HALMASHAURI za Mkoa wa Tanga zimetakiwa kuweka bajeti mahususi kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya utoaji wa elimu ya watu wazima ili kuondoka changamoto zilizopo katika utoaji wa elimu hiyo.
Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Saitori Steven ametoa wito huo jana kwenye kilele cha maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima na Elimu nje ya Mfumo rasmi yaliyofanyika Kimkoa, wilayani Handeni.
Amesema elimu ya watu wazima ina mchango mkubwa katika kujenga ustahamilivu na ubunifu katika kuleta mabadiliko chanya, lakini pia kupambana na mmomonyoko wa maadili kwa jamii.
"Hivyo nitoe maelekezo kwa wakurugenzi wa Halmashauri zote kuhakikisha zinatrnga bajeti mahususi kutekeleza shuhuli za elimu hiyo pamoja na elimu nje ya mfumo rasmi na kuanzisha vituo vya mfano vya programu za MKEJA na MEMKWA,
"Lakini pia Elimu ya sekondari kwa njia mbadala pamoja na Vyuo vya VETA ili kusaidia wananchi mkoani hapa kujipatia fursa za kielimu na elimu ya uzalishaji mail na kuniletea maendeleo katika jamii, kiuchumi na kisiasa" amesema.
Hata hivyo amewataka wakurugenzi hao kuzitambua takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 na kudahili wote ambao hajui kusoma, kuandika na kuhesabu ili kuanzisha vituo vya utoaji elimu kupitia programu hizo.
Ofisa Elimu ya Watu Wazima Mkoa wa Tanga Joseph Shayo amesema utoaji wa elimu ya watu wazima inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo bajeti ndogo ya utekelezaji wa shughuli za elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi.
Amesema Mkoa unaendelea kuhamasisha wadau mbalimbali kuwekeza katika programu za elimu hiyo kwa kushirikiana na Halmashauri ili kuondoa tatizo la bajeti huku ukiendelea kuhamasisha wananchi wote wajitokeze kujiunga na kujiendeleza kupitia programu za MEMKWA, MUKEJA, Elimu ya sekondari kwa njia mbadala pamoja na Vyuo vya VETA ili kujiletea maendeleo.
Shayo amebainisha kwamba asilimia ya kiwango cha kujua kusoma, kuandika na kuhedabu kwa kunfi la watu wenye umri wa miaka 15 na kuendelea ni 83 ukilinganisha na asilimia 79.8 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.
"Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi mwaka 2022 wanaume wanaongoza kwa asilimia 87.7 ukilinganisha na wanawake ambao ni asilimia 78.8" amesema.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Mussa Mwanyumbu amewataka watu wazima ambao bado hawajapata elimu waende darasani kwani itaeasaidia pia katika kusimamia elimu ya watoto wao.
"Suala la Elimu tulipe kipaumbele, wazazi tuhakikishe tunaenda darasani kupata elimu lakini pia tusimamiie vizuri watoto wasome ikiwa ni pamoja na kushirikiana na walimu kuwakagua watoto wetu' amesema.
Social Plugin