No title









Na Mwandishi Wetu, Kwanza

Mwenyekiti wa Bodi ya Parole Taifa, Balozi Khamisi Kagasheki, leo Oktoba 17,2024, amefungua kikao cha Bodi hiyo katika Hoteli ya Aden Paris, iliyopo Pasiasi, Jijini Mwanza. Kikao hiko kitadumu kwa siku mbili kuanzia leo, na lengo lake ni kujadili maombi ya wafungwa 131 kutoka katikaa mikoa 25 Tanzania Bara.




Balozi Kagasheki alisema kuwa maombi hayo yalipitia kwenye Bodi za Parole za ngazi ya mikoa kabla ya kuwasilishwa kwenye Sekretalieti ya Taifa, ambapo yameletwa kwa ajili ya kujadiliwa na Bodi ya Parole Taifa.




Balozi Kagasheki alisisitiza kuwa wajumbe wa Bodi hiyo wanajitahidi kuyapitia maombi hayo kwa kina, wakizingatia vigezo vilivyowekwa ili kubaini wafungwa wenye sifa za kunufaika na mpango wa parole.




Parole ni mchakato unaowaruhusu wafungwa kukamilisha vifungo vyao wakiwa uraiani, kwa masharti ya kuwa na tabia njema.






Kwa upande wa Kamishna wa Jeshi la Magereza Nchini, CGP Jeremiah Yoram Katungu, alieleza kuwa jukumu la Jeshi la Magereza ni kuwapokea wafungwa wenye tabia na maadili tofauti, kisha kuwabadilisha tabia kwa kuwapatia ujuzi katika nyanja za ufundi, ufugaji, kilimo, na ujasiriamali, ili waweze kutumia ujuzi huo baada ya kumaliza vifungo vyao.




Katika kikao hicho, mnufaika wa mpango wa parole, Ndg. Damian George, alitoa shukrani kwa mwenyekiti wa Bodi ya Parole Taifa na kuahidi kuwa Mwalimu kwa vijana wenzake Kwa kuwasisitiza umuhimu wa kuacha matendo yasiyo na maadili na kushirikiana na viongozi wa serikali katika kuijenga nchi yetu, alieleza mnufaika wa parole Ndg George.




Viongozi mbalimbali walioshiriki kikao hiki ni pamoja na Mhe. Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu, John Samwel Mgetta (Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Parole Taifa), Dkt. Juma Ally Malewa (Mjumbe wa Bodi), Bw. Silvester Mwakitalu (DPP), Dkt. Ahmad Makuwani (Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Serikali), Bi. Vivian Kaiza (Mwakilishi wa Kamishna wa Ustawi wa Jamii), na Bw. Francis P. Mossongo (Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais Ikulu).




Kikao hicho kimeahirishwa hadi kesho asubuhi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post