MATUNDA YA UWEKEZAJI WA BANDARI YA TANGA YAANZA KULIPA MELI YA 12 ILIYOBEBA SHEHENA YA MAGARI YATUA

Meneja wa Bandari ya Tanga Masoud Mrisha akizungumza na waandishi wa habari ambao hawapo pichani baada ya kuipokea meli iliyotoka nchini China moja kwa moja kuleta shehena ya magari kupitia kampuni ya Meli ya SeaFront Shipping Services Limited (SSS).
Afisa Uhusiano wa TPA Enock Bwigane akizungumza wakati wa mapokezi ya meli hiyo

Na Oscar Assenga,TANGA

 MATUNDA ya Uwekezaji wa Bandari ya Tanga wa Sh.Bilioni 429 uliofanywa na Serikali umeanza kulipa kutokana na maboresho makubwa na hivyo kuwezesha ongezeko kubwa la idadi ya meli zinazopitisha shehena kutoka meli 197 kwa mwaka 2022/2023 hadi kufikia meli 307 kwa mwaka 2023/2024

 Hayo yalisemwa leo na Meneja wa Bandari ya Tanga Mrisha Masoud wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuipokea meli ya XINHAITONG 50 iliyotoka nchini China moja kwa moja kuleta shehena ya magari kupitia kampuni ya Meli ya SeaFront Shipping Services Limited (SSS).

 Alisema ujio wa meli hizo kushusha magari katika Bandari hiyo inadhihirisha kwamba ufanisi mkubwa katika shughuli za kupakia na kupakua zimeimarika kutokana na maboresho hayo makubwa.


 “Lakini niseme kwamba maboresho haya pia yameleta ongezeko kubwa la ajira na hadi sasa idadi ya makampuni ya wakala wa usafirishaji katika bandari yameongezeka kutoka 32 hadi 132”Alisema

Akizungumzia kuhusu ongezeko la mapato katika Bandari hiyo alisema kwamba yameongezeka ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Bandari ilikusanya mapato ya Sh.Bilioni 16 lakini kwa mwaka 2023/2024 mapato hayo yameongezeka hadi Sh.Bilioni 18.6 ikiwa ni ongezeko la asilimia 74.1.

  “Ongezeko hilo la mapato linatokana na maboresho yaliyofanyika katika bandari ya Tanga,na ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa nchi kwa ujumla “Alisema

 Alisema kwamba maboresho haya yanaonyesha jinsi uwekezaji katika miundombinu unavyoweza kuleta matokeo chanya kwa jamii na uchumi wa Taifa.

 Hata hivyo alisema Serikali inaendelea na juhudi za kuboresha sekta ya usafirishaji ili kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa kitovu cha biashara katika eneo la Afrika Mashariki.

 Awali akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi  Mkuu wa TPA,Afisa Uhusiano wa TPA nchini Enock Bwigane amesema wan mshukuru mdau wa kampuni ya Sea Front ambaye amefanikisha kuwasili kwa meli hiyo iliyobeba shehena mchanganyiko yakiwemo magari zaidi ya 350.

 Bwigane alisema kwamba asilimia kubwa ya shehena hiyo inaelekea nje ya nchi na kuwepo kwa meli hiyo ambayo inahudumiwa kwa saa 48 tangu ifike leo alfariji inafikisha meli idadi ya meli 12 ambazo zimehudumiwa na mteja wao Kampuni ya Sea Front Shipping.

 Alisema kwamba mteja wao huyo alikuwa akifanya huduma za kibandari katika Bandari ya Dar lakini kutokana ana uwekezaji uliofanywa na Serikali wa Bilioni 429 .1 kwa awamu zote mbili kuboresha bandari ya Tanga umepelekea meli kubwa nyingi kwa shehena tofaui kuhudumiwa katika Bandari ya Tanga.

 “Huyu ni mteja mojawapo alileta meli kutoka nchini China na ambapo meli hii imefikisha idadi ya meli 12 ambazo zimeshuhudumiwa na tunapoongelea ufanisi wa mapato katika Bandari ya Tanga tunajivunia”Alisema

 Alisema  robo ya kwanza ya Julai Mosi  hadi Septemba 30 mwaka huu Bandari hiyo ilikusanya Bilioni 18.6 na Bilioni 8 katika mapato hayo zimetokana na mteja huyo ambaye amekwisha kuwezesha ujio wa meli 12 katika Bandari hiyo.

 “Tunamshukuru Rais Dkt Samia Suluhu kwa maamuzi yake ya kufanya maboresho katika Bandari zote nchini ikiwemo Bandari ya Tanga ambapouwekezaji mkubwa uliofanyika umesaidia kuongeza ufanisi katika Bandari na mapato yameongezeka na huduma ya shehena zimeongezeka kila mwaka ukiangalia kwa miaka miwili iliyopita”Alisema

Alisema shehena hiyo imeongezeka kutoka kuhudumia shehena tani 800,000 na sasa wana Milioni 1.5 na mwaka huu wanatarajia kuhudumia shehena tani Milioni 1.4 katika robo ya kwanza na wameshahudumia shehena tani  laki 3.3 .

Aidha alisema kwa hiyo wanapiga hatua kubwa kwenye kuhudumia shehena nyingi katika Bandari ya Tanga na kuhudumia shehena kwa ushoroba wa Kanda ya Kaskazini na wanafarajikia kwa mara ya kwanza kwa nchi ya DRC na Zambia mzigo mkubwa unaopita hapo ni Copper ambapo zaidi ya tani 30,000 zimehudumiwa hapo.

Alisema katika meli hiyo iliyokuja kuna mizigo mchanganyiko unakwenda Rwanda katika mchanganyiko wao na wao kama Bandari wanafarijika kwa kazi kubwa iliyofanywa na Serikali katika Bandari.

“Tunasema kwamba baada ya uwekezaji katika Bandari ya Tanga umelipa ni jambo ambalo tunamshukuru Rais Dkt Samia Suluhu na tumefarijika nasi tunamuhaidi kwamba hatutamuangusha tutafanya kazi kwa bidii na kuongeza mapato ili kuimarisha uchumi wa nchi”Alisema Bwigane

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post