Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RC BURIANI ATAHADHARISHA WANANCHI WASIFANYE MAKUBALIANO YA KIMKATABA WA UNUNUZI WA ARDHI NA WENYEVITI WA MITAA SASA



Na Hadija Bagasha Tanga, 

MKUU wa mkoa wa Tanga Balozi Dkt Batilda Salha Burian, amewahadharisha wananchi Mkoani Tanga kuwa wasifanye makubaliano yoyote ya kimkataba wa ununuzi wa ardhi na wenyeviti wa mitaa ambao wanamaliza muda wao hapo kesho Oktoba 19 huku akieleza shughuli zao walizokuwa wakizifanya zitashikwa na watendaji kwenye maeneo yao.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mapema leo Balozi Dkt Batilda amesema kwa mujibu wa Sheria namba 21 ya tangazo la serikali  572 kanuni ya 22 na 571, 573 na 574 ya Julai 12 2024 Kuhusu ukomo wa viongozi hao, hawaruhisiwi kufanya jambo lolote la kimkataba wa kisheria.

Hivyo, Mkuu wa mkoa  amesema ukomo wao unafikia octoba 19 ambao ni siku saba kabla ya wagombea wa nafasi hizo hawajachukua fomu ya kugombea katika vyama vyao vya siasa zoezi litakalofanyika ifikapo Oktoba 27 mwaka huu.

"Ukomo wa madaraka yao unafikia kesho tarehe 19 octoba mwaka 2024 na wasijihusishe kwa namna yeyote na utendaji na majukumu waliyokuwa wanayatekeleza kwasababu sasa kisheria muda wao unakwisha na kufanya hivyo ni kosa, "alisistiza Balozi Dkt Batilda. 

"Wajue kwamba maamuzi watakayoyafanya leo ama waliyoyafanya jana ambayo yanakinzana na matakwa ya kiserikali,  kuingia mikataba ambayo sio ya kihalali kugawa maeneo katika maeneo ya utawala wao wakishirikiana na kamati zao za kijiji wajue kabisa tutasitisha maamuzi yao lakini na wenyewe pia tutawaweka katika vyombo vya dola vishughulike nao kwa kupata adhabu kulingana na makosa waliyoyafanya, "alibainisha Dkt Batilda.

Dkt Burian aliwataka viongozi hao kutii takwa hilo la kisheria ya mamlaka yao na wasijihusishe kwa namna yoyote ile ya utendaji na majukumu waliokuwa wakitekeleza kwasababu sasa muda wao umekwisha na kufanya hivyo ni kosa na endapo watafanya mkoa utawachukulia hatua.

Alisema Mkoa unaowajibu wa kulielekeza jambo hilo na kulishusha katika ngazi za wilaya ili viongozi hao wajue ukomo wao baada ya Wizara husika kutoa maelekezo.

"Maamuzi yoyote watakayofanya leo ama wameyafanya jana au huko nyuma ambayo yanakinzana na serikali ikiwemo kuingia mkataba isiyokuwa ya kihalali kugawa maeneo ya utawala wao wakishirikiana na wajumbe wao wajue tutasitisha maamuzi yao na tutawachukulia hatua za kisheria," alisema.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa alikutana na kufanya mkutano na viongozi wa dini kupitia baraza lao la Amani kuhamasiahana umuhimu wa kuwahamasisha waumini wao waende wakajiandikishe.

Amesema viongozi wa dini watumie majukwaa yao ya kukutana na waumini wawahamishe waende kujiandikisha lakini pia Novemba 27 wajitokeze kwenda kupiga kura kuchagua viongozi wao.

Alisema zoezi la uandikishaji lina umuhimu wa pekee kwakuwa linachagua viongozi wazuri ambao wataweza kusimamia na kuzina migogoro ya wakulima na wafugaji mkoani hapa.

Mwenyekiti wa baraza la Amani la viongozi wa dini mkoani Tanga, Sheikh Jumaa Luwuchu amesema viongozi wa dini siku zote wapo pamoja na serikali kuhakikisha nchi inapiga hatua kimaendeleo na kudumisha Amani hivyo wanaowajibu wa kuwahamasisha waumini wao waende wakajiandikishe.

Mratibu wa zoezi la uandikishaji mkoani Tanga Sebastian Masani alisema zoezi la kujiandikisha kwa mwananchi halichukui muda mrefu zaidi ya dakika mbili hivyo amewataka wananchi mkoani Tanga kutumia siku zilizobaki kwenda kujiandikisha ili wapate haki yao ya kuchagua viongozi wazuri kwa ajili ya maendeleo yao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com