Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC -SEOM) nchini Botswana, Mhe. Mizengo Pinda amekutana na kuzungumza na Mwenyekiti na Uongozi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Botswana (IEC) katika mazungumzo yaliyofanyika jijini Gaborone, Botswana.
Mhe. Pinda amekutana na kuzungumza na Mwenyekiti na Uongozi wa IEC Mhe. Jaji Barnabas Nyamadzabo na Katibu Mtendaji wa Tume hiyo Bw. Jefferson Siamisang ikiwa ni miongoni mwa viongozi na Taasisi mbalimbali ambazo SEOM inakutana nazo ili kusikiliza na kufahamu mawazo na mitazamo yao kuhusiana na masuala mbalimbali ya uchaguzi Mkuu wa Botswana uliopangwa kufanyika tarehe 30 Oktoba, 2024.
Akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa IEC Mhe. Jaji Nyamadzabo alielezea Majukumu ya Tume hiyo kama yalivyoainishwa katika Kifungu cha 65A cha Katiba ya Botswana kuwa ni Kusimamia na kuendesha uchaguzi wa Wabunge wa Bunge la Taifa na Mamlaka za Serikali za Mitaa; Kuendesha kura ya maoni; Kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa ufanisi, kwa usahihi, kwa uhuru na kwa haki; Kutoa maagizo na maelekezo kwa Katibu wa Tume kuhusiana na majukumu yao chini ya Katiba na Sheria za Uchaguzi kwa ujumla na Kutekeleza majukumu mengine yoyote kama itakavyowekwa na Sheria ya Bunge la nchi hiyo.
Alisema kuwa IEC pia inajukumu la kuandikisha wapiga kura na kudhibiti gharama za kampeni na kuongeza kuwa Tume hiyo haina mamlaka ya kuamua migogoro ya uchaguzi ambayo inapelekwa Mahakama Kuu.
Naye Katibu Mtendaji wa Tume hiyo Bw. Siamisang alieleza kuwa IEC imejipanga kikamilifu kuendesha zoezi la Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo na iko tayari kuifanya kazi hiyo kwa tija na ufanisi.
Amesema IEC tayari imeendesha zoezi la upigaji kuwa kwa diaspora wa Botswana, watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama na watumishi wa IEC lililofanyika tarehe 18 Oktoba 2024 na kuongeza kuwa IEC imeandikisha wapiga kura sawa na asilimia 80 ya lengo walilojiwekea katika zoezi lililofanyika kwa awamu tatu ikiwa ni ongezoko la asilimia Saba kutoka kwa wapiga kura wa mwaka 2019 walipofanya uchaguzi mkuu.
“IEC imeshaendesha zoezi la kupiga kura kwa hatua ya kwanza, zowezi hilolimehusisha diaspora wetu tuliowaandikisha, vyombo vya ulinzi na usalama n ahata awatumishi wa Tume, nikuhakikishie kuwa tumejipanga na tuko tayari kusimamia na kuendesha zoezi la uchaguzi kwa ufanisi, kila kitu kiko tayari na wahudumu wetu pia wako tayari kwa ujumla maandalizi yamekamilika tunasubiri tu siku ya kupiga kura,” alisema
Akizungumza baada ya kupokea taarifa ya Tume hiyo ya IEC, Mkuu wa misheni ya Uangalizi ya SADC -SEOM Mhe. Mizengo Pinda ameishukuru IEC kwa kukutana nao na kuwalezea jinsi walivyojipanga kuendesha zoezi zima la uchaguzi.
Mhe. Pinda alieleza kuwa SEOM wanajukumu la kuangalia namna uchaguzi huo unavyoeendeshwa ikiwa ni sehemu ya kukuza na kuendeleza demokrasia katika ukanda a wa SADC.
Amesema SEOM imepeleka waangalizi katika wilaya na majiji yote ya Botswana ili kuangalia zoezi zima kabla ya uchaguzi, siku ya uchaguzi na baada ya uchaguzi jinsi itakavyokuwa na inatarajia kutoa taarifa ya awali kuhusu hali ilivyokuwa tarehe 1 Novemba 2024.
Social Plugin