Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KAMPENI YA 'NI RAHISI SANA' : SAUTI YA WATU WENYE ULEMAVU KATIKA ULIMWENGU WA KIDIJITALI!


Wadau wanufaika wa mafunzo ya usalama mtandaoni kwa watu wenye mahitaji maalum mkoa wa Shinyanga wakiwa katika picha ya pamoja.


Na Kadama Malunde – Shinyanga

Watu wenye mahitaji maalumu wameipokea kwa shangwe kampeni ya "Ni Rahisi Sana," iliyoanzishwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). Kampeni hii ni hatua ya kihistoria inayolenga kuhimiza matumizi sahihi na salama ya mtandao, huku ikiwapa watumiaji maarifa ya kujilinda dhidi ya uhalifu mtandaoni.

Kwa kutoa fursa hii ya elimu na uelewa, TCRA inachangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha usalama na ujasiri wa watu wenye ulemavu na kuonesha kwamba kila mtu ana haki ya kutumia mtandao kwa usalama lakini pia ni hatua muhimu katika kuelekea ulimwengu wa kidigitali ulio na usawa kwa wote!.

Mkoa wa Shinyanga umepewa fursa ya mwanzo kabisa ya kufaidika na elimu hii, mafunzo ya usalama mtandaoni yalitolewa tarehe 17 Oktoba 2024 ambapo Watu wenye mahitaji maalum walifundishwa kuhusu hatari za mtandaoni na jinsi ya kujilinda, jambo ambalo limeleta matumaini na ujasiri kwa wahusika.


Kampeni ya 'Ni Rahisi Sana' ambayo ilizinduliwa Oktoba Mosi,2024 na Mkurugenzi mkuu wa TCRA Dkt. Jabiri Bakari imelenga kuwahimiza Watanzania wote wajilinde dhidi ya uhalifu mtandaoni kwani uwepo wa mazingira salama mtandaoni utawezesha kufikia malengo ya uchumi wa Kidijiti.
Mwenyekiti wa  Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Mkoa wa Shinyanga (SHIVYAWATA), Richard Mpongo (kulia anayezungumza) anasema kutokana na uelewa huu waliopewa, sasa wanaweza kutumia mtandao kwa ujasiri zaidi na kwa faida, bila hofu ya kudhurika.

“Ni muhimu sana kwa watu kama sisi kuwa na elimu hii, kwani inatupa sauti na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika jamii. Kampeni ya 'Ni Rahisi Sana' kutoka TCRA ni muhimu sana kwetu watu wenye mahitaji maalum. Sasa nina uelewa mzuri kuhusu jinsi ya kujilinda dhidi ya uhalifu mtandaoni”,anaeleza Mpongo.

Anasema amejifunza jinsi ya kuanzisha neno la siri salama, kutambua ulaghai na jinsi ya kukabili matukio ya unyanyasaji mtandaoni. 

"Ninawashukuru TCRA kwa kutuletea mafunzo haya na kwa kuhakikisha  watu wenye ulemavu hatujaachwa nyuma katika ulimwengu wa kidigitali".

"Kabla ya kupata mafunzo haya nilikuwa na wasiwasi mkubwa kuhusu kutumia mtandao. Nilikuwa na hofu ya kutokuelewa hatari zinazoweza kunikabili. Hii imenipa ujasiri zaidi kutumia mitandao ya kijamii na kuungana na watu mtandaoni. Nimeelewa jinsi ya kuripoti matukio ya unyanyasaji mtandaoni. Sasa naweza kushiriki mawazo yangu bila hofu, najihisi salama zaidi katika matumizi yangu ya mtandao",anabainisha Flora Nzelani ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Tanzania Mkoa wa Shinyanga.

Mwenyekiti wa Chama cha Viziwi Tanzania Mkoa wa Shinyanga,Flora Nzelani

Naye Katibu wa Chama cha Watu wenye Ualbino Manispaa ya Shinyanga, Masanja William anasema kupitia mafunzo hayo, amejifunza jinsi ya kujilinda dhidi ya uhalifu mtandaoni na jinsi ya kutambua hatari zinazoweza kumkabili anapotumia mtandao.

"Mafunzo haya yamekuwa na umuhimu mkubwa kwangu. Kama mtu mwenye ualbino, mara nyingi napitia changamoto za kipekee mtandaoni. Nimejifunza mbinu za kutambua ulaghai na jinsi ya kulinda taarifa zangu binafsi. Hii imenipa ujasiri zaidi kutumia mitandao ya kijamii na kushiriki mawazo yangu bila hofu.

"Mafunzo yamenisaidia sana nilikuwa nasumbuliwa na SMS za matapeli , sasa naweza kutoa taarifa kuhusu mtu anayetaka kunitapeli kwa kutuma namba yake kwenye namba 15040 ili kukomesha tabia za wezi wa mtandaoni. Yameniepusha kuingia kwenye hasara mfano nikitoa neno la Siri au kubonyeza viunganishi nisivyovijua", ameongeza.

Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Ansila Joackim Materu anaeleza kuwa, elimu ya kujilinda mtandaoni ni hatua muhimu katika kuwasaidia watu wenye ulemavu kujitambua na kujilinda dhidi ya uhalifu mtandaoni.

Amesema, kwa kuwa na uelewa mzuri wa masuala ya usalama mtandaoni, sasa wanaweza kuwasaidia watu wenye ulemavu kuelewa hatari wanazokabiliana nazo na jinsi ya kujilinda.
Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Ansila Joackim Materu 

Anaeleza kuwa, kupitia shughuli za jamii atahakikisha anatoa elimu zaidi kupitia warsha, mikutano na kampeni za uhamasishaji.

“Kama Afisa Ustawi wa Jamii, naona ni wajibu wangu kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa elimu hii. Nitashirikiana na wadau mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali ili kufanikisha kufikisha elimu hii kwa watu wengi zaidi. TCRA imeonesha njia, na sasa ni jukumu letu kuendelea na juhudi hizi ili kuhakikisha kila mtu hasa watu wenye ulemavu, wanapata taarifa na maarifa muhimu ili waweze kutumia mtandao kwa usalama Naishukuru sana TCRA kwa juhudi hizi za thamani”,ameongeza Materu.

Daniel Patrick Kapaya, Katibu wa Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Kanda ya Ziwa pia anasisitiza umuhimu wa kampeni hii akibainisha kuwa, Mafunzo hayo ni hatua muhimu katika kuhakikisha jamii inakuwa na uelewa mzuri kuhusu matumizi sahihi na salama ya mtandao.

“Watu wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto nyingi, na elimu hii inawapa nguvu na uwezo wa kujilinda dhidi ya vitendo vya uhalifu mtandaoni. Tunashukuru TCRA kwa kutambua umuhimu wa kuwaletea watu wenye ulemavu mafunzo haya, na tunatarajia kuendelea kushirikiana ili kufikia malengo haya ya maendeleo na ustawi wa jamii. Pamoja tunaweza kujenga jamii salama na yenye ushirikiano",ameongeza Kapaya.
Katibu wa SMAUJATA, Kanda ya Ziwa ,Daniel Patrick Kapaya.

“Kama SMAUJATA, tumejipanga kuendelea kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa usalama mtandaoni. Tutatumia matukio yetu ya kijamii, mikutano, na semina ili kufikisha ujumbe huu kwa watu wengi zaidi. Lengo letu sisi na TCRA ni kuhakikisha kila mwanajamii, bila kujali hali yao, anapata maarifa na uelewa wa kutosha kuhusu hatari za mtandao na jinsi ya kujilinda”,ameeleza Kapaya.

Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa Mhandisi Imelda Salum anabainisha kuwa TCRA inatekeleza majukumu yake ya kuhakikisha watumiaji wote wa mitandao wakiwemo watu wenye ulemavu wanapata huduma salama na sahihi mtandaoni.

“TCRA inatekeleza Kampeni ya 'Ni Rahisi Sana' yenye lengo la kuwahimiza watanzania wote wajilinde dhidi ya uhalifu mtandaoni. Kampeni hii inahusisha jinsi ya kutambua uhalifu mtandaoni, uonevu wa mtandaoni na matapeli. Tunatoa mafunzo juu ya kutumia nywila salama, kujilinda dhidi ya utapeli wa kifedha mtandaoni na jinsi ya kuweka mipangilio ya faragha kwenye mitandao ya kijamii”,anafafanua Mhandisi Imelda.
Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa Mhandisi Imelda Salum

Anaeleza kuwa TCRA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wanaendelea kudhibiti vitendo vya uhalifu na wanaendelea kutoa elimu ili watumiaji wote wa mtandao wanakuwa salama bila kuwaacha nyuma watu wenye ulemavu ili kuhakikisha wanapata haki sawa za usalama wa taarifa binafsi.

“ TCRA ina wajibu wa kuwalinda watumiaji wote wa mtandao na kupitia juhudi hizi, tunahakikisha watu wenye ulemavu wanaweza kutumia mtandao kwa usalama na bila wasiwasi wa kukumbana na uhalifu au ukiukwaji wa haki zao na imeendelea kutoa njia za kuripoti uhalifu na matukio ya hatari mtandaoni kama vile uonevu, udanganyifu au utapeli”,anaeleza.

“Usiruhusu kitambulisho chako cha NIDA kumsajilia mtu mwingine laini ya simu na usimpatie mtu yoyote namba ya siri (PIN) ya pesa. Kwenye masuala ya mtandao hakuna mambo ya mwili mmoja ndiyo maana kila mtu anasajili kwa kutumia namba yake ya NIDA. Hakiki namba zako kupitia *106# ”,ameeleza Mhandisi Imelda.
Meneja wa TCRA Kanda ya Ziwa Mhandisi Imelda Salum (katikati) akitoa elimu ya Usalama Mtandaoni kwa Watu Wenye Ulemavu Mkoa wa Shinyanga

Anawashauri watumiaji wa mtandao kulinda taarifa zao kwa kutumia nywila (neno la siri) thabiti akisisitiza kutumia neno la siri tofauti kwa kila akaunti.

“Pia tuwaelimishe watoto juu ya hatari zilizomo kwenye mtandao na jinsi ya kutumia mitandao ya kijamii kwa usalama. Tunza faragha yako binafsi pamoja na ile ya familia yako, epuka kuweka kwenye mtandao wa kijamii taarifa binafsi kwa kina. Achana na mambo ya kuweka kila kitu chako mtandaoni, kuweka taarifa zako nyingi mtandaoni ni hatari”,ameongeza Mhandisi Imelda.

“Ni rahisi sana kumtambua tapeli kwani atakupigia namba ya kawaida badala ya namba 100, Ni rahisi sana kutoa taarifa kwa mtu anayetaka kukutapeli tuma namba yake kwenye namba 15040. Ni rahisi sana kuwasiliana na TCRA endapo una malalamiko yanayomhusu mtoa huduma wako au ukitaka kupata elimu au ushauri wa kutaka kuanzisha biashara ya mawasiliano piga namba ya bure 0800008272”, anasisitiza Mhandisi Imelda.

Anawatahadharisha watumiaji wa mtandao kuwa makini wanapotuma pesa kwa kuhakiki namba na kuwa na taarifa sahihi za mtu unayemtumia pesa.

“Punguza uharaka unapotuma pesa, hakiki namba unayotaka kuitumia pesa. Kabla ya kufanya malipo au kununua bidhaa mtandaoni, hakikisha taarifa za mtu unayemlipa au tumia huduma ya wakala aliyesajiliwa. Usitume pesa kabla ya kupokea mzigo au kuwa na mawasiliano ya uhakika ili kulinda usalama wa pesa zako, usiwe na haraka”,anasema.

“Epuka kufungua fungua, kubofya viunganishi (links) usivyovifahamu mtandaoni, jiepushe ili kulinda taarifa zako na ukihisi akaunti yako imeingiliwa au kudukuliwa (Hacked) toa taarifa kwa jeshi la polisi”,anasema Mhandisi Imelda.

Aidha anawataka watumiaji wa mtandao kuepuka kusambaza mtandaoni maudhui yaliyokatazwa kama vile udhalilishaji, uongo, uchochezi au upotoshaji lakini pia wahakikishe kabla ya kusambaza taarifa, wajiridhishe kama ni za kweli na zimethibitishwa kutoka chanzo rasmi kama vile chombo cha habari rasmi au ukurasa rasmi wa taasisi.

“Epuka kusambaza maudhui ya ngono mtandaoni kwa sababu inaweza kusababisha madhara kwa watoto na kuharibu mahusiano. Usikubali kutuma picha za utupu hata kama unampenda kiasi gani. Lile wazo la kupiga picha za utupu, unapiga ili iweje, unazipakua, unazitunza za kazi gani? Huu ni ushetani. Tuwe makini haya mambo ni hatari usiombe yakukute mtu kasambaza picha zako za utupu”,ameongeza.

Kwa Mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) hadi kufikia Septemba 2024 kuna Watumiaji wa Intaneti wapatao Milioni 41.4 nchini Tanzania ikiwa ni ongezeko la asilimia 5 kutoka Watumiaji wa Intaneti Milioni 39.3 mwezi Juni 2024 hivyo upo umuhimu mkubwa wa kuwalinda watumiaji wa mtandao ili wawe salama.

Kampeni ya "Ni Rahisi Sana" kutoka TCRA inatoa mwanga wa matumaini kwa watu wenye ulemavu, ikiwapa uelewa na ujasiri wa kutumia mtandao kwa usalama. Hii ni hatua muhimu katika kuhakikisha jamii yetu inakuwa salama, inayojiamini, na inayoweza kushiriki kikamilifu katika ulimwengu wa kidigitali. Kwa pamoja, tunaweza kujenga jamii yenye ushirikiano na uelewa wa masuala ya usalama mtandaoni.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com