MHE. PINDA AKUTANA NA RAIS WA BOTSWANA


Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC-SEOM), Mheshimiwa Mizengo Pinda, amekutana na Rais wa Jamhuri ya Botswana, Mheshimiwa Mokgweetsi Eric Keabetswe Masisi, katika ofisi yake jijini Gaborone. SEOM ilitumia ziara hiyo kujitambulisha kwa Mhe. Rais Masisi na kubadilishana mawazo kuhusu hali ya kidemokrasia na maendeleo nchini Botswana.

Akizungumza na Mheshimiwa Masisi, Mheshimiwa Pinda alisisitiza wajibu wa SEOM kulingana na Misingi na Mwongozo wa SADC kuhusu Uchaguzi wa Kidemokrasia na kuonesha utayari kwa SEOM kutekeleza jukumu la uangalizi katika uchaguzi mkuu ujao wa Botswana.

Mhe. Pinda alieleza shukrani zake kwa mapokezi mazuri aliyoyapata yeye na timu yake tangu walipowasili Botswana na kumueleza Mhe. Rais Masisi kuwa kabla ya kukutana na yeye, SEOM ilikutana na kuzungumza na wadau mbalimbali, ambao ni pamoja na Tume Huru ya Uchaguzi ya Botswana (IEC), Kamishna wa Polisi wa Botswana, Wizara ya Mambo ya Nje, viongozi wa vyama vya kisiasa, NGO, na Mabalozi wanaowakilisha Botswana na SADC.

Aliongeza kuwa timu hiyo pia inapitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ili kupata ufahamu kuhusu masuala mbalimbali yanayohusiana na uchaguzi mkuu ujao wa nchi hiyo.

Kwa upande wake, Mhe. Rais Masisi aliwakaribisha waangalizi wa SEOM na kuwahakikishia kuwa Batswana iko tayari kwa uchaguzi mkuu utakaofanyika tarehe 30 Oktoba 2024 na kuongeza kuwa Serikali ya Botswana iko tayari kushirikiana na wadau wote, ikiwa ni pamoja na waangalizi na aliwaambia SEOM kuzungumza na yeyote wanayefikiri atawasaidia kutekeleza jukumu lao la uangalizi.

“Serikali iko tayari kufanya kazi na waangalizi; nendeni mkazungumze na yeyote mnayefikiri anaweza kuwasaidia nyinyi na timu yenu kufanya kazi zenu vizuri. Botswana ni nyumbani kwa SADC; nyote mnakaribishwa hapa na fanyeni kazi yenu kwa uhuru," alisisitiza Mheshimiwa Masisi.

Alisema anaamini kuwa Tume Huru ya Uchaguzi ya Botswana (IEC) imeshirikisha wadau wote wanaohusika na uchaguzi huo mkuu, na kwamba Serikali yake ina imani kuwa kila kitu kitakuwa sawa na uchaguzi utakuwa huru, haki, na wa kuaminika, na kwamba usalama na amani vitakuwepo wakati wa uchaguzi na hata baada ya uchaguzi huo.

Aliwahakikishia wajumbe wa SEOM kuwa Serikali imetumia rasilimali zote zilizopo kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa mafanikio makubwa na alisisitiza kuwa Serikali iko tayari kutoa msaada wowote kwa SEOM pale itakapohitajika.

Septemba 2024, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa Ulinzi na Usalama ya SADC TROIKA, alimteua Mheshimiwa Pinda kuongoza Misheni ya Uangalizi wa SADC katika uchaguzi mkuu wa Botswana.

SEOM ilijumuisha maafisa kutoka Sekretarieti ya SADC, wanachama wa Taasisi ya SADC Troika kutoka Jamhuri ya Malawi, Zambia, na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Baraza la Ushauri la Uchaguzi la SADC (SEAC).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post