Na Hadija Bagasha Tanga,
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Tanga Rajab Abrahman Abdallah amewataka madereva wa vyombo vya moto kutii sheria za usalama barabarani Ili kudhibiti madhara yatokanayo na ajali za barabara ambazo zimekuwa zikigharimu maisha ya watu.
Mwenyekiti Rajab ametoa rai hiyo kwenye hafla ya kuwakabidhi vyeti vya kuhitimu mafunzo ya udereva daraja la tatu Kwa madereva 600 wa vyombo vya moto Jijini Tanga iliyofanyika katika stendi ya daladala eneo la Ngamiani Jijini Tanga.
Alisema kuwa sheria za usalama barabara zimewekwa sio Kwa ajili ya kumuonea mtu bali Kwa ajili ya kulinda usalama wa watumiaji wengine wa barabara na kudhibiti uzembe unaosababisha ajali.
"Leo tunawakabidhi madereva hawa vyeti wakiwa wamehitimu na Sasa wapo tayari kuendelea na shughuli zao za kuendesha vyombo vya moto hivyo hatutarajii muweze kuvunja sheria Kwa kutozingatia sheria za usalama barabarani",alisema Mwenyekiti Rajab.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Tanga Balozi Dkt. Batilda Burian amesema madereva hao sasa wataepukana na adha waliyokuwa wakikutana nayo kutokana na kuendesha vyombo vya moto bila kuwa na sifa zinazotakiwa.
"Madereva hawa 600 sasa hawatasumbuliwa na mtu yeyote yule walikuwa ni madereva lakini walikosa sifa kwasababu walikuwa hawajaenda kwenye kozi ya veta kama sheria inavyosema ila sasa hivi wamefanikiwa kupitia kwa Mwenyekiti wetu wa Mkoa, ",alisisitiza Balozi Dkt. Batilda.
Mbunge wa Jimbo la Tanga Ummy Mwalimu ametumia mkutano huo kueleza mambo makubwa ambayo serikali imeyafanya chini ya Dkt Samia Suluhu Hassan katika Mkoa Tanga ikiwemo uwekezaji mkubwa katika bandari ya Tanga ambayo hivi sasa inapokea meli kubwa kutoka duniani kote.
"Niliposema nataka kuifanya Tanga kama Singapore kama nilivyoahidi na sasa meli kubwa zinatia nanga katika bandari yetu ya Tanga kutoka China na maeneo mengine duniani kote hii ndio Tanga ya Dkt Samia Suluhu Hassan tiliyokuwa tunaitaka, "alisisitiza Ummy.
"Jambo la kwanza tumuunge Mkono na kumuombea Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan nimefanya kazi na marais watatu sijawahi kuona Rais mwenye upendo, utu anayejituma na kuwapambania watanzania kama Dkt Samia Suluhu Hassan, jambo la pili twendeni tukashiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa tatehe 11 mpaka 21tunaanza zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la kudumu nawaomba sana mkajiandikishe katika mitaa yenu, "alisisitiza Ummy.