REA INATEKELEZA MKAKATI WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA KWA VITENDO


-MITUNGI YA GESI (LPG) 452,445 KUSAMBAZWA KWA BEI YA RUZUKU

-KILA WILAYA KUPATA MITUNGI 3,255

-MAJIKO BANIFU 200,000 KUSAMBAZWA KWA RUZUKU YA HADI 75%

Katika kuhakikisha asilimia 80 ya Wananchi wanatumia Nishati Safi za Kupikia ifikapo Mwaka 2034, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unaendelea na jitihada mbalimbali za uelimishaji, uhamasishaji na usambazaji wa bidhaa za Nishati Safi za Kupikia katika Mikoa yote Tanzania Bara.

Hayo yameelezwa Oktoba 22, 2024 Jijini Dar es Salaam katika Kongamano la 10 la Jotoardhi Afrika (ARGeo-C10) na Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji Miradi REA, Mhandisi Emanuel Yesaya.

"Katika kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia, REA imeandaa program mbalimbali kuwezesha wananchi hasa wa maeneo ya vijijini kufikiwa na bidhaa mbalimbali za nishati safi za kupikia kwa gharama nafuu," amesema Mhandisi Yesaya.

Alisema program hiyo inahusisha usambazaji wa mitungi ya gesi ya kupikia (LPG) ya kilo 6 kwa bei ya ruzuku na kwamba kwa mwaka huu wa fedha 2024/2025 kiasi cha mitungi 452,000 inasambazwa katika Wilaya zote Tanzania Bara kwa bei ya ruzuku ya asilimia 50.

Mhandisi Yesaya vilevile alibainisha kuwa kupitia program hiyo ya REA, jumla ya majiko banifu 200,000 yatauzwa kwa bei ya ruzuku ya hadi asilimia 75 chini ya ufadhili wa Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia.

“Tupo katika maandalizi ya kuanza kusambaza majiko banifu ambapo wananchi watachangia asilimia 25; kwa sasa mradi huu upo katika hatua za uandaaji wa mikataba na watoa huduma ambapo jumla ya majiko 200,000 yatasambazwa nchi nzima,” alifafanua Mhandisi Yesaya.

Alisema Serikali inatambua umuhimu wa kulinda afya za wananchi wake sambamba na kuhifadhi mazingira ambayo kwa kiasi kikubwa yameathiriwa na matumizi ya Nishati chafu za kupikia zikiwemo kuni na mkaa na sasa mwelekeo ni kujikita katika matumizi ya Nishati Safi za Kupikia ambazo Serikali inafanya kila njia zifike kwa kila mwananchi kwa gharama anayoweza kumudu.

"Hii ni fursa adhim ambayo imetolewa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ndiye kinara wa Nishati Safi ya Kupikia kwa wananchi wake, tunatoa rai kwa Watanzania kuchangamkia fursa hii," alisema Mhandisi Yesaya.

Wakala wa Nishati Vijijini unashiriki Kongamano la 10 la Jotoardhi (ARGeo-C10) kwa kueleza mafanikio ya Serikali katika kusambaza umeme maeneo ya vijijini na sasa vitongojini, kuonyesha majiko ya kisasa yanayotumia nishati ya umeme sambamba na kutoa elimu kuhusiana na Nishati Safi za Kupikia kwa washiriki wa kongamano.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post