MBUNGE UMMY MWALIMU ATOA PHOTOCOPY MASHINE...ATAKA SIASA SAFI, WAGOMBEA SERIKALI ZA MITAA WASICHAFUANE

Na Hadija BagashaTanga,

Mbunge wa jimbo la Tanga, Ummy Mwalimu, amewataka wagombea katika uchaguzi wa serikali za mitaa kuzingatia maadili ya uongozi na kuepuka kampeni za kuchafuana na zenye kuumizana huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana kama wanachama wa CCM baada ya uchaguzi kumalizika.

Ummy ametoa kauli hiyo wakati akikabidhi mashine ya photocopy yenye uwezo wa kufanya kazi tatu kwa wakati mmoja, pamoja na karatasi za Rim 10 kwa Katibu na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tanga zenye thamani ya shilingi milioni 3.5 mashine inayotarajiwa kusaidia kudurufu karatasi kwa haraka hususani katika kipindi hiki cha uchaguzi wa serikali za mitaa.

"Tusiende kufanya kampeni za kuchafuana baada ya uchaguzi, lazima tuendelee kuwa wamoja niwatakie kila la heri wagombea wote 181 katika mitaa 181 ya Halmashauri ya jiji la Tanga  ," alisema Ummy.

Aidha Ummy alifafanua kuhusu umuhimu wa mashine hiyo na kueleza kuwa, "Mashine hii inaweza photocopy, print, na scan document lakini pia ina uwezo wa kutoa karatasi 25 kwa dakika, na ndani ya saa moja inaweza kutoa zaidi ya karatasi 1500."

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tanga, Meja mstaafu Hamis Mkoba, amewataka wakazi wa jiji la Tanga kuhakikisha hawatenganishwi na maneno ya baadhi ya watu na badala yake amewaasa kuendelea kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika miradi mikubwa ya maendeleo ambayo amekuwa akiileta jijini humo.

 “Nitoe wito kwa wakazi wa jiji la Tanga kuhakikisha wanashirikiana katika maendeleo yanayoendelezwa na serikali chini ya Rais wetu mpendwa daktari Samia Suluhu Hassan kupitia Mbunge wetu Ummy Dkt. Samia ni mwanamama anayepigania taifa hili  na Ummy ni jicho letu katika kipindi hiki," aliongeza Mkoba.

Katibu wa CCM Wilaya ya Tanga Shaban Hamis, alimshukuru Ummy kwa msaada wa mashine hiyo, akisisitiza kuwa itarahisisha kazi za ofisi na kata.

"Mhe. Mbunge, umetuwezesha kwa kununua mashine yenye thamani ya milioni tatu na laki tano, ambayo itarahisisha kazi za uchaguzi na za chama," alisisitiza Katibu huyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post