Na Mwandishi Wetu,MBEYA
Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma Tanzania mkoa wa Mbeya Ipyana Njiku, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuchagua viongozi bora Novemba 27, 2024 akisema hiyo ndio itakuwa dira halisi ya kuleta maendeleo nchini.
Njiku amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Mbeya kuhusu maandalizi ya chama hicho kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji baadaye Novemba 27, 2024.
"Tumeona wimbi la muamko mdogo wa watu kujitokeza kupiga kura lakini niwambie hii ni haki yetu ili kupata viongozi bora kwa maendeleo yetu", amesema Ipyana Njiku.
Pia amewataka wananchi kuwa chachu ya kutunza amani ya nchi wakati na baada ya chaguzi ili kuendelea kuwa Taifa moja na kuwaalika wenye nia na uwezo kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali.
"Haki ya kupiga kura ni silaha muhimu kwa kila raia katika kuhakikisha uongozi bora maendeleo yetu, bila kura unatoa nafasi kwa wengine kuamua nani awe kiongozi wao kwahiyo tunaomba siku ya uchaguzi tujitokeze kwa wingi kwenda kuchagua viongozi bora.
Pamoja na kupiga kura lakini hii ni fursa kwa watu wenye sifa, dhamira safi, uadilifu na utayari kuwatumikia wananchi kwa kujitokeza kugombea kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma CHAUMMA", amesema Njiku.
Aidha amesema amewasilisha Serikalini baadhi ya mapendekezo ikiwemo zilizojitokeza kwenye uandikishaji wapiga kura ambapo kundi hasa la walemavu kutozingatiwa kuwekewa mazingira rafiki hivyo kutoa wito wa kuzingatia hayo wakati wa uchaguzi wa Serikali za mitaa, vitongoji na vijiji.
Social Plugin