NAIBU WAZIRI PINDA ASHIRIKI KONGAMANO LA KIMATAIFA KUHUSU MIJI AUSTRIA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe, Geophrey Pinda (wa tano kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wanaoshiriki Kongamano la Kimataifa la Miji linaloendelea Jijini Vienna nchini Austria. 

***********************

Na Mwandishi Wetu

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.Geophrey Pinda anashiriki Kongamano la Kimataifa kuhusu Miji linalofanyika Vienna nchini Austria.

Kongamano hilo lililobeba kauli mbiu ya "Suluhu Bunifu kwa Miji ya Kesho” linafanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Vienna, Austria kuanzia tarehe 9 hadi 11 Oktoba 2024 na kuhusisha viongozi na wataalamu wanaohusika na masuala ya usimamizi wa ukuaji na uendelezaji miji kutoka nchi mbalimbali.

Kupitia kongamano hilo, mhe. Pinda aliwaeleza washiriki namna serikali ya Tanzania chini ya Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan inavyofanya jitihada kukuza na kuendeleza miji.

Amezitaja baadhi ya jitihada hizo kuwa, ni pamoja na uamuzi wa serikali kuhamia Dodoma, Matumizi ya Mifumo ya Kielektroniki kwenye masuala ya ardhi, Uanzishwaji Kituo cha Taifa cha Ubunifu na Mafunzo cha Taarifa za Kijiografia pamoja na maboresho mbalimbali ikiwemo ya Sera ya Taifa.

Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi ameongeza kwa kusema, kwa sasa Tanzania imeanza pia kutumia Teknolojia ya kisasa kutambua wazalishaji taka ngumu ambapo amesema Teknolojia hiyo imerahisisha namna ya kuwafikia watumiaji na ukusanyaji wa Taka ngumu.

Kwa mujibu wa mhe. Pinda, katika Jijiji la Da es salaam, tathmini inaonyesha kuwa, teknolojia hiyo imekuwa ufanisi kwa asilimia 129 (129%) katika kutambua wazalishaji na maeneo taka ngumu yanapozalishwa kwa wingi ikilinganishwa na mfumo wa kawaida uliokuwa ukitumika kuksanya taka ngumu.

Akigeukia suala la ushirikishwaji wananchi katika masuala uendelezaji miji, mhe, Pinda, amesema Tanzania imebaini michango mikubwa ya wanachi katika upangaji na uendelezaji miji ambapo wananchi hushirikishwa kikamilifu huku akibainisha kuwa, mfumo huo umeonekana kuleta tija katika upangaji na usimamizi wa miji na kutolea mfano katika Jiji la Arusha eneo la Mianzini ambapo makundi mbalilmbli ya jamii yalihusishwa na kushirikishwa katika kuandaa mpango wa uendelezaji wa eneo hilo.

‘’Wazee, vijana, wamama na viongozi wa eneo husika walishirikishwa na sauti yao kusikika.huu nao ni ubunifu mzuru unaleta suluhu kwa miji ya kesho’’. Amesema Mhe. Pinda

Amelishukuru Shirika la Kimatifa la Maendeleo ya viwanda (UNIDO) kuandaa kongamanao hilo muhimu lililowakutanisha pamoja viongozi wanaohusika na masuala ya usimamizi wa ukuaji na uendelezaji miji kushirikishana ubunifu na mbinu mpya ya uendelezaji wa miji ya kesho

Lengo la mkutano huo ni kujadili na kushirikishana juu ya Suluhu bunifu kwa miji ya kesho pamoja na kutoa fursa kwa nchi wanachama kubadilishana uzoefu kwa mustakabali endelevu wa miji kwa watu wote duniani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post