta, gesi asilia na maji na usafi wa mazingira na pia wateja wanapaswa kuitumia wiki hiyo kupata huduma mbalimbali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com