RAIS SAMIA MGENI RASMI KILELE CHA WIKI YA VIJANA MWANZA


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete.


Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha wiki ya vijana itakayofanyika kitaifa kwenye Viwanja vya Furahisha Jijini Mwanza kuanzia Oktoba 8-13, 2024 .

Aidha maashimisho hayo yataenda sambamba na Kumbukumbu ya Miaka 25 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kwenye Kanisa Katoliki la Nyakahoja Mkoani Mwanza.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete ameeleza hayo Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari na kutoa rai kwa wananchi na vijana kujitokeza kwa wingi kushiriki maadhimisho ya wiki hayo yatakayofanyika kitaifa kwenye Viwanja vya Furahisha Jijini Mwanza kuanzia Oktoba 8-13, 2024 na Kilele cha Mbio za Mwenge kitakachofanyika Uwanja wa CCM Kirumba Oktoba 14, 2024.

"Maadhimisho haya yameanza Oktoba 8, 2024,ambapo katika wiki hiyo shughuli mbalimbali zitakazo fanyika ikiwamo kongamano la fursa na kuwajengea uelewa vijana pamoja na Kongamano la kuwajengea uelewa wa fursa za ujasiriamali, ubunifu wa kidijitali katika kujifunza na kujiajiri sambamba na elimu ya Sera mpya ya maendeleo ya vijana (2007), Toleo la Mwaka 2024,"ameeleza.

Mbali na shughuli hizo amesema kutakuwa na maandamano ya amani ya vijana na kwamba jumla ya vijana 1000 watashiriki wakiwa wamebeba jumbe mbalimbali ambazo serikali itazifanyia kazi.

"Malengo ya wiki hii ni kuwakutanisha vijana kujadili fursa na changamoto zinazowakabili, kuhamasisha kushiriki katika program mbalimbali za usaidizi wa jamii kwa njia ya kujitolea, kuwawezesha vijana kupata uzoefu wa namna ya utekelezaji wa masuala ya kiuchumi na kijamii, "ameeleza

Waziri huyo pia ameeleza kuwa wiki hiyo inalenga kuwahamasisha vijana kutambua kuwa wao ni sehemu ya jamii na wenye jukumu katika kushughulikia changamoto za kijamii kama vile VVU na UKIMWI, Ukiukwaji wa haki za binadamu na watoto na kushiriki katika majukumu ya kiraia .







Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post